Na Bashir Yakub.
Ukisoma kichwa cha habari utaona nimeongelea nyumba lakini kimsingi mchakato huu unahusisha mali zote za wanandoa vikiwemo viwanja, magari, na kila kitu ambacho ni mali ya wanandoa. Kichwa kinajieleza kuwa ni makosa benki au taasisi yoyote ya fedha kuuza nyumba au mali yoyote ya wanandoa ikiwa wakati wa kuchukua mkopo mwanandoa mmojawapo hakushirikishwa katika mchakato wa mkopo huo.
1. MAANA YA MALI YA WANANDOA.
Mali ya wanandoa ni mali yoyote ambayo imepatikana kwa nguvu au juhudi za pamoja kati ya mme na mke walio kwenye ndoa ya kikristo, kiislam, ya serikali au ndoa nyingine yoyote halali ikiwemo ile ya kuishi wote kwa muda wa miaka miwili ( presumed marriage ).
Hizi zote ni ndoa ambazo mali ikipatikana ndani yake huwa ya wanandoa. Pia ile mali ambayo mmoja wa wanandoa amekuwa nayo kabla ya ndoa lakini baada ya ndoa ikaendelezwa na wanandoa kwa kiasi kidogo au kikubwa nayo hubadilika kuwa ya wanandoa wote.
Hii inajumuisha mali zilizopatikana kabla ya ndoa lakini wanandoa wenyewe wakaamua kwa hiari yao kuzifanya kuwa zao wote kwa pamoja kama familia kwa makubaliano maalum. Nalazimika kutoa ufafanuzi huu ili ninaposema mali ya wanandoa hairuhusiwi kuuzwa ieleweka hata kwa kiwango kidogo mali zipi ni za wanandoa na hivyo kuhitaji ridhaa ya wote katika kuwekwa dhamana.
2. MIVUTANO KATI YA TAASISI ZA MIKOPO NA WANANCHI.
Kipindi cha hivi karibuni hasa baada ya kuongezeka wito wa ujasiriamali mali na wingi wa taasisi za fedha kumekuwepo na kesi nyingi sana kati ya raia na taasisi hizi za fedha. Unapoangalia kesi hizi kwa haraka unaweza kugundua mambo mawili, kwanza umakini mdogo wa taasisi za fedha hasa katika ufuatialiaji wa uhalali wa dhamana na pili uelewa mdogo wa raia kuhusu taratibu na haki walizonazo katika mikopo.
Raia wanazilalamikia taasisi za mikopo kwa kuwa wababe , wasio na subira na wakiuka taratibu na huku taasisi za fedha nazo zinawalaumu raia kwa kuwa wakaidi ,wakorofi na wasiopenda kurejesha amana wanazopewa. Ni msuguano mtupu.
3. BENKI HAIWEZI KUUZA NYUMBA KWA MKOPO AMBAO MMOJA WA WANANDOA HAKUSHIRIKI.
Hili liko wazi kuwa benki au taasisi yoyote ya fedha ni makosa kuuza dhamana au kitu chochote kilichowekwa rehani kwa ajili ya kuchukulia mkopo ikiwa kitu hicho ni mali ya wanandoa na mwanandoa mmoja kati ya wanandoa hao hakushirikishwa katika hatua za kuchukua mkopo.
Mali ya wanandoa inaweza kuuzwa iwapo tu wote wawili walishirikishwa katika kuchukua mkopo lakini si mkopo achukue mmoja halafu eti nyumba au kiwanja cha familia kipigwe mnada kwa kushindwa kurejesha. Ikitokea mali kuuzwa kwa mazingira kama hayo basi litakuwa limetendeka kosa sawa na makosa mengine tunayoyajua.
4. NINI MWANANDOA AFANYE IKIWA HAKUSHIRIKISHWA NA MALI INAELEKEA KUPIGWA MNADA.
Ikiwa wewe ni mke na mme wako ndiye alichukua mkopo bila kukushirikisha au wewe ni mme na mke wako ndiye alichukua mkopo bila kukushirikisha basi unayo nafasi nzuri na ya kuaminika kuweza kuzuia uuzwaji wa nyumba au mali yoyote isiuzwe kwa sababu hiyo tu kuwa hukushirikishwa ukiwa kama mwanandoa.
Ni rahisi tu kwani inahitaji kukimbilia mahakamani na kuomba kusitishwa uuzaji kwasababu ukiwa kama mwanandoa haukushirikishwa wakati wa kuchukua mkopo na hivyo huutambui. Ni sababu ya msingi na ya kisheria na inakubalika vizuri mahakamani na kwasababu hiyo utapata zuio na mali haitouzwa.
5. WAJIBU WA BENKI AU TAASISI YA FEDHA.
Benki au taasisi ya fedha inawajibu kisheria kufanya uchunguzi na kujiridhisha kabla haijatoa mkopo kwa kuangalia ikiwa mali inayowekwa dhamana ni ya wanandoa au hapana. Huu ni wajibu wa benki na raia hahusiki nao. Kama wao watafanya uzembe wasichunguze hili au wachunguze lakini wasilione hili basi waliobaki hawahusiki na benki wawe tayari kupoteza iwapo mwanandoa ataibuka kupingana nao.
6. NINI UFANYE KAMA TAYARI MALI IMESHAUZWA.
Hapo juu nimesema kuwa kama wewe ni mwanandoa na hili limekukuta basi kimbilia mahakamani uzuie uuzaji. Zaidi nitoe hamasa kuwa kama tayari nyumba imeshauzwa basi hujachelewa fungua kesi ya kuomba kurejesha nyumba kwa sababu hii hii ya kutoshirikishwa na katika hili huna haja ya kutia shaka nyumba itarejeshwa vizuri tu. Badilika na chukua hatua.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE (Muro)

No comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA