Na
Victor Melkizedeck AbusoWatu wa Kabila la Dinka Ngok katika jimbo la Abyei nchini Sudan wameamua kuwa wangependa kuwa raia wa nchi ya Sudan Kusini baada ya matokeo ya kura ya maoni iliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Jumapili iliyopita kutangazwa.
Kamati iliyoandaa na kusimamia kura hiyo ya maoni iliyowashirikisha tu watu wa Kabila la Dinka Ngok imetangaza kuwa asilimia 99 nukta 9 ya wakaazi wa Abyei wameamua kuwa wangependa kuwa raia wa Sudan Kusini.
Baada ya matokeo hayo kutangazwa, sherehe zinashuhudiwa katika jimbo hilo ambalo linawaniwa kati ya nchi ya Sudan na Sudan Kusini kutokana na utajiri wake wa mafuta.
Kati ya wapiga kura 64,775 waliojisajili kushiriki katika kura hiyo ya maoni, ni wapiga kura 63,433 ndio waliojitokeza kupiga kura.
Luka Biong, msemaji wa Kamati hiyo ya kura ya maoni ameliambia shirika la Habari la Ufaransa AFP kuwa ni watu 12 ndio waliopiga kura kuwa raia wa nchi ya Sudan.
Nchi za Sudan na Sudan Kusini hazitambui kura hiyo ya maoni baada ya viongozi wa nchi hizo mbili zinazowania eneo hilo lenye utajiri wa mafuta kushindwa kuafikana tarehe ya upigaji kura na ni nani wanaostahili kushiriki katika zoezi hilo.
Umoja wa Afrika pia umekosoa kufanyika kwa kura hiyo ya maoni na kusema kuwa huenda ikasababisha machafuko kati ya makabila yanayoishi katika jimbo hilo.
Viongozi wa Kabila la Dinka -Ngok wanasema kuwa waliamua kuendelea na zoezi hilo baada ya kusubiri kwa muda mrefu kupatikana kwa muafaka kati ya serikali ya Khartoum na Juba kuhusu kura hiyo ya maoni bila mafanikio.
Katika hatua nyingine, kiongozi wa Kabila lenye asili ya Kiarabu la Misseriya ambalo linasema ni sharti lishirikishwe katika upigaji kura huo linaonya kuwa litaishambulia kabila la Dinka-Ngok ikiwa litatangaza kuwa jimbo hilo liko Sudan Kusini.
Mapema juma hili, rais wa Sudan Omar Al Bashir alisema kuwa atahakikisha kuwa anapata ufumbuzi wa eneo la Abyei baada ya kuzuru Sudan Kusini wiki iliyopita na kushindwa kuafikiana na mweyeji wake Salva Kiir ni lini kura hiyo ya maoni ingefanyika.
Watu wa Abyei walistahili kupiga wanataka kuwa raia wa nchi gani wakati wenzao wa Sudan Kusini walipokuwa wanapiga kura ya kujitenga na Sudan mwaka 2011 lakini mzozo umesalia kuhusu ikiwa kabila la kuhamahama la Misseriya lishiriki katika zoezi hilo au la.