Silaha za sumu zaanza kuangamizwa nchini Syria

Wataalam wa kimataifa wameanza leo mchakato wa kuziteketeza silaza za sumu za Syria kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa ambalo linaihitaji Syria kuzisalimisha silaha zake za sumu. Duru kutoka ujumbe huo wa kimataifa inasema wataalamu watathibitisha maelezo ya silaha zilizosalimishwa na serikali ya Syria na kuanza mchakato wa kuziangamiza pamoja na vituo vya kuzitengenezea. Jopo hilo lina jukumu kubwa la kutokomeza takribani tani 1,000 za gesi ya sumu aina ya sarin, pamoja na silaha nyingine zilizopigwa marufuku, katika maeneo kadhaa nchini Syria ifikapo katikati wa mwaka ujao kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa. Operesheni hiyo imeanza wakati Rais Bashar al-Assad akikiri katika mahojiano yaliyochapishwa na jarida la habari la Ujerumani - Spiegel, kuwa serikali yake ilifanya "makosa" katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini mwake. Lakini amekanusha tena kuwa majeshi yake yalitumia silaha za sumu katika shambulizi la Agosti 21 ambalo lilichochea kutayarishwa azimio la kumtaka azisalimishe silaha zake za sumu. Kundi hilo la watalaamu kutoka Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Kupambana na Matumizi ya Silaha za Sumu - OPCW, liliwasili mjini Damascus mapema wiki hii.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company