HABARI KUU ZA LEO na OSCAR SAMBA
print this page
HABARI NA Oscar Samba

Mtanzania anayetuhumiwa kwa ugaidi Kenya kizimbani

Rashid Charles Mberesero 
KWA UFUPI
Mtuhumiwa huyo ambaye pia anafahamika kwa jina la Rehani Dida alirejeshwa Nairobi kutoka Garissa alikopelekwa awali kwa ajili ya kuhojiwa baada ya kukiri kujihusisha na kundi la Al- Shabaab.
Dar/Dodoma/Nairobi. Mtanzania anayedaiwa kuhusika katika shambulizi la kigaidi lililoua watu 148 katika Chuo Kikuu cha Garissa – Kenya, Rashid Charles Mberesero, jana alifikishwa mahakamani na kuwekwa kizuizini kwa mwezi mmoja wakati polisi wakiendelea kukusanya ushahidi dhidi yake.

Mtuhumiwa huyo ambaye pia anafahamika kwa jina la Rehani Dida alirejeshwa Nairobi kutoka Garissa alikopelekwa awali kwa ajili ya kuhojiwa baada ya kukiri kujihusisha na kundi la Al- Shabaab.

Mahakama jijini Nairobi ilisema jana kuwa mtuhumiwa huyo ambaye hakutakiwa kujibu tuhuma hizo na wenzake wanne watalazimika kuwa chini ya uchunguzi mkali wa polisi kwa kipindi cha mwezi mmoja na baadaye wanaweza kusomewa mashtaka ya kuhusika katika shambulizi hilo lililoua watu hao, wengi wao wakiwa ni wanafunzi.

Haikufahamika mara moja sababu za kuamuliwa kuwekwa kizuizini kwa muda huo mbali ya taarifa kueleza kuwa ‘watashikiliwa na polisi tena katika kituo cha siri’.

Mwendesha Mashtaka, Daniel Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa Mtanzania huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano, alikuwa amepanga safari ya kuelekea Somalia kwa ajili ya kujiunga na makundi ya kigaidi.

Watuhumiwa hao ni kati ya 14 waliotiwa mbaroni hivi karibuni baada ya shambulizi hilo la kigaidi.

Mahakama hiyo pia imewaamuru washukiwa wengine kuendelea kushikiliwa na polisi kwa muda wa siku tano hadi 15.

Awali, Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa polisi walikuwa wakifuatilia kwa karibu uhusiano baina ya wale waliofanya shambulizi hilo na mfanyabiashara mmoja anayemiliki hoteli mjini Garissa. Inasemekana kuwa watu waliotekeleza shambulio hilo walikuwa wamelala katika hoteli hiyo.

Hakula chakula cha shule
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kigwe, mkoani Dodoma alipokuwa akisema Mberesero baada ya kufaulu kutoka Gonja, wamesema hakuwahi kula chakula chochote shuleni kwa kipindi cha mwezi mmoja aliokaa akisubiri kuhamishwa na kubadilishiwa mchepuo wa masomo.

Wakizungumza na mwandishi wetu shuleni hapo jana, wanafunzi wa kidato cha tano, Yoram James na Thomas Godwin, walisema siku zote alizoishi shuleni hapo alikuwa akila kwa mama lishe jirani na shule hiyo.

“Lakini alikuwa na mkarimu kwetu wakati mwingine alikuwa akitununulia maandazi ya kunywea chai,” alisema Yoram.Hata hivyo, walisema kutokana na upole wake, jinsi anavyoongea na kutumia muda mrefu msikitini, walimpa jina la Ustaadhi.

“Alikuwa akienda mjini mara kwa mara, nadhani alikuwa akiomba ruhusa kwa walimu au alikuwa akitoroka,” alisema Thomas.

Thomas alisema Rashid alikuwa akipenda kucheza mpira wa miguu kwa hiyo alitenga muda wake kwa ajili hiyo.

Uhamisho wake
Mkuu wa Shule hiyo, Ramadhan Bakari alisema ofisi ya elimu mkoa ilituma taarifa ya kuwataka wanafunzi wanaopenda kubadilisha mchepuo kuandika barua ya maombi.

“Rashid alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi watano walioomba kubadilishiwa mchepuo kutoka Sanaa kwenda Sayansi, walikubaliwa wanne akiwamo yeye,” alisema Bakari.

Hata hivyo, mwalimu huyo alisema Rashid alikuwa akihangaika ahamishiwe Shule ya Sekondari ya Bihawana, tangu aliporipoti Kigwe.

“Hatuwezi kuzungumza kuhusu tabia zake maana hapa hakuishi siku nyingi, alikuwa kama yuko njiani,” alisema.

“Aliondoka hapa shuleni kwenda Bihawana Agosti 19, mwaka jana baada ya taratibu kukamilika,” alisema.
Uvumi wasambazwa
Hofu imetanda katika maeneo mbalimbali baada ya kusambazwa ujumbe kwenye simu na mitandao ya kijamii ukidaiwa kutolewa na Umoja wa Mataifa (UN) kutahadharisha watumishi wake waepuke kukaa katika makundi makubwa na mikusanyiko katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha leo kuepuka mashambulizi ya kigaidi.

Hata hivyo, Msemaji wa UN, Usiah Ledama alikanusha umoja huo kuhusika na ujumbe huo akisema ni feki na hauna ukweli wowote.Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Diwani Athumani alisema hata kama ujumbe huo ni feki, bado Jeshi la Polisi linachukua tahadhari kuhakikisha Taifa linakuwa salama.

“Huo ujumbe uwe feki au wa kweli, lazima tuchukue tahadhari, Tanzania si kisiwa, tutakuwa salama kwa asilimia 100, kwa hiyo ulinzi unaimarishwa,” alisema.

Alisema ni lazima kila mtu awe mlinzi wa mwenzake na ahakikishe kuwa anakuwa mzalendo kwa kutoa taarifa zozote ambazo anadhani zitalisaidia Jeshi la Polisi katika ulinzi.
0 Toa maoni yako.

UTT-PID YASHIRIKI MKUTANO MKUU WA 30 WA ALAT JIJINI DAR

Naibu waziri wa TAMISEMI,Khasim Majaliwa,akipata maelezo na kusaini kitabu cha wageni kutoka kwa Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Tasisi ya Miradi na Maendeleo ya Miundombinu chini ya Wizara ya Fedha, Bw, Uli Mtebe

Na Andrew Chale wa Modewji blog

Taasisi ya Miradi na Maendeleo ya Miundombinu (UTT-PID) inayoshiriki mkutano mkuu wa miaka wa 30 wa jumuia za Serikali za Mitaa Nchini (ALAT), unaofanyika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.Mkutano huo ulioanza Aprili 8 na kutarajiwa kumalizika Aprili 11, UTT-PID imeendelea kutoa elimu na huduma za taasisi hiyo.(P.T)




Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa, Mh Hawa Ghasia, akisaini kitabu na kupata maelezo kutoka Afisa Uhusiano Mkuu wa Tasisi ya Miradi na Maendeleo ya Miundombinu (UTT-PID), Uli Mtebe, akiambatana na Afisa Masoko, Bi, Kilave Atenaka .

UTT-PID ambayo imejikita hususani katika upimaji wa viwaja na upangaji wa miji katika maeneo mbalimbali ya Nchi ikiwemo Halimashahuri ya Lindi, Bukoba, Sengerema, Bagamoyo, Chalinze, Morogoro na Halimashahuri nyingine mbalimbali za hapa Nchini.

Aidha, katika maonyesho hayo, banda la UTT-PID limeendelea kutoa elimu na huduma kwa watu mbalimbali kuhusiana na kazi zao zinazofanywa na taasisi hiyo kwa wajumbe wa ALAT na wananchi wanaotembelea banda hilo.

Pia viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia.



Naibu Waziri wanchi Tawala za Mikoa Agrey Mwanri akisaini kitabu cha wageni na kupata maelezo kutoka kwa Afisa Uhusiano Mkuu wa Tasisi ya Miradi na Maendeleo ya Miundombinu (UTT-PID), Uli Mtebe, akiambatana na Afisa Masoko, Bi, Kilave Atenaka

KAZI ZA UTT-PID

Kazi za UTT-PID ni pamoja na Utoaji huduma za ushahuri katika maeneo ya upembuzi yakinifu wa miradi mbalimbali, Uratibu wa fedha na huduma zinazohusiana katika maandalizi ya mapendekezo ya miradi kwa benki au taasisi za fedha, uteuzi wa watoa huduma kuhusiana na maandalizi ya zabuni na usimamizi wa majengo na mali ambao ni utoaji wa huduma fanisi za usimamizi wa majengo yaliyochini ya uangalizi thabiti wa taasisi.



Moja ya mradi uliofanikisha na UTT-PID wa jengo la kisasa la Ushirika Bulding lililopo, Mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam.
0 Toa maoni yako.

Baraza la mahakama kuamua adhabu ya mlipua bomu Boston

Mchoro wa picha ya Dzhokhar Tsarnaev (C) akiwa na wanasheria Miriam Conrad (L) na Judy Clarke (R) wakati kesi ikiendelea.

Baada ya kumkuta na hatia katika shambulizi la bomu katika mbio ndefu za Boston Marathon mwaka 2013 Dzhokhar Tsarnaev baraza la mahakama litachukua siku chache za mapumziko kabla ya kuamua iwapo impe hukumu ya adhabu ya kifo au kifungo cha maisha jela.

Baada ya siku mbili za mashauriano marefu na makini katika mahakama ya serikali kuu baraza la mahakama hapo Jumatano lilimkuta na hatia Tsarnaev mwenye umri wa miaka 21 kwa mashtaka yote 30 anayokabiliana nayo ikiwemo 17 ambayo yana uwezekano wa kupatiwa adhabu ya kifo. Hatua ya hukumu ya kesi hiyo inatarajiwa kuanza katika chumba hicho hicho cha mahakama wiki ijayo mjini Boston nchini Marekani.

Baraza la mahakama litatakiwa kupiga kura ya pamoja ili kutoa hukumu ya kifo kwa Tsarnaev.
Tamerlan Tsarnaev (L) na Dzhokhar Tsarnaev

Wanasheria wake walikiri kutoka mwanzo wa kesi kwamba Dzhokhar alihusika kupanga kulipua mabomu yaliyotengenezwa kienyeji kwa kutumia sufuria maalumu karibu na mstari wa kumaliza mbio zinazofanyika kila mwaka za Boston Marathon na kusababisha vifo vya watu watatu akiwemo mvulana mwenye umri wa miaka minane pamoja na kuwajeruhi 264 wengine huku watu 17 wengine wakipoteza sehemu za viungo vya mwili na wengine wengi kubaki na ulemavu wa maisha kutokana na majeraha waliyoyapata.

Lakini upande wa utetezi ulisihi kwamba kaka yake aliyekuwa na mtazamo mkali Tamerlan Tsarnaev mwenye umri wa miaka 26 alikuwa mhusika mkuu kwenye shambulizi hilo. Wakili wa utetezi Judy Clarke ambaye amefanikiwa kuwaepusha na adhabu ya kifo washukiwa wengine walioshtakiwa kwa mauaji Marekani aliliambia baraza la mahakama kwenye taarifa yake ya kufunga “kama sio Tamerlan, tukio hilo lisingetokea”.

Tamerlan Tsarnaev aliuwawa siku kadhaa baada ya milipuko ya April 15 mwaka 2013 wakati Dzhokhar alipomgonga kwa gari kwa bahati mbaya wakati ndugu hao wawili walipokuwa wanajaribu kuwakimbia polisi waliokuwa wakiwasaka kwenye maeneo yote ya Boston. Walimfyatulia risasi na kumuuwa polisi mmoja wa chuo kikuu wakati wakijaribu kuwakimbia maafisa.
Boti aliyojificha Dzhokhar huko Boston

Dzhokhar aliishi Marekani kwa muda wa muongo mmoja kabla ya tukio hilo la ufyatuaji mabomu na baadaye alipatikana akiwa amejificha ndani ya boti moja iliyoegeshwa nyuma ya nyumba kwenye eneo la wazi katika kiunga kimoja huko Boston.

Waendesha mashtaka walisema Dzhokhar aliandika maandishi yasiyosomeka vyema kuhusu shambulizi hilo ndani ya ukuta wa boti hiyo kwamba ndugu hao walijaribu kulipiza kisasi mashambulizi ya waislam yanayofanywa na Marekani katika vita vya Marekani nchini Iraq na
0 Toa maoni yako.

Iran yataka vita dhidi ya Houthi kukoma

Rais Hassa Rouhani wa Iran

Rais wa Iran Hassan Rouhani, ametoa wito wa kusitishwa kwa mashambulio dhidi ya wapiganaji wa Kihouthi nchini Yemen, akiyataja kama makosa makubwa.

Iran pia imepinga madai ya Saudi Arabia kuwa utawala wa Tehran unawapa wapiganaji hao wa Kihouthi ambao ni wa shia mafunzo ya Kijeshi.

Balozi wa Saudi Arabi mjini Tehran, alishutishwa kufika mbele ya wizara ya mambo ya nje ya Iran, kupokea rasmi malalamishi ya Iran.

Nchini Yemen, Ndege za kivita za muungano unaongozwa na Saudi Arabia, zimefanya mashambulio zaidi ya anga dhidi ya wapiganaji wa Houthi katika maeneo ya Kaskazini, Kusini na kati kati mwa Yemen.

Wapiganaji hao wa Houthi ambao wanapinga utawala wa rais Abd Rabbu Mansour Hadi, wamechukua uthibiti wa maeneo kadhaa nchini humo katika miezi ya hivi karibuni.

Akiongea mjini Tehran, rais Rouhani alitaja mashambulio hayo kama makosa makubwa.

Awali waziri wa mambo ya nje wa Marekani John kerry alionya Iran dhidi ya kuwaunga mkono wapiganaji hao wa Houthi.

Kerry aliyasema hayo baada ya Iran kutuma manuwari mbili za kijeshi katika eneo la Guba la Aden.
0 Toa maoni yako.

Marekani kuimarisha uhusiano na Cuba

Rais Barack Obama na Waziri Mkuu wa Jamaica, Portia Simpson-Miller katika mkutano wa pamoja huko Kingston, Jamaica.

Rais Barack Obama wa Marekani amesema Alhamisi kwamba atafanya uamuzi karibuni iwapo ataiondoa nchi ya kikomunisti ya Cuba kwenye orodha ya mataifa ambayo Marekani inayaona yanafadhili ugaidi.

Akiwa kwenye ziara nchini Jamaica, Bw Obama amesema kwamba wizara ya mambo ya nje imeangalia kwa kina mwenendo wa Cuba kwenye maswala ya ulimwengu na lililobaki ni pendekezo kutoka kwa washauri wake.

Kwa muda sasa, kiongozi huyo wa Marekani ameashiria kuiondoa Cuba kwenye orodha hiyo, ikiwa mojawapo ya juhudi za kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili ambao aliutangaza mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuitenga nchi hiyo kwa zaidi ya miongo mitano.

Nchi nyingine tatu ambazo Marekani imeziorodhesha kama wafadhili wa ugaidi ni Syria, Iran na Sudan. Uamuzi huo wa Bw Obama una uwezekano wa kufanyika baadaye wiki hii pale atakapokutana na rais wa Cuba, Raul Castro mjini Panama kuhudhuria kikao cha mataifa ya amerika.
0 Toa maoni yako.

John Kerry aionya Iran kuhusu Yemen

John Kerry na Javad Zarif wa Iran

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani John Kerry ameionya Iran dhidi ya hatua yake ya kuwaunga mkono wapiganaji wa Houthi wanaopambana na serikali ya Yemen.

Katika mahojiano ya Televisheni, John Kerry amesema Marekani itaiunga mkono nchi yoyote mashariki ya Kati itakayotishiwa na Iran.Iran na Marekani

Jana Iran ilituma meli mbili za kivita katika bandari ya Aden kuwaunga mkono waasi, ambao wanapambana kuudhibiti mji huo.

Marekani inaunga mkono muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia ambalo lengo lake kuu ni kuwafurusha waasi hao na kurudisha utawala wa rais Abdrabbuh Mansour Hadi ambaye alilitoroka taifa hilo mwezi uliopita.Mkutano kati ya Iran na viongozi wa mataifa sita bora duniani

Hatahivyo Iran imekana madai kwamba inawapatia usaidizi wa kijeshi waasi hao wa Houthi.

Wakati huohuo, raia wa Comoro wapatao 42 wanaoishi Yemen wamekwama nchini humo.

Balozi wa Comoro ameiomba Qatar isaidie kuwahamisha, lakini nchi hiyo imelipeleka ombi hilo kwa Saudi Arabia.

Kuna mpango sasa wa kuwahamisha Wacomoro hao kwa njia ya barabara, lakini kufanya hivyo kuna hatari zake.
0 Toa maoni yako.

Yemen: msaada wa kibinadamu wawasili kwa kiwango kidogo

Shirika la Afya Duniani (WHO) imeongeza idadi ya waathirika wa machafuko Yemen kufikia watu 643 waliuawa na 2,226 waliojeruhiwa tangu tarehe 19 Machi mwaka 2015.
REUTERS/Mohamed al-Sayaghi
Na RFI
Mapigano yameendelea kurindima katika mji wa pili wa Yemen wa Aden, kusini mwa nchi hiyo kati ya wafuasi na wapinzani wa rais Abd Rabbo Hadi Mansour, ambaye alikimbilia ukimbizini nchini Saudi Arabia.
Takriban watu 22 waliuawa Jumatano wiki hii katika mashambulizi yaliyoendeshwa na waasi wa Houthi, na wengine 70 kujeruhiwa, wengi wao wakiwa ni raia wa kawaida.

Meli za kwanza zinazobeba msaada wa kiutu zimewasili katika mji wenye bandari wa Aden. Hata hivyo msaada huo unaonekana kutowatosheleza walengwa.

Meli moja kutoka Djibouti imeweza kupakua tani 2.5 za dawa kwa ajili ya hospitali ya Aden. Huu ni msaada wa kwanza wa kibinadamu kuwasili katika mji wa Aden tangu kuanza kwa mashambulizi yanayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen.

" Msaada huo ni pamoja na dawa na vifaa vingine vinavyotumiwa hospitalini kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa na majeruhi", amesema Dk Abdullah Radman, msemaji wa Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka katika mji wa Aden.

Dk Ramdan amesema kwamba msaada huo hautoshi ikilinganishwa na idadi ya waathirika.

" Ndani ya kipindi cha siku kumi, tumepokea zaidi ya majeruhi 660. Tunahitaji msaada zaidi. Tunasubiri siku mbili zijazo tani kumi ya dawa, ambazo zitawasili kwa meli au kwa ndege", ameongeza Dk Ramdan.

" Hali ya kibinadamu ni mbaya katika mji wa Aden tangu kuanza kwa machafuko na hali hiyo inazidi kuwa mbaya", amethibitisha kwa upande wake Marie-Claire Frali, msemaji wa shirika la msalaba mwekundu duniani ICRC.

" Sehemu kubwa ya mji huo imezingirwa. Njia ya majini na angani zimefungwa. Na kutokana na mapigano yanayoendelea ni vigumu kutumia barabara. Wakaazi wa mji huo hawawezi hata kutoka nje ya nyumba zao na kwenda kununua chakula au maji. Hata hivyo, uhaba wa mafuta unaripotiwa katika mji wa Aden. Miili ya watu waliouawa imetapakaa mji mzima, huku ndugu wa marehemu wakishindwa kuchukua miili ya ndugu zao kwa ajili mazishi", ameongoza Frali.

Wengi mwa wakimbizi kutoka Yemen wamekimbilia Djibouti, na wengine nchini Saudi arabia na Somalia.

Hayo yakijiri, Marekani kupitia waziri wake wa mambo ya nje, John Kerry ameionya Iran kwa uamzi wake wa kuwaunga mkono waasi, baada ya nchi hiyo kutuma mawari zake mbili katika ghuba ya Aden.
0 Toa maoni yako.

Obama apinga ubadilishaji wa maumbile

Mwanamume aliyejibadilisha maumbile na kuwa mwanamke

Rais Barrack Obama amesema swala la kisaikolojia miongoni mwa vijana ili kubadilisha maumbile yao linafaa kukoma mara moja.

Wengi wa wanaotaka kufanyia mabadiliko ya maumbile yao ni watu wa mapenzi ya jinsia moja hasa vijana.

Mshauri mkuu katika Ikulu ya Marekani Valerie Jarrett amesema kuwa utawala wa Bwana Obama umekubali kwa kauli moja kuwa ushahidi wa kisayansi kuhusiana na maamuzi ya kujibadilisha maumbile, ni swala ambalo haliwezi kukubalika kitaaluma na kimatibabu.

Taarifa hiyo ya Obama inajiri baada ya kifo cha kijana mmoja ambaye alikuwa amebadili jinsia yake na ambaye alijitia kitanzi mwezi wa Disemba baada ya kulazimishwa kuhudhuria mabadiliko hayo ya kimaumbile.
0 Toa maoni yako.

KESI YA MWENYEKITI WA JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA NCHINI KUANZA LEO

Kesi ya kushawishi wafanyabiashara wasilipe kodi kwa serikali inayomkabili Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Johnson Minja inaanza kusikilizwa leo.

Kesi hiyo iko katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini mbele ya Hakimu Mkazi, Rebecca Mbilu ambapo leo itaanza usikilizwaji kwa mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya kesi yake.

Mshitakiwa huyo ambaye yuko nje kwa dhamana anakabiliwa na mashtaka mawili ikiwemo la kuchochea wafanyabiashara wasilipe kodi ya serikali.


Upande wa mashtaka kuiongozwa na Wakili wa Serikali, Godfrey Wambali ulidai kuwa, Septemba 6, mwaka jana wakati Minja alipokuwa katika mkutano na wafanyabiashara uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Mjini hapa mshitakiwa alitenda makosa mawili ya kushawishi wafanyabiashara wasilipe kodi na kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs).

Upande wa mashtaka ulidai kitendo alichofanya mshtakiwa ni kinyume na kifungu cha 390 kinachosomeka pamoja na kifungu cha 35 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 ni kosa kushawishi vitendo vyovyote vya jinai.

Alidai hata kifungu cha 107 kifungu kidogo cha Sheria ya kodi sura ya 332 ya mwaka 2004 ni kosa kuzuia ulipaji wa kodi kwa Serikali. Mshitakiwa alikana mashtaka hayo. Minja anatetewa na wakili wa kujitegemea Godfyey Wasonga.
0 Toa maoni yako.

MAAZIMISHO YA MIAKA 21 YA KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA KIMBARI RWANDA.



Mgeni rasmi Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dr. Harrison Mwakyembe na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Eugene Kayihura wakiwasha mishumaa maalumu kuwakumbuka raia waliouwawa katika mauaji ya Kimbari.



Mratibu Mkazi wa UN, Alvaro Rodriguez akizungumza katika Maazimisho ya Miaka 21 ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari. Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania yamefanyika jana ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.



Mgeni rasmi Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dr. Harrison Mwakyembe (wa pili kulia) akipata maelezo juu ya mwenendo wa mashauri toka ICTR mara baada ya kuwasili kwenye Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania yamefanyika jana ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam wakiwa pichani.



Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dr. Harrison Mwakyembe akizungumza na wageni waalikwa katika Maazimisho ya Miaka 21 ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari. Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania yamefanyika jana ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.



Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Eugene Kayihura akizungumza katika Maazimisho ya Miaka 21 ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari.



Mgeni rasmi Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dr. Harrison Mwakyembe na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Eugene Kayihura pamoja na meza kuu wakiwa wamesimama kimya kuwakumbuka raia waliouwawa katika mauaji ya Kimbari.



Bendera za mataifa mbalimbali zikipepea nusu mlingoti nje ya ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, kuashiria tukio la kuwakumbuka raia wa Rwanda waliouwawa mauaji ya kimbari.



Ofisa Mkuu wa Utawala wa Mahakama ya Mauji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Sarah Kilemi akizungumza katika Maazimisho ya Miaka 21 ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari.



Viongozi na mabalozi mbalimbali wakiwa katika Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania yamefanyika jana ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.



Baadhi ya wanafunzi waliohudhuria Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania yamefanyika jana ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam wakiwa pichani.



Ofisa Habari wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Stella Vuzo akitoa salamu za shukrani kwa wageni waalikwa kwenye Maazimisho ya Miaka 21 ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari. Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania yamefanyika jana ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.



Mmoja wa wageni waalikwa akitia saini katika daftari la wageni waalikwa katika Maazimisho ya Miaka 21 ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari.



Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Eugene Kayihura (kushoto) akimkaribisha Mratibu Mkazi wa UN, Alvaro Rodriguez katika Maazimisho ya Miaka 21 ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari.



Ofisa Habari wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Bi. Usia Nkhoma akizungumza katika Maazimisho ya Miaka 21 ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari.



Mwakilishi toka Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania, Lambert Sano akizungumza katika Maazimisho ya Miaka 21 ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari.



Viongozi na mabalozi mbalimbali wakiwa katika Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania yamefanyika jana ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
0 Toa maoni yako.

RADIO ZASHUKURU KWA KUPOKEA KATIBA INAYOPENDEKEZWA KWA NJIA YA SAUTI

Wasimamizi wa redio za jamii wakisikiliza kwa makini wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.



Mwenyekiti wa Mtandao wa redio za Jamii, Joseph Sekiku akiongea machache kabla ya kuwagawia wasimamizi wa redio za jamii wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.




Mkurugenzi Mkaazi wa UNESCO nchini Tanzania Bi Zulmira Rodrigez, akiwagawia wasimamizi wa redio za jamii katiba iliyopendekezwa iliwekwa kwa nji ya sauti.

Wakurugenzi na viongozi mbalimbali wa Radio za jamii wamethibitisha kupokea na kuanza kurusha Katiba Inayopendekezwa kwa njia ya sauti, makala na michezo ya radio iliyoandaliwa na Kampuni ya Focus Media na COMNETA zenye maudhui ya katiba inayopendekezwa.

Wakizungumza na Focus Media ambao ndio waandaaji na wasambazaji wamekiri kwamba wamepokea kwa wakati muafaka, kwani hawakuwa na chanzo sahihi cha kupata maudhui yanayohusu elimu ya uraia na uchaguzi mkuu na kura ya maoni.

Baadhi ya wasimamizi wa radio zilizo katika mtandao wa radio za kijamii Community Media Network of Tanzania ambao wamethibitisha kupokea vitendea kazi hivyo ni Bw. Ali Khamis Mtwana, Mkurugenzi Mtendaji wa Tumbatu Island Community Radio, Bw. Anton Masai Triple A FM Arusha, Dr. Lazaro Ole Mongoi Mkurugenzi Mtendaji wa IDEA Radio, Henry Bernard, Adelina Lweramla, Jackson Mollel, wa ORS FM Arusha, Edwin Mpokasye, Radio Fadhila Mkurugenzi Radio Kwizera- Ngara.

Vipindi vinapokuwa vikiruka hewani wasikilizaji wamekuwa wakishiriki kwa kupiga simu na kuuliza maswali ilikuelewa zaidi Katiba Inayopendekezwa.

Wengine wanapiga simu kupongeza na mnamichezo ya radio ilivyoratibiwa vizuri na ikielimisha jamii juu ya mambo mbalimbali muhimu.

