LEO tuangazie kwa karibu kwenye ugaidi wa Kipalestina, maana, tumeshajadili ugaidi wa Kiyahudi. Na jana hapa tuliangalia ushiriki wa Jenerali Idd Amin katika Ugaidi wa Kimataifa. Na hoja ya Idd Amin katika kuunga mkono ugaidi ilikuwa ni kuonyesha mshikamano kwenye suala la Wapalestina.
www.hakleo.blogspot.comKatika kuungalia mgogoro wa Wapalestina na Waisrael na tuangalie kwa karibu harakati za mapambano ya Wapalestina dhidi ya dola ya Israel. Bado tuna kumbukumbu, kuwa chama cha Hamas kimepata kushinda uchaguzi wa bunge .Hivyo basi, Hamas kimepewa nafasi ya kuunda serikali.
Mara tu baada ya ushindi wa Hamas, Israel ilitamka wazi, kuwa haitashirikiana na Hamas kwa lolote lile . Ni kwa vile Hamas ni chama cha kigaidi, vivyo hivyo Marekani na Umoja wa nchi za Ulaya zilionyesha kutoiunga mkono Hamas. Chama hicho kinashutumiwa pia na taasisi za Umoja wa Mataifa zenye kuhusika na haki za kibinadamu kama vile Amnesty International na Human Right Watch.
Hamas, jina la chama hicho ni neno la Kiarabu lenye maana ya hamasa au enye kutia hamasa. Bila shaka yeyote, Hamas kama lilivyo jina ake, imefanikiwa kuwahamasisha Wapalestina wengi na hususan vijana kuwapigia kura na hivyo basi kufanikisha ushindi wao.
Hamas ilishinda uchaguzi wa wabunge kihalali kwa njia ya masanduku ya kura. Tofauti na PLO, Hamas kwa takribani miaka 20 sasa imewekeza
kwa wapiga kura waliokuwa bado watoto wadogo miaka 20 iliyopita. Hamas imejikita kwa Mpalestina wa kawaida mwenye maisha duni. Hamas wamekuwa
wakiendesha huduma za kijamii kama vile shule, afya na kujenga misikiti.
Hamas wamevuna walichopanda.
Mwasisi wa Hamas ni Sheikh Ahmed Yassin, mzee aliyekuwa akitembelea kiti cha baiskeli ya gurudumu mbili. Aliuawa na walenga shabaha
wa Israel Machi 22, 2004 alipokuwa akitoka msikitini saa za alfajiri. Mrithi wake Bw. Abdul Aziz Rantisi naye aliuawa kutokana na majeruhi aliyoyapata baada
ya shambulizi la helikopta lililofanywa na makomandoo wa Israel Aprili 17, 2004.
Kiongozi wa sasa wa Hamas anaitwa Ahmed Mashal. Kimsingi Mashal, kutokana na sababu za kiusalama, amekuwa na makazi yake Damascus, Syra. Si ajabu leo kuona Israel ya Benjamin Nethanyau inarusha ndege zake za kivita kwenda kuishambulia Syria. Israel imeamini siku zote, kuwa Syria inawahifadhi wanaharakati wa Hamas. Mwaka 1997, mawakala wa kijasusi wa Israel walijaribu bila mafanikio kumwua Ahmed Mashal kwa kumtilia sumu kwenye chakula.
Mkakati wa kuitenga Hamas huenda ukapelekea Intifada ya nne katika Palestina. Itakumbukwa, katika miaka ya themanini, mashambulizi ya
kigaidi dhidi ya dola ya Israel yaliendelea. Ingawa hivyo, ni katika kipindi hiki , ambako mashambulizi ya kigaidi yaliendelea huku hatua za majadiliano ya kufikia amani ya Palestina zikifanyika. " Ardhi kwa Amani" ni msemo uliojulikana katika kipindi hicho. Ardhi kwa Amani ina maana ya kuundwa kwa taifa la Palestina ndani ya mipaka ya Israel. Kwamba Wapalestina walikuwa
tayari kuishi na wavamizi wa ardhi yao kama majirani.
Maeneo hasa ambayo Wapalestina wanataka iwe ni sehemu ya taifa la Palestina ni maeneo yote yaliyovamiwa na kukaliwa na Israel kunako mwaka 1967, haya ni maeneo ya Gaza, Ukingo wa Magharibi na milima ya Golan. Hilo ndilo liwe taifa la Palestina. Hata hivyo, dai hilo halitoshelezi matakwa ya Wapalestina wengi.
