Pages

Sunday, October 6, 2013

TANZANIA YETU NA BIASHARA ZA KISHIRIKINA. Monday, 07 October 2013


Na: Albert Sanga, Iringa.

Wiki iliyopita niliandika makala iliyokuwa na kichwa, "Je kufanya biashara ni kipaji?". Ninafurahi kuwa imekuwa makala iliyowavutia wengi ambao hawakusita kunitumia mirejesho ya pongezi na maoni kupitia ujumbe wa simu, barua pepe na simu za miito. Msomaji mmoja amenitumia ujumbe ulionifurahisha kweli kweli; ninanukuu, "Makala yako ni nzuri na umechambua kitaalamu, lakini pia utajiri wa Waking asilimia 70 huwezi kuutenganisha na ushirikina. Vile vile Wachaga nao utajiri wao asilimia 30% ni ushirikina na 20% ni ujambazi. Na asilimia zilizobaki ndizo zinazoangukia kwenye uchambuzi wako". Mwisho wa kunukuu. Leo nitachambua kwa mara nyingine tena hili sekeseke la ushirikina kuhusishwa na biashara, sio tu kwa Wakinga na Wachaga pekee, isipokuwa kwa wafanyabiashara wote bila kujali kabila wala eneo waliko. Lakini kabla ya kuendelea na uchambuzi huu
kiharaka haraka nina taarifa moja ya muhimu kwa wasomaji wetu.

Kwa muda sasa wasomaji wengi wamekuwa wakiniulizia ikiwa nimeshaandika kitabu. Na kila ninapowajulisha kuwa sijaandika kitabu chochote mpaka sasa, wengi wamekuwa wakiniomba kufanya hivyo. Ombi hilo nimekuwa nikilipokea tangu zamani sana, na hatimaye mwaka huu nimeamua kulitekeleza.

Tangu Februari ya mwaka huu nimekuwa katika mradi wa kuandika kitabu kiitwacho NI WAKATI WAKO WA KUNG'AA. Ni kitabu kinachoeleza namna ya kuwa mshindi katika maeneo yote ya maisha. Kinaeleza namna ya kujitambua, jinsi ya kuwa mshindi kiuchumi, jinsi ya kung'aa kifamilia na kuwa mtu unaeona ladha halisi ya maisha.

Ninaamini kuwa kitabu hiki kitakuwa na matokeo makubwa mno kwa kila atakaebahatika kununua nakala yake. Kitabu hiki kimefikia hatua nzuri na ninatazamia kuwa kitaingia sokoni mwishoni mwa mwezi Novemba ama mwanzoni mwa mwezi Desemba. Ni kitabu ambacho asilimia tisini (90%) ya mauzo yote nitazipeleka katika kusaidia huduma za afya za watoto barani Afrika.

Msomaji aliyenitumia ujumbe wa takwimu za ushirikina na ujambazi wa Wakinga na Wachaga hakuweza kunieleza, ni wapi ametoa takwimu hizo. Wenye hekima wanatueleza kuwa pasipo kufanya utafiti hauna haki ya kuzungumza. Suala la ushirikina lipo "kiroho" na "kihisia" sana kiasi kwamba watu wengi mtaani wanaongea na kuwataja wafanyabiashara washirikina pasipo kuwa na utafiti wa kitaalamu kuhusiana na hilo.

Kwa miaka mingi nchini Tanzania (na duniani) kumekuwepo na imani, hisia, visa na matukio yanayohusisha ushirikina na mafanikio ya mtu kibiashara. Katika uzoefu wangu wa kusoma na kusikiliza sijakutana na utafiti ama maandishi yeyote rasmi yanayodhihirisha kiusawa (fair verification) nafasi ya ushirikina katika mafanikio ya mtu kibiashara.

Wataalamu wa masuala ya biashara, taasisi za maendeleo, wanadini na watu wa kada ya kawaida mara zote wasimamapo katika hadhara husisitiza watu kutoamini mchango wa ushirikina katika mafanikio ya mtu katika biashara. Pamoja na hayo; Je, ni kweli kuwa ushirikina haupo? Je, mioyo ya watu inaamini nini kuhusu hili?

Ukweli ni kwamba watu wengi wanaamini uwepo wa imani hizi za kishirikina katika biashara mbalimbali. Ni wachache wanaokiri peupe ikiwa wanatumia ushirikina lakini siku kwa siku idadi ya wanaofika kwa waganga wa kienyeji kutaka ndumba za kuwatajirisha inaongezeka.

Huku Nyanda za Juu kusini kabila la Wakinga (kama nilivyoeleza katika makala ya wiki lililopita); ni maarufu sana kibiashara. Ni kawaida sana kusikia habari za wafanyabiashara hawa kuhusishwa na ushirikini. Ukweli na uhalisia wa Wakinga (na watu wengine popote) kutumia ushirikina ni jambo ambalo huwezi kulithibitisha wala kulikanusha kirahisi.

Nakiri kuwa licha ya kwamba ni vigumu kukanusha ama kuthibitisha uwepo wa ushirikina katika biashara; vipo visa, tetesi na stori nyingi sana kuhusu ushirikina kwenye biashara. Mathalani, hivi karibuni kumevuma habari za uwepo wa waganga wa jadi nchi za jirani(Zambia, Malawi na DRC) ambao wanatoa "utajiri" kwa staili ya aina yake.

Inasemekana kuwa, huko kuna kuku wa uganga ambapo "mteja" huchota punje za mahindi na kuzirusha chini; kisha kuku wa uganga huanza kuyadonoa. Idadi ya punje atakazodonoa ndio miaka utakuwa hai ukiwa na utajiri wa kupindukia.

Mbali na habari hii ya utajiri wa kudonoa (kama unavyojulikana kwa jina maarufu) vile vile tumekuwa tukisikia taarifa za watu kumiliki misukule ambayo inatumika kuwafanikisha kibiashara kwa kuiba fedha kutoka kwa wengine. Maeneo mengi imani hii ya misukule, majini ama ndumba kuiba na kupeleka fedha inaitwa chuma ulete

Pengine hii ni changamoto kwa sisi wataalamu wa masuala ya biashara. Haitakuwa busara kwa wataalamu na wadau wa biashara kukaa kimya, ama kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu na mawingu mazito namna hii.

Lazima tutafiti na kujiridhisha kuhusu suala hili. Je, kwa ukweli kiasi gani kuwa ushirikina unaweza kumfanikisha mtu kibiashara? Kama ushirikina hauna nafasi katika biashara mbona kuna watu wanaoutumia na wanakiri kuwa wanafanikiwa?

Miaka kama mine huko nyuma nimewahi kufanya utafiti mdogo kuhusu nguvu ya ushirikina katika biashara. Nilikutana na kuzungumza na waganga wa jadi takribani watatu hivi. Waganga wawili kati ya hao hawakuwa tayari kuzungumzia suala hili kwa uwazi.

Lakini mganga mmoja maarufu kutoka maeneo ya milima ya Livingstone niliekutana nae mjini Makambako alikuwa tayari kunipa mawili matatu. Mganga huyu alikiri kuwa zipo dawa na utundu wa kijadi ambao humuwezesha mtu kufanikiwa kibiashara. Ingawa mganga huyu alisema kuwa wanatumia zaidi kanuni za kiakili (kisaikolojia) kuliko dawa.

Kwa mfano mtu apewapo dawa hizi za utajiri hupewa masharti mbalimbali ya kiuganga. Baadhi ya masharti haya ni kama; "kutokula nyama" ambapo ulaji wa nyama huongeza bajeti na kupunguza faida.

Mara nyingine mganga anaweza kumpiga marufuku muombaji wa dawa hizi za biashaa "Kutotembea nje ya ndoa". Anachozuia mganga hapa ni utapanyaji wa mali kwa sababu ni vigumu mfanyabiashara uwe na kimada halafu usihonge-haiwezekani. Na sote tunafahamu kuwa kuhonga kunapoteza fedha na kupunguza mtaji!

Waganga wengi pia hupiga marufuku waombaji wa dawa hizi "Kutovaa nguo nzuri wala kulala mahali pazuri". Hapa napo kuna janja! Kwa mujibu wa saikolojia ya walaji (Consumer beheviours) ni kwamba mtu awapo na hela hujikuta anatamani kununua vitu vingi hata visivyo na umuhimu. Mganga anapomwambia mtu huyu kuwa asile wala kuvaa vizuri, 'technically' anakuwa akipambana na "Consumer Behaviour" ya kupenda kutumia ovyo.

Waganga wengi wanafahamu kuwa pasipo kumdhibiti kisaikolojia mfanyabiashara huyu; anaweza kutumia ovyo hela ya mtaji na kujikuta biashara haikui. Ikiwa mtu hafanyi 'shopping' za gharama na ikiwa mtu hali vyakula vya anasa, 'automatically' ni kuwa fedha nyingi itabaki kwenye mzunguko na hivyo mtaji na biashara kwa ujumla kukua.