ILI KUSIKILIZA VIPINDI HIVI VYENYE MAUDHUI YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA TEMBELEA

http://myradiostream.com/focusradiotz

www.katibainayopendekezwa.or.tz

www.facebook.com/KatibaInayopendekezwaTanzania
0 Toa maoni yako.

Lowassa: Natazamwa na CCM kila kona

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara. Picha na Maktaba
Na Julius Mathias, Mwananchi

Dar es Salaam. Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema anashindwa kujitokeza kuzungumzia au kufanya mambo yanayohusiana na urais kwa kuwa Kamati ya Maadili ya CCM inamfuatilia kwa karibu.


Alisema hayo jana alipoulizwa kuhusu kauli ya Rais Jakaya Kikwete wiki iliyopita akiwa Marekani ambako alielezea mafanikio na changamoto alizokumbana nazo wakati wa uongozi wake wa miaka 10.

Kikwete alisema: “Wakati unaingia Ikulu unakuwa na shauku kubwa pamoja na furaha ya ushindi, lakini hakika urais ni kadhia kubwa. Ukipata fursa ya kuwa rais kwa awamu mbili kama mimi nadhani zinatosha kabisa. Nimefanya mengi kwa nchi yangu atakayekuja ataendeleza nilipoishia.”

Kauli ya Lowassa inakuja ikiwa ni siku chache baada ya makada wengine wanaotajwa kuwania urais kupitia CCM kueleza maoni yao juu ya kauli hiyo ya Rais.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ameshalieleza gazeti hili kuwa kauli hiyo inampa hamasa kwa nia yake ya kutaka kuwania urais na kwamba alitangaza nia hiyo huku akifahamu kwa asilimia 100 uzito wa jambo hilo akisema kufahamu changamoto hizo ndiyo moja ya vitu vilivyomsukuma kuchukua uamuzi huo.


Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema: “Kama mtu ameamua kuwania nafasi hiyo ina maana anafahamu anachokitaka. Tunajua ziko changamoto na namna ya kukabiliana nazo, kwa hiyo hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.”


Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla alisema: “Kauli kama hiyo haiwezi kumvunja mtu moyo, ari itabaki palepale tu kwa aliyetangaza nia. Aliyetangaza nia anataka kutoa utumishi wake kwa nchi yake kama mimi.”

Lowassa hajatangaza wazi nia hiyo zaidi ya kusema ameshawishika kuwania urais baada ya hivi karibuni, makundi mbalimbali kufika nyumbani kwake mjini Dodoma kumshawishi achukue fomu kuwania nafasi hiyo.

Miongoni mwa makundi yaliyojitokeza na kumshawishi pamoja na kumchangia fedha za kuchukua fomu ya kugombea urais ndani ya CCM ni pamoja na masheikh kutoka wilayani Bagamoyo, wachungaji wa makanisa ya Kipentekoste, wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na madereva bodaboda.

Msimamo wake hadi jana
Akizungumza jana wakati wa kuaga mwili wa Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Mohamed Mhita nyumbani kwa marehemu Oysterbay jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema: “Muda mwafaka ukifika nitatangaza nia na kuweka mikakati yangu wazi ili wananchi waijue. Kwa sasa siwezi kusema chochote kwa sababu ninatazamwa sana na chama. Ninachoweza kusema, siku nitakayotangaza nia, nitaeleza ni nini nitafanya kukabiliana na changamoto zote zilizopo Ikulu.
“Ninafahamu kuna changamoto nyingi, lakini siwezi kusema, subirini siku nitakapotangaza nia, nitaelezea ni kwa namna gani nitakabiliana na changamoto zilizopo katika ofisi hiyo nyeti nchini.”

Waziri mkuu huyo wa zamani, mmoja kati ya makada wa CCM ambao wameonyesha nia ya kutaka kumrithi Rais Kikwete katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba na pia ni miongoni mwa makada sita wa chama hicho waliokuwa wamefungiwa kwa miezi 12 na kamati kuu kwa kufanya shughuli zinazoashiria kufanya kampeni mapema.

Wana-CCM wengine waliotangaza nia na wanaotajwa katika kinyang’anyiro hicho ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
CHANZO MWANANCHI
0 Toa maoni yako.

Bakora sita za Ukawa kwa CCM

Wafusia wa Chama cha Mapinduzi wakiwa katika moja ya mikutano ya hadhara ya chama hicho jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba
Na Kelvin Matandiko, Mwananchi
                                KWA UFUPI

Vikwazo hivyo ni kuwapo kwa makundi ndani ya CCM yanayotokana na mitandao ya urais, hasira za wananchi juu ya mchakato wa Katiba Mpya, tuhuma za ufisadi ama kwa makada au Serikali yake, suala la Mahakama ya Kadhi, ahadi za Rais 2010 ambazo hazijatekelezeka na kuimarika kwa upinzani na muungano wake wa Ukawa.
Dar es Salaam. Uhakika wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutamba katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utategemea umahiri wake katika kukabiliana na vikwazo sita vinaonekana kuwa mwiba kwake ambavyo upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unatarajiwa kuvitumia kama mtaji wake katika kampeni.

Vikwazo hivyo ni kuwapo kwa makundi ndani ya CCM yanayotokana na mitandao ya urais, hasira za wananchi juu ya mchakato wa Katiba Mpya, tuhuma za ufisadi ama kwa makada au Serikali yake, suala la Mahakama ya Kadhi, ahadi za Rais 2010 ambazo hazijatekelezeka na kuimarika kwa upinzani na muungano wake wa Ukawa.

Hata hivyo, baadhi ya makada wa chama hicho bado wanaona kuwa pamoja na vikwazo hivyo, chama hicho kitapenya katika uchaguzi huo na kuongoza tena Dola kwa kuwa kinao mtaji mkubwa wa wanachama na mtandao wake ni mpana kuliko chama chochote nchini.

Mgawanyiko na makundi
Kwa nyakati tofauti, viongozi wa CCM kupitia vikao vya ndani na mikutano ya hadhara, wamekuwa wakizungumzia jinsi ya kudhibiti mivutano ya makundi ya urais miongoni mwa wanachama wake, tatizo kubwa likiwa ni jinsi gani ya kuwaleta pamoja na kuponya makovu baada ya uteuzi.

Mathalani, tangu uchaguzi mkuu uliopita, viongozi wa CCM wamekuwa wakieleza mgawanyiko baada ya uteuzi kama sababu ya kuyakosa baadhi ya majimbo muhimu nchini na tatizo hilo linaweza kukikumba hata ngazi ya urais, kisipokuwa makini.

Makundi ya watia nia ya urais kwa sasa yamesambaa mikoani kimyakimya kutafuta uungwaji mkono na baadhi yake yamejijengea ushindani wa kihasama kati ya kundi moja na jingine hadi kutupiana maneno makali na tuhuma mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo linaweza kuhatarisha uimara wa chama na kukiathiri katika uchaguzi wa Oktoba.

Mchakato wa Katiba
Tangu ulipoanza mchakato huo hadi sintofahamu inayoendelea ya Kura ya Maoni, yametokea mambo mengi na kuzua hasira kwa baadhi ya Watanzania, hivyo kuwa miongoni mwa mambo yanayohofiwa kutumika kama bakora ya kuiadhibu CCM katika Uchaguzi Mkuu.

Hasira hiyo inatokana na jinsi wananchi walivyoipokea na kuiamini Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na kuyakubali matokeo ya kazi yake lakini baadaye yakapinduliwa na Bunge la Katiba, kwa wingi wa kura za wajumbe wa CCM, ambazo hadi leo bado zinatia shaka.

Hata kitendo cha kushindikana kwa karata ya Serikali kuitisha Kura ya Maoni Aprili 30, ni kikwazo kingine kwa chama hicho, kwa kuwa hakuna namna nyingine ya kuonyesha kuungwa mkono na umma, ikiwa ni siku chache baada ya nguvu yake kuonekana kupungua katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.


UfisadiHaitoshi, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Serikali imekuwa kwenye kipindi kigumu cha matukio ya ufisadi yaliyosababishwa na ama watendaji au makada wake. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na sakata la Richmond ambavyo kwa vyovyote mwaka huu, litaibuka kwa kuwa linahusishwa na baadhi ya wagombea, sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo bado ni bichi, Epa ambayo baadhi ya watuhumiwa walisamehewa baada ya kurejesha fedha ambazo hazikuelezwa bayana zilikopelekwa na matukio yasiyokoma yanayoibuliwa katika ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


Nguvu ya upinzani
Matokeo ya upinzani katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 nayo yanaonekana kujenga hofu kwa CCM kwa kuwa yameibua picha mpya kuwa vyama vya upinzani vinakubalika hadi vijijini ambako chama hicho kimekuwa kinazoa kura bila upinzani.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, ushindi wa CCM umepungua kutoka zaidi ya asilimia 91 za uchaguzi wa 2009 hadi asilimia 70 katika mitaa na vijiji mwaka jana, jambo ambalo lisipoangaliwa linaweza kukiathiri chama hicho.


Ahadi zisizokamilika
Mambo mengine mwiba kwa CCM kama chama tawala ni baadhi ya ahadi za 2010 ambazo hazijakamilika, zikiwamo za ilani ya uchaguzi na nyingine alizotoa Rais Jakaya Kikwete binafsi kadri alivyokuwa anaona mahitaji ya wananchi katika kampeni zake.

Baadhi ya ahadi hizo ni meli katika baadhi ya maziwa, barabara, vivuko, madaraja, hospitali na huduma nyingine mbalimbali.
Mahakama ya Kadhi

Pengine suala ambalo limeacha kovu kubwa katika uso wa CCM ni suala la Mahakama ya Kadhi. Suala hili liliingizwa katika ilani yake ya 2005 kuwa ikishinda itatafuta suluhisho ambalo hadi leo limeshindikana, badala yake likaweka ufa mkubwa katika utengamano wa Taifa.

Katika siku za karibuni, Waislamu walishuhudiwa wakidai ahadi hiyo iingizwe kwenye Katiba Mpya, lakini Serikali ikaomba isiwemo, ikisema itatungiwa sheria ambayo hata hivyo inapingwa na viongozi wa Kikristo wanaodai Serikali haina dini hivyo isijihusishe nayo. Muswada huo tayari umewasilishwa na kuondolewa bungeni mara mbili.

Maoni ya wachambuzi
Akizungumza vikwazo hivyo, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, aliungana na gazeti hili, akisema kashfa serikalini kwa vyovyote utakuwa ni mtaji mkubwa kwa Ukawa katika Uchaguzi Mkuu ujao.Alisema suala la Katiba ni kesi inayojitegemea kwa Watanzania wengi wasiokubaliana na uamuzi wa Serikali kulazimisha muundo wa Serikali mbili ikiwa ni tofauti na maoni yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba.

“Kuna athari za escrow ambazo zimeanza kuonekana tangu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hakuna aliyetegemea matokeo yale kwa upinzani, kwa hivyo hali siyo nzuri mpaka baadhi ya maeneo ya vijijini,” alisema na kuongeza:

“Hali ni mbaya katika tathmini inayoonekana kwa sasa na kama asingekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana chama hicho kisingekuwa na dalili za kurudi Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, Kinana ameiombea CCM msamaha na kwa kiwango fulani ameibeba.”

Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Mallya alisema vikwazo hivyo, haviwezi kuwa kipimo pekee cha kuikwamisha CCM kutokana na uzoefu uliopo.

“Kuna makundi matatu ninayoyajua, kuna Watanzania ambao huwezi kuwabadili kitu kwa CCM, wataichagua tu bila kujali changamoto hizo. Pili, kuna kundi la vijana ambao hufanya uamuzi dakika za mwisho, hawajulikani, kuna kundi la vijana la mabadiliko na kundi la kina mama wanaoangalia upepo wa utulivu, hawa hupiga kura kwenye utulivu wa chama,” alisema Dk Mallya.

Alisema Serikali bado inayo nafasi kubwa ya kutafuta maridhiano na taasisi, mashirika na makundi mbalimbali kwenye jamii ili kuondoa athari zinazoweza kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu.

Dk Mallya alisema masuala ya Mahakama ya Kadhi na Mchakato wa Katiba yanaweza kuwa na athari kubwa kwa CCM kwa wananchi kupigia kura vyama vya upinzani.

“Serikali inaweza kurejesha imani ya Watanzania hata kwa muda uliobakia endapo itakubali kujadiliana, kukubaliana na taasisi, mashirika, viongozi wa dini na wadau,” alisema Dk Mallya.

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama alisema suala la Katiba limewakatisha tamaa Watanzania wengi waliokuwa wameweka maoni yao na kuondolewa.

Profesa Penina alisema mchakato wa Katiba ulikuwa na matarajio mazuri kwa Watanzania lakini jinsi ulivyochakachuliwa, umewafanya wengi kugawanyika.

“Sasa siwezi kujua kama hatua hiyo inaweza kuwa ni hasira ya kuiadhibu CCM, hilo sijui, ila kwa kweli imewakatisha tamaa sana, labda tusubiri tuone,” alisema Profesa Mlama.

Kauli ya CCMKupitia ziara zake za ujenzi wa chama, Kinana amekuwa akisema asilimia 90 ya ahadi za 2010 zimeshatekelezwa.

Siku chache zilizopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alilieleza gazeti hili kwamba, hata kama Ukawa wangeunganisha vyama vyote vya upinzani, bado CCM itakuwa na mtaji mkubwa wa kushinda Uchaguzi Mkuu.

Kauli ya Nape inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba aliyesema CCM haiteteleki kutokana na muungano wa Ukawa kwa kuwa ina mtaji wa wapigakura wengi.

“CCM tunajivunia kwa sababu Watanzania bado wana matumaini nasi, lakini hata kwa umoja wetu kama chama, tumefika vijijini tofauti na chama chochote, hao wapinzani wanakomea mjini tu,” alisema Simba.

Hata hivyo, mwenyekiti mstaafu wa UWT, Anna Abdallah alitoa maoni yake kwa tahadhari akisema kigezo pekee na muhimu kuliko vyote kitakachoifanya CCM kurejea madarakani ni uteuzi wa mgombea anayekubalika kwa wananchi, kwa kuwa huo ndiyo mtaji mkubwa kuliko vyote.

Alisema CCM imewahi kufanya makosa katika uteuzi wa majimbo kadhaa na kuchukuliwa upinzani.
“Kuchagua anayekubalika ni kigezo kikubwa kuliko vyote, kuhusu habari nyingine ya tuhuma au vigezo sita, sioni kama zina mashiko sana. Waswahili wanasema, “ukimpenda Mmakonde basi penda na ndonya yake”, alisema akimaanisha ukikipenda chama, penda na makandokando yake.
CHANZO MWANANCHI
0 Toa maoni yako.

Wabunge 50 kutua ACT

Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza na wahariri wa gazeti la Mwananchi alipotembelea makao makuu ya Mwananchi Communications Limited, yaliyopo Tabata Relini, Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
KWA UFUPI

Zitto ambaye alijivua ubunge wa Kigoma Kaskazini baada ya kufukuzwa uanachama wa Chadema, amebainisha kuwa wabunge hao, wakiwamo wa CCM na Chadema, ni miongoni mwa watu wanaokichangia fedha chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei, mwaka jana na kuzinduliwa mwezi uliopita.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe amesema zaidi ya wabunge 50 wa vyama mbalimbali vya siasa nchini watajiunga na chama hicho kipya na kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Zitto ambaye alijivua ubunge wa Kigoma Kaskazini baada ya kufukuzwa uanachama wa Chadema, amebainisha kuwa wabunge hao, wakiwamo wa CCM na Chadema, ni miongoni mwa watu wanaokichangia fedha chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei, mwaka jana na kuzinduliwa mwezi uliopita.

Pia, amewatangazia vita wabunge wa majimbo manane ya Mkoa wa Kigoma, akijigamba kuwa ili waweze kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo ni lazima wakubali kujiunga na ACT kwa kuwa chama hicho kimejipanga kuyabeba majimbo yote.

Akizungumza na waandishi wa Mwananchi katika ofisi za gazeti hili, Dar es Salaam jana, Zitto alisema ACT ni chama kilichojipanga na ndiyo maana haikuwa ajabu katika mkutano wake mkuu wa hivi karibuni kuhudhuriwa na wanachama zaidi ya 400 na kufanya uzinduzi wa aina yake, huku akisisitiza kuwa chama hicho kinaungwa mkono na watu wengi.

“Tuna wagombea ubunge wengi wakiwamo wabunge wa sasa ambao katika Uchaguzi Mkuu Oktoba hawatagombea kupitia vyama vyao vya sasa. Wapo ambao hawatakwenda hata katika kura za maoni za vyama vyao na wameshafanya uamuzi,” alisema.

Huku akizungumza kwa kujiamini, Zitto alisema wabunge hao ndiyo sababu ya chama hicho kuwa na uwezo wa kujiendesha na kufafanua kuwa ACT kinawakaribisha wabunge na makada wote kutoka vyama vya Chadema na CCM.


“Wale ambao wanabanwa CCM na kukosa uhuru wa kuhoji jambo lolote hiki (ACT) ndicho chama chao. Wale ambao wanaamini kuwa aina za siasa tulizotaka kuzifanya ndani ya Chadema tukashindwa kuzifanya na wanadhani ni siasa muhimu zinazotakiwa, wapo na sisi,” alisema.

Kuhusu Kigoma
“Nahitaji majimbo yote ya Kigoma kuchukuliwa na ACT bila kukosa hata moja na hili hata Serukamba (Mbunge wa Kigoma Mjini-CCM) analijua. Mwanasiasa anayetaka kuwa mbunge Kigoma lazima aje ACT,” alisema Zitto ambaye pia alirejea kauli yake kuwa atagombea ubunge katika jimbo jingine lakini siyo Kigoma Kaskazini.

Kauli hiyo ya Zitto inawagusa wabunge wa sasa wa majimbo ya Kigoma ambao ni; Felix Mkosamali (Muhambwe), Moses Machali (Kasulu Mjini), Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) na David Kafulila (Kigoma Kusini), wote wa NCCR-Mageuzi na Peter Serukamba (Kigoma Mjini, Christopher Chiza (Buyungu) na Albert Obama (Manyovu) wa CCM.

Alipoulizwa iwapo wabunge hao wa majimbo ya mkoa huo ni miongoni mwa watu watakaohamia chama hicho alisema, “Sasa huo ni mtizamo wenu. Ukiwa mwanasiasa lazima uwe na msingi, nataka msingi uwe Kigoma.

Tutakutana tena kwenye chumba hiki (cha mikutano) baadaye mwezi Novemba ili mnisute kwa kauli yangu na hapo itakuwa baada ya matokeo kutoka. Nahitaji kushinda kila kitu.Nafasi ya CCM

Akizungumzia nafasi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu alisema: “CCM inaweza kuondoka madarakani katika uchaguzi huu. Unajua chama hiki ilikuwa kiondoke madarakani mwaka 1995 wakati wa (Augustine) Mrema lakini kulikuwa na (Julius) Nyerere ambaye alikuwa na uwezo wa kuzunguka na kusema watu waendelee kuichagua CCM.

“Lakini mwaka 2015 Nyerere hayupo na hakuna mwenye kaliba yake ambaye anaweza kuzunguka na kusema msichague upinzani, chagueni CCM.

“Katika chaguzi za Serikali za mitaa zilizopita, CCM ilikuwa ikishinda kwa asilimia 91 hadi 96, lakini katika uchaguzi wa mwaka 2014 asilimia zimeshuka hadi 75.

Alifafanua kuwa kipindi ambacho CCM ilikuwa ikipata kura nyingi katika uchaguzi wa mitaa katika ubunge ilikuwa ikipata asilimia 60.


Akitolea mfano asilimia ya kura za urais za CCM tangu mwaka 1995 alisema, “Mwaka 1995, CCM ilipata asimilia 61, mwaka 2000 (asilimia 71), mwaka 2005 (asilimia 80) na mwaka 2010 (asilimia 60).

“Kipindi ambacho CCM ilikuwa inapata kati ya asilimia 90 hadi 96 ya uchaguzi wa mitaa katika ubunge ilikuwa inapata asilimia 60. Sasa hivi imepata asilimia 75 Serikali za mitaa unategemea nini katika Uchaguzi Mkuu? Hiki ni kiashiria kwamba hali ni mbaya kwa CCM.”

Alisema changamoto iliyopo ni uwezekano wa kupata rais ambaye chama chake kitapata wabunge wachache na hivyo kushindwa kupata waziri mkuu kwa mujibu wa Katiba.

“Kuna uwezekano wa kuwa na rais kutoka upinzani na waziri mkuu kutoka CCM.”

Alisema vyama vya upinzani vinaweza kutoa rais lakini haviwezi kupata viti vingi vya ubunge kwa sababu vyama hivyo vinapata ushindi zaidi katika majimbo ya mijini na miji midogo ambako watu wanataka mabadiliko na siyo katika majimbo ya vijijini ambako watu wanachagua mtu kwa uwezo wake wa fedha na umaarufu wake.

“Jambo hilo likitokea itakuwa ni changamoto ya kikatiba kwa sababu chama chenye wabunge wengi ndicho kinakuwa na waziri mkuu, lakini Katiba inasema waziri mkuu anateuliwa na rais.

Rais anatakiwa kumteua waziri mkuu kutoka chama chenye wabunge wengi na Bunge linaweza kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais.Ikitokea hivyo, rais anachoweza kukifanya ni kuvunja Bunge ili kurudi katika uchaguzi,” alisema.

Alisema ili kuepuka jambo hilo, lazima upinzani umtangaze mtu atakayekuwa waziri mkuu iwapo utashinda jambo ambalo alisema siyo maarufu katika siasa za Afrika.
0 Toa maoni yako.

Bei za vyakula zapaa, mfumuko wa bei mwezi Machi wafikia asilimia 4.2

Bidhaa za vyakula katika moja ya masoko nchini.
Picha ya mtandao. 

Na Suzan Mwillo, Mwananchi
KWA UFUPI
Upandaji wa bei za bidhaa hizo zimesababisha mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi iliyopita kuongezeka hadi ukufikia asilimia 4.3 kutoka asilimia 4.2 ya mwezi Februari mwaka huu.

Dar es Salaam. Upungufu wa chakula kwa baadhi ya mikoa nchini umeendelea kusababisha ongezeko la mfumuko wa bei wa Taifa kutoka asilimia 4.2 hadi asilimia 4.2 ndani ya mwezi mmoja.

Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ephraimu Kwesigabo, aliwaambia waandishi wa habari leo kuwa, kutokana na upungufu huo bei za bidhaa za vyakula zimeongezeka.

“Mfumuko wa bei wa Taifa kwa kipimo cha mwaka unapimwa kwa kiwango cha badiliko la kasi ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi,”alisema.

Aliongeza: “Hivyo kutokana na ongezeko la bei za bidhaa hizo pamoja na huduma zote kwa kaya zimesababisha mfumuko wa bei wa taifa,”alisema Kwesigabo.

Aliendelea kueleza kuwa, kasi ya upandaji wa bei za bidhaa hizo zimesababisha mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi iliyopita kuongezeka hadi ukufikia asilimia 4.3 kutoka asilimia 4.2 ya mwezi Februari mwaka huu.

Kwesigabo alisema, ongezeko la mfumuko wa bei kwa mwezi Machi umesababishwa hasa na kuongezeka bei za bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia Machi mwaka huu tofauti na ilivyokuwa kwa Machi mwaka jana.

Alizitaja bidhaa hizo kuwa ni pamoja na mchele, unga wa muhogo, nyama, samaki, maharage, choroko na sukari.

Alisema kutokana na hali hiyo wananchi wataendelea kushuhudia bei za vyakula zikiendelea kupanda na kwamba bei waliyokuwa wakinunua bidhaa za vyakula hapo awali itabadilika.

Akizungumzia thamani ya shilingi ya Tanzania kwa mwezi uliopita ikilinganishwa na mwezi Septemba, 2010 alisema, uwezo wa Sh 100 katika kununua bidhaa na huduma umefikia Sh 64 na senti 15 mwezi Machi mwaka huu kutoka Septemba, 2010.

“…ikilinganishwa na Sh 64 na senti 59 ilivyokuwa Febriari mwaka huu,”alisema Kwesigabo.

0 Toa maoni yako.

KWANINI CHE GUEVARA ALICHAGUA CODE NAME ' TATU' ?

Ndugu zangu,
Nimepata kuandika juu ya kitabu nilichosoma kiitwacho " The African Dream"- The diaries of the revolutionary war in the Congo. Ama hakika ni kitabu chenye maelezo yenye kusisimua, kufurahisha na kusikitisha juu ya mwanamapinduzi Che Guevara na harakati zake za mapambano ya ukombozi wa kimataifa.
Ni kweli kuwa Che aliingia Dar April 1965 na alikutana na Nyerere ili kupata baraka zake kabla ya kwenda Congo Mashariki.
Hata hivyo, katika kitabu hicho Che hakuweka wazi jina la hotel aliyoishi alipokuwa Dar. Lakini, kwa Dar ilivyokuwa hata miaka ya 70 , basi,kulikuwa na restaurants nne pale katikati ya jiji ambazo nami nimeziona kwa macho na nimepata kuingia mara kadhaa utotoni, nazo ni Zahir Restaurant ( Sasa New Zahir Restaurant iliyo Mtaa wa Msikiti).
Ni Restaurant hii ambayo Che alikwenda mahali hapo kwa chakula na chai. Kulikuwa pia na Royal Restaurant na Nakhuda Restaurant zote zikiwa Mtaa wa Jamhuri. Restaurant ya nne iliitwa The Khalid pale mtaa wa Kipande.
Hitimisho. Kama Che Guevara alikunywa chai na kula chakula Zahir Restaurant,basi,yawezekana kabisa kuwa ama aliishi Zahir Guest House iliyokuwa nyuma ya mgahawa huo, au kwenye Ubalozi wa Cuba pale Upanga. Taarifa za kuaminika zaidi ni kuwa Che aliishi Ubalozi wa Cuba.
Ni kwanini hilo halikuwekwa wazi katika kitabu cha kumbukumbu zake siwezi kujua,maana, siamini kama aliishi kwenye moja ya hoteli za gharama jijini Dar kwa vile hakutaka hata kwenda New Africa Hotel ambapo ndio ilikuwa kijiwe cha akina Abeid Karume na wapigania ukombozi wengine. Ni kwa vile, Che Guevara hakutaka kabisa kuonekana na mawakala wa CIA.
Na kwanini Che alichagua Code Name ' Tatu'? Sababu hasa haifahamiki, isipokuwa, jambo hilo liliwashangaza sana wapiganaji wa KiCongo kwenye Uwanja wa Mapambano, maana, walishangaa sana kuwa, katika mawasiliano, mwenye kuitwa TATU ndiye aliyekuwa na sauti zaidi kuliko MBILI na MOJA. MBILI ilikuwa ni Code name ya mtu wa pili na wa karibu na Che, wakati MOJA alikuwa ni mkalimani!
Maggid Mjengwa,
Iringa,
0 Toa maoni yako.

MAGAZETI LEO ALHAMISI Thursday, 09 April 2015




























































0 Toa maoni yako.
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company