Mwanzo wa kile kinachoitwa Intifada katika Palestina ni ajali ya gari iliyoua Wapalestina. Ajali hiyo iliyosababishwa na askari wa kivamizi wa Israel ilitokea mwaka 1987 katika eneo la Gaza.
Vijana wa Kipalestina walianza kuwarushia mawe askari wa Israel. Huo ndio ukawa mwanzo wa kinachoitwa Intifada. "Intifada " ni neno la Kiarabu lenye maana ya "mtikisiko" ama "machafuko ya upinzani". Mwanzo wa Intifada ikawa ni kukua kwa mgogoro baina ya Wapalestina na Waisrael.
Kati ya miaka hiyo ya themanini na kuendelea, tunaweza kuona awamu mpya ya vitendo vya kigaidi, yaani mauaji ya Wahanga. Shambulizi la kwanza na kubwa la Wahanga ni lile lilitokea Lebanon mwaka 1983. Lori lililosheheni silaha za milipuko lilikwenda moja kwa moja hadi Makao Makuu ya kambi ya jeshi la Wana-maji la Marekani mjini Beirut.
Takribani wanajeshi 200 wa Marekani waliuawa. Matokeo ya shambulizi lile ni uamuzi wa Marekani na majeshi yake kuondoka Lebanon.
Shambulizi lile la Kihanga lilianzisha ukurasa mpya wa mashambulizi ya kigaidi.
Leo tunashuhudia , vijana wa kike na kiume wenye kujifunga miilini mwao silaha za milipuko tayari kwenda kufanya mashambulizi yatakayopelekea vifo vyao pia. Vijana hawa huchagua maeneo yenye watu wengi.Wahanga hawa wanafanya hivi wakiwa na imani ya kidini. Imani ya kuwa tayari kufa kwa kupigania kile kilicho haki yao. Na kwamba mwenyezi Mungu amewandalia pepo ya mbinguni.
Kasi ya mauaji ya kihanga iliongezeka mwishoni mwa miaka ya tisini. Sababu kubwa ni kutokana na serikali ya Israel kutokuwa na nia thabiti ya kutaka kujadiliana na Wapalestina juu ya kupata jawabu la kudumula mgogoro husika. Waisrael walitaka chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO kianze kwanza kuwadhibiti Wahanga na Waislamu wenye imani kali kabla ya Israel kuingia kwenye meza ya majadiliano ya kweli na Wapalestina.
Hii ni sawa na "Moment 22" kwa wale waliosoma kitabu cha Joseph
Hellers. Katika hili Wapalestina na hususan PLO, nayo inataka Israel iondoke
katika maeneo iliyoyavamia kwanza, ili angalau PLO ipate nguvu na mamlaka
ya kuwadhibiti Wahanga.
Isitoshe, Arafat na PLO wangeweza vipi kudhibiti hali ya mambo katika maeneo yaliyo chini yao, wakati kila shambulizi la kihanga linapotokea, Israel hujibu kwa kushambulia taasisi za Palestina ya PLO ikiwemo vituo vya polisi? Mathalan, kwa muda mrefu sana , Arafat alipokuwa hai, alizuiwa na Israel kutoka nje ya Ramallah.
Baada ya Hamas kuingia madarakani, kuna kila dalili kuwa mgogoro wa Israel na Wapalestina umechukua sura mpya. Safari hii kuna uwezekano pia kwa Al qaida ikawatumia vijana wa Hamas katika kuendesha mapambano yao dhidi ya dola ya Israel na kutishia zaidi maslahi ya Wamarekani katika Mashariki ya Kati.
Na kwa kutambua hilo, jitihada za hivi karibuni ni kwa Barack Obama kumtumia Waziri wake wa Mambo ya Kigeni, John Kerry kwenye kufanya mazungumzo ya kupatikana kwa suluhu ya amani kati ya Israel na Palestina. Ni kuunga mkono jitihada za nchi za Kiarabu katika kutafuta suluhu hiyo.
Inahusu ardhi. Na Wapalestina chini ya Hamas hawaonekani kuridhika na mapendekezo yaliyopo mezani. Hivyo basi, kuzidi kuwepo kwa hofu ya ugaidi. Itaendelea...