Kinachowasababisha watu wengi kuhangaika na kufuatilia ndumba katika biashara kunatokana na ukosefu wa elimu sahihi ya mambo ya kibiashara. Nyingi ya kanuni ambazo zinatumika na waganga wa kienyeji zikitolewa kama masharti kwa wateja wao zipo katika sayansi ya biashara pia.

Kuna wakati waganga huwaambia wateja wao kuwa ili kuwapata wateja wengi katika biashara; waweke dawa katika milango ya kuingilia na kisha wahakikishe wanaongea vizuri na kila mteja anaeingia. Suala la kumjali mteja na kumchangamkia aingiapo katika biashara ndilo ambalo linazalisha wateja wazuri na wa kudumu. Hii ni kanuni katika sayansi ya biashara na kamwe dawa iliyotundikwa haina cha maana inachokifanya pale!

Kutokana na kuendekeza imani za kishirikina biashara nyingi zilizopo katika nchi yetu zinakuwa sio za kudumu ama endelevu. Kwanza ni namna zinavyoendeshwa na pili ni kukosa maono endelevu. Wengi wa wafanyabiashara ambao wanatumia ndumba katika biashara zao hawana mfumo wa uendeshaji (Business management system).

Biashara ndio wao na wao ndio biashara. Kwa kuwa mganga alimwambia "dawa hii uweke katika droo ya mauzo na asishike mtu mwingine yeyote", basi mfanyabiashara analazimika kuwepo eneo la biashara masaa yote, ili kukwepa "kukiuka masharti"!

Wengi hawaajiri wafanyakazi na kuwaelekeza "A-Z" ya biashara zao kwa sababu ya masharti ya kipuuzi wanayopewa na waganga wa jadi. Wapo wafanyabiashara ambao hata wake zao hawajui namna biashara zao zinavyoendeshwa kwa sababu tu wameambiwa kuwa, "mke wako akishika fedha za mauzo akiwa kwenye siku zake za hedhi atakuwa amekiuka masharti na hivyo kufilisika"

Tena mara nyingi mmiliki wa biashara anapofariki biashara zake humfuata nyuma yake (hufilisika). Utawasikia watu wakisema, fulani alikuwa tajiri sana alipofariki, mke wake ama watoto wake walishindwa "kufuata masharti" ya mganga ndio maana wamefilisika. Sehemu kubwa ya ukweli sio kukiuka masharti ya mganga wa kienyeji, bali ni kushindwa kwa walioachiwa kuendesha biashara kwa sababu hawakushirikishwa katika uendeshaji wake pindi mmiliki alipokuwa mzima.

Kuamini ushirikina imekuwa ni sumu mbaya sana kwa sababu watu wanabweteka wakiamini kuwa "ndumba" ni kila kitu. Kuna visa vingi tunashuhudia vya kufilisika kwa wafanyabiashara mbalimbali ambako huambatana na maneno kuwa huenda wamekosea masharti ya waganga wao.

Kumbe uhalisia ni kuwa, huwa hawatambui kabisa biashara zina ukomo na bila kuzihuisha, kuziboresha na kubuni mpya; muda utafika nguvu ya soko itakulazimisha uondoke na kujikuta umefilisika.

Wengi hawana ushauri wa kitaalamu kuwajulisha, Je, biashara zao zinazalisha faida kiasi gani kwa mwaka? Je, hali ya masoko na ushindani ikoje na ina athari gani?. Je, biashara zake zitakuwa na hali gani miaka mitano, kumi ama ishirini ijayo? Je, mikakati na mipango gani ifanyike kuhakikisha biashara zinadumu hadi kizazi cha wajukuu zake?

Wajasiriamali wanatakiwa kufundishwa elimu ya biashara ikiwemo namna ya kutafuta masoko ya bidhaa na huduma, namna ya kuendesha biashara katika mifumo rasmi, jinsi ya kushindana katika ulimwengu wa kistaarabu pamoja na utunzaji wa kumbukumbu za kimahesabu. Kubwa kuliko yote ni namna wanavyoweza kufundishwa na kujizoeza kuwa wabunifu (creative and innovative) katika biashara zao.

Wajasiriamali tunastahili ushindi
stepwiseexpert@gmail.com 0719 127 901www.hakileo.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA