HABARI KUU ZA LEO na OSCAR SAMBA
print this page
HABARI NA Oscar Samba
Showing posts with label KITAIFA. Show all posts
Showing posts with label KITAIFA. Show all posts

ni matokeo ya serikali dhaifu,kuwafukuza wanafunzi walioingia vyuoni kimakosa

NA WAANDISHI WETU, DODOMA/DAR

NI kizaazaa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya migomo na fukuzafukuza ya wanafunzi kutawala katika vyuo vikuu nchini hali ambayo inaonekana kuibua hisia miongoni mwa Watanzania.

Kufuatia kurudishwa nyumbani kwa wanafunzi 7,802 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Jumuiya ya Wanataaluma wa chuo hicho, imevunja ukimya na kubaini mikakati yenye shaka dhidi ya uongozi.

Kutokana na hali hiyo wanataaluma hao wamelaani kitendo cha kurudishwa nyumbani kwa wanafunzi hao wa programu maalumu ya ualimu wa msingi na sekondari bila kupewa muda wa kutosha kujiandaa kwa kuzingatia umri wao na mazingira waliyokuwa wanaishi.

Tamko la jumuiya hiyo lilitolewa jana na kusambazwa kwa vyombo vya habari na katibu wake, Lameck Thomas, ambaye alisema lawama zimekuwa zikitupwa kwa walimu kutokana na taarifa hizo kutolewa na upande mmoja wa utawala pekee kwenda serikalini bila uwepo wa ushirishwaji wowote wa wahadhiri kupitia jumuiya yao.

Kutokana na hali hiyo, Thomas alisema si busara wao kama jumuiya kukaa kimya kwa jambo hilo bila kueleza usahihi wake kwa kina, hasa katika madai ya fedha ambapo kumekuwa na uchezewaji wa tarakimu.

“Si kweli kuwa walimu tuligoma kufundisha programu hii kama inavyoelezwa sehemu mbalimbali,” alisema Thomas.

Alisema tatizo kubwa ni kutokuelewana kati ya walimu na menejimenti ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo chuoni hapo, ambapo malalamiko hayo waliyatoa tangu iliponzishwa.

“Na kumekuwa hakuna dalili yoyote ya ufumbuzi huku wakiendelea kufundisha kwa uzalendo mkubwa. Jumuiya ya Wanataaluma inapata hisia kuwa wizara imeamua kwa makusudi kushirikiana na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kupotosha uhalisia wa jambo hilo kwani hakuna hata wakati mmoja ambapo wamefanya mawasilianao na walimu kupata taarifa kutoka upande wao,” alisema.

Katibu huyo alisema kuwa katika kutafuta ufumbuzi kuhusu mgogoro huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya, alikutana na menejimenti ya chuo hicho Mei 19, mwaka huu chuoni hapo ambapo katika kikao hicho wajumbe walikubaliana kwa pamoja kuundwa kwa kamati ndogo ya kufuatilia suala hilo.



UTATA WA MADAI

Alisema madai yanayoelezwa na menejimenti si sahihi na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, imepotosha kwani haijaeleza ukweli wa madai yaliyowasilishwa na chuo husika.

“Mfano katika Kitivo ‘Koleji’ cha Sayansi Asilia na Hesabu taarifa inasema yaliwasilishwa madai ya shilingi milioni 367.88 na kupungua mpaka shilingi milioni 90. Wakati uhalisia ni kwamba madai hayo hata kama yangebanwa kwa namna gani yasingepungua mpaka chini ya shilingi milioni 223.78,” alisema Thomas.

Alisema kuwa Kitivo cha Kompyuta taarifa inasemwa waliwasilisha madai yanayozidi sh milioni 100 wakati taarifa za Koleji zinasema madai halisi ni Sh milioni 53.7.

“Kwa nini utaratibu wa malipo uliotumika mwaka jana haukutumika wakati ulifanyika bila ya kuleta matatizo yanayoonekana wakati huu? Kama tatizo ni uhakiki wa madai kwa nini mpaka sasa tunapoongea walimu wa Koleji za Ualimu na Sayansi Asilia na Hesabu hawajalipwa hata senti moja ambapo ni katikati ya muhula huu wakati walifundisha muhula uliopita?’’ alihoji Thomas.

Katibu huyo alipinga kile alichodai kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alitoa kauli ya upande mmoja Mei 30, mwaka huu suala ambalo haliwezi kuleta utatuzi wa kudumu kwani walimu hao wana mambo mengi ya kuzungumza ikiwamo mgogoro wa madai yao.

“Mfano mpaka sasa katika Koleji ya Sayansi Asilia na Hesabu kuna upungufu wa walimu 128 waliokuwa wanahitajika kufundidha programu hiyo kwa ufanisi, kwa muhula uliopita ni walimu 72 tu ndiyo waliobeba mzigo wa upungufu huo na kwa muhula huu hali ilikuwa inaelekea kuwa mbaya sana,” alisema.

Alisema kuwa wingi wa wanafunzi na uhaba wa walimu ulisababisha upangaji wa ratiba ya kufundisha kuwa ngumu kutokana na kozi kugawanywa katika mikondo mingi ambayo walimu walilazimika kuifundisha huku wakiwa na majukumu ya kufundisha kozi za shahada na majukumu mengine.



RAIS MAGUFULI

Akizungumza jana katika sherehe za utoaji tuzo za rais kwa wazalishaji bora viwandani kwa mwaka 2015, Rais Dk. John Magufuli alisema kuwa anashangazwa na wanasiasa wanaotetea watu waliopata daraja la nne kutaka waachwe wasome chuo kikuu.

“Ukigeuka hivi unakutana na wanafunzi hewa, ni nchi hii tu ambapo mtu unaweza kupata Divisheni 4 ya form 4 ukaingia chuoni na ukapata mkopo wa Serikali wakati wa form 6 hawapati mkopo. Ni nchi hii tu na anatoka mtu mwanasiasa mmoja anasema hawa wangesoma tu… kama tulifanya makosa ni lazima tuyamalize.

“Ninyi mnafahamu mtu ukimaliza form four (kidato cha nne) ukifeli sana sana utakwenda kuanzia certificate (cheti), ukifaulu then (halafu) unakwenda kuchukua diploma, baada ya miaka kadhaa tungejikuta ni Taifa la watu wa ajabu sana, ninasema haitawezekana, kama tuliyafanya makosa ni lazima tuyarekebishe na wakati ni sasa. Tuache siasa kwenye makosa,” alisema Rais Magufuli.



WANAFUNZI WAFUNGUKA

Baadhi ya wanafunzi waliorudishwa nyumbani katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wameelezea kushangazwa na tangazo lililotolewa la kutakiwa kurudi nyumbani huku wakiwa hawana kosa lolote.

Mmoja wa wanafunzi hao aliyejitambulisha kwa jina la Praygod Emmanuel, alisema kuwa aliyekuwa chuoni hapo mwaka wa pili akichukua Diploma ya Sayansi ya Ualimu, alisema anashangaa wao kufukuzwa mithili ya wanyama huku kosa likiwa si la kwao.

“Tunashangazwa kufukuzwa mithili ya wanyama, sasa hivi tunaishi kwa hofu na hatujui hatma yetu kwani tunaambiwa tutaona katika vyombo vya habari na kwenye mtandao wa chuo,’’ alisema.

Naye Joshua Meshack alisema kwa sasa hawajui hatima yao na kuiomba Serikali kuwaangalia kwani hawana wanachotegemea zaidi ya elimu waliyokuwa wakiipata ili ije iwasaidie katika siku za usoni.

Meshack alisema kinachowaumiza zaidi ni kutofanya kosa lolote, lakini wamejikuta kwenye adhabu na mateso makubwa ikiwamo kukosa fedha za kuwawezesha kurudi makwao.

“Sisi hatuna kosa, kosa ni la watu wengine vipi tuumie sisi? Maisha yetu ni ya shida, mimi sijarudi nyumbani nipo na sina hata nauli ya na sijui nitafikaje nyumbani,” alisema.



PROFESA NDALICHAKO

Juzi jioni akitoa taarifa ya Serikali bungeni, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Ndalichako, aliahidi kupitia upya mfumo wa utoaji wa mafunzo ya stashahada maalumu kwa walimu wa sayansi Udom ili kuondoa matatizo yaliyopo.

Alisema Serikali imeamua kupitia mfumo huo ili kuufanyia marekebisho na kuweza kuwasaidia wanafunzi wa kada hiyo.

“Serikali itashirikina na uongozi wa chuo cha Udom kupitia upya mfumo wa utoaji wa mafunzo hayo ya diploma ya sayansi, tutaangalia utaratibu mzuri zaidi ambao utakuwa na tija kwa wanafunzi, wahadhiri na Taifa kwa ujumla,” alisema Profesa Ndalichako.

Aliongeza kuwa walimu wanaofundisha stashahada ya ualimu wa masomo ya sayansi walianza mgomo Mei 9, mwaka huu kutokana na madai ya malipo ya muda wa ziada wanaotumia kuwafundisha wanafunzi hao.

Alisema baada ya malalamiko uongozi wa chuo uliamua kuhakiki madai yao na yalipohakikiwa yalionekana yapo juu kwa mujibu wa sera ya chuo na uzito wa kazi, yaani walipaswa kulipwa posho hiyo.

Profesa Ndalichako alisema kuwa kiasi cha madai kilichowasilishwa ni Sh milioni 934 wakati fedha zilizohakikiwa ni Sh milioni 252 kiasi ambacho waajiri wamekipinga.



UAMUZI WAPINGWA

Hata hivyo uamuzi huo wa Serikali kuwaondoa wanafunzi wa Udom chuoni uliotolewa bungeni na Profesa Ndalichako umepingwa kila kona na wadau mbalimbali wakiwamo walimu, wazazi wa watu wa kawaida.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimemuomba Rais Magufuli kumaliza sakata hilo la wanafunzi bila kuendelea kuwaathiri.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Helen Kijo- Bisimba, alisema Dar es Salaam jana kuwa Rais Magufuli anapaswa kuliangalia kwa jicho la karibu tatizo la wanafunzi hao kwa sababu wananyanyasika na kudhalilishwa.

“Kimsingi mgogoro ulipofikia Rais Dk. Magufuli aone umuhimu wa kusuluhisha kwani kwa taarifa zilizopo wanafunzi hawa wanadhalilika, kunyanyasika wakati waliowapeleka chuoni hapo ni Serikali yenyewe,” alisema Dk. Helen ambaye pia ameutaka uongozi wa Bunge kuwarejesha wabunge wote waliosimamishwa waendelee na vikao ili kuwawakilisha wananchi wao.

Dk. Helen alisema kuwaondoa wanafunzi hao bila kuwapa nauli, kuwaandalia mazingira salama ni hatari kwa kuwa wengi wametoka kwenye familia masikini na hawakuja kimakosa katika chuo hicho bali ilikuwa mpango wa Serikali.

Alisema mgomo wa walimu wa kudai masilahi haukupaswa kuwaadhibu vijana hao na badala yake Serikali ichukue nafasi ya kuzungumza na walimu hao ili kumaliza tatizo hilo kwa njia ya amani.

“Inasikitisha watoto hao kufukuzwa chuoni, tena kwa kupewa saa 24 kama wahalifu wa makosa ya jinai wakati waliingia chuoni hapo kwa taratibu na vigezo vya Serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

“Watoto hawa wametimuliwa kama wakimbizi au wahalifu kwa kupelekewa polisi wenye mabomu ya machozi bila kujali hali yao ya kiuchumi, kisaikolojia wala utu, huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa ndani ya nchi ambayo inajinasibu kutekeleza demokrasia, sheria na haki za binadamu.

“Kwa maana hiyo kiongozi huyo haoni haja ya maisha ya wanafunzi hao hata kama wakibakwa, kutekwa, kuuawa kwani kwake hilo si jambo la dharura na halihitaji muda wa kujadiliwa,” alisema Dk. Helen.



WABUNGE KUTIMULIWA

Aidha Dk. Helen alizungumzia kusimamisha wabunge saba wa upinzani wasihudhurie vikao vya bunge vikiwamo vya bajeti.

Alisema miezi sita tangu bunge la 11 lianze hakuna jipya ndani ya Bunge hilo mbali ya kushuhudia likiendeshwa kibabe na kisiasa.

“Katika kuonyesha ubabe wa kiti cha Spika wa Bunge hilo, tumeshuhudia wabunge saba wakipewa adhabu ya kutohudhuria vikao kwa vipindi tofauti kwa madai wamekidharau kiti katika kikao cha Januari 27, mwaka huu,” alisema.

Wabunge waliosimamishwa ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Esther Bulaya (Bunda Mjini), Pauline Gekul (Babati Mjini), Godbles Lema (Arusha Mjini), Halima Mdee (Kawe, John Heche (Tarime Vijijini) na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini).



KAGERA

Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu (CWT) Mkoa wa Kagera, Paul Kosta alisema uamuzi wa Serikali kuwarudisha nyumbani wanafunzi wa Udom kwa muda usiojulikana hauna nia njema kwa mustakabali wa elimu nchini.

Kosta ambaye pia ni mwalimu wa hisabati katika Shule ya Sekondari Rutabo iliyopo Tarafa ya Kamachumu wilayani Muleba, alisema lengo la Serikali kuweka utaratibu wa kusomea shahada kwa wanafunzi hao si wa bahati mbaya kwani ulitokana na nia yake ya kupunguza pengo la walimu wa sayansi linalolikabili taifa kwa sasa.

“Tumesikitishwa na hatua hiyo, mahitaji ya taifa kwa walimu wa sayansi bado ni makubwa kwa shule za msingi na sekondari, tunaambiwa Serikali ya sasa imevunja rekodi ya ukusanyaji kodi, kwanini inashindwa kuwalipa wahadhiri? alihoji.

Sunday Bubelwa ambaye ni mjasiriamali katika Mji mdogo wa Kamachumu alipiga simu MTANZANIA akisema hakuona sababu ya Naibu Spika kupinga hoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari bungeni juzi.

“Vijana wetu tunasikia wamegeuka ombaomba na machangudoa katika mji wa Dodoma, Sisi tunajua mawaziri na baadhi ya wabunge wa CCM wanafanya hivyo kwa sababu watoto wao hawako katika mazingira kama hayo,” alisema Bubelwa.



DAR

Athman Mwamtemi ambaye ni dereva teksi katika Mtaa wa Samora jijini humo alisema: “Dk. Tulia amepotoka, hayo ni matumizi mabaya ya kiti kwa kukiuka haki ya msingi ya Bunge hilo kujadili suala zito kama hilo la elimu kwa watoto wa Tanzania.

“Ni haki ya wabunge kutetea masuala ya wananchi, hakuna sababu ya kuwafungia, haya ni matumizi mabaya ya kiti na hapa Naibu Spika amepotoka, anapaswa kukubali hilo na anapaswa kusahihisha makosa na kuacha ubabe,” alisema Chande.



WANAFUNZI UDSM WAGOMA

Wanafunzi wa shahada ya kwanza wanaonufaika na mkopo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), sehemu ya Mlimani, wameingia kwenye mgomo kutokana na kucheleweshwa kwa fedha za kujikimu, huku wakimtaka RaisMagufuli kuwatumbua viongozi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB).

Pia wanafunzi hao wamekumbusha ahadi za Rais Magufuli wakati wa kampeni kuwa katika Serikali yake hatomvumilia kiongozi wa bodi atakayechelewesha fedha za kujikimu za wanafunzi wa elimu ya juu.

Vuguvugu la mgomo huo lilianza juzi usiku katika hosteli za wanafunzi hao zilizopo Mabibo ambapo inadaiwa walikuwa wanapiga kelele za kudai fedha hizo wakilalamika kuwa wana njaa.

Akizungumza na MTANZANIA jana katika eneo linalotumika kwa mikutano ya wanachuo maarufu kama ‘Revolution Square’, mmoja wa wanafunzi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa kuhofia kufukuzwa chuo, alisema juzi walikutana na Rais wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO) ambaye aliahidi kuitisha mkutano wa wanafunzi wote kujua hatima ya malipo yao.

“Tumekusanyika hapa kutokana na agizo la rais wetu kuwa atakuja kuzungumza juu ya madai yetu ya kucheleweshewa fedha, jana (juzi) tulianza harakati hizo katika hosteli za Mabibo na leo (jana) hatujaingia darasani na hatutaingia hadi tupate fedha zetu,” alisema mwanafunzi huyo.

MTANZANIA ilifika katika eneo hilo jana saa 4 asubuhi na kushuhudia baadhi ya wanafunzi wakiwa wamekusanyika huku wengine wakipita kuelekea madarasani kuendelea na masomo kama kawaida.

Ilipofika saa 7 mchana rais wa DARUSO, Erasmi Leoni, aliwasili katika eneo hilo ambapo aliwataka wanafunzi hao kuwa na subira wakati akiendelea kuwabana utawala kutoa majibu huku akiwataka waendelee kubaki katika eneo hilo hadi watakapopata majibu ya kuridhisha.

“Naungana na ninyi kuendelea kukaa hapa hadi tutakapopata fedha zetu na tunatoa nusu saa kwa uongozi wa chuo kutupa majibu ya kupata fedha hizo leo (jana) na kama hawatatoa majibu ya kuridhisha tutachukua hatua zaidi,” alisema.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Mikopo Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Mikopo mstaafu wa UDSM, Evance Shitindi, alisema atashangaa kuona wanafunzi wanafukuzwa kwa mgomo huo badala ya kufukuzwa viongozi wa bodi huku akikumbushia ahadi ya rais kwa kuweka katika kipaza sauti, sauti iliyorekodiwa ya Rais Magufuli iliyokuwa katika simu yake.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mkandala, aliliambia MTANZANIA kuwa chuo hakina mamlaka ya upatikanaji wa fedha hizo, lakini wanashirikiana na bodi kuhakikisha zinapatikana kwa wakati.

“Sisi kazi yetu ni kuhakiki majina ya wanafunzi wanaopokea mikopo ili kusiwepo hewa, lakini mpaka wakati huo waliwasiliana na bodi ya mikopo kwamba wamepeleka fedha hizo benki,” alisema Profesa Mkandala.

Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo, Cosmas Mwaisoga, alisema mchakato wa malipo umekwishafanyika na hundi za malipo hayo zimepelekwa benki.

“Siku ya malipo ilikuwa ni Mei 28 mwaka huu ambayo ilikuwa Jumamosi na sisi siku hiyo hatufanyi kazi ndiyo maana sasa tunapigana kuharakisha mchakato ili wapate fedha zao haraka iwezekanavyo,” alisema.



CHUO CHA MAJI

Zaidi ya wanachuo 40 wanaosoma shahada ya uhandisi wa maji na umwagiliaji katika Chuo Kikuu cha Taasisi ya Maji (WDMI) nao wameandamana kwenda Bodi ya Mikopo wakilalamikia kucheleweshewa fedha za chakula na kujikimu.

Akizungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wanachuo hao alisema wamefikia hatua hiyo baada ya bodi hiyo kushindwa kutoa fedha zilizotakiwa tangu Mei 20, mwaka huu.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Joseph Ikingu alisema taarifa waliyoipata kutoka kwa ofisa mikopo wa chuo hicho ni kwamba taratibu za kusaini hundi kwa ajili ya kutolewa fedha hizo zilikwishakamilika.

Meneja Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo nchini, Omega Ngole aliliambia MTANZANIA kuwa wanafunzi hao wanachokifanya ni upotoshaji kwani tarehe waliyopaswa kuanza kupokea mikopo yao ni Mei 26, mwaka huu hivyo hakukuwa na ucheleweshwaji.

Habari hii imeandaliwa na LEONARD MANG’OHA (MSJ), CHRISTINA GAULUHANGA NA FROLIAN MASINDE (DAR ES SALAAM), Ramadhan Hassan, Aziza Masoud (Dodo
0 Toa maoni yako.

JPM awatangazia vita wafanyabiashara ‘wajanja’

Rais John Magufuli kwenye hafla ya utaoji wa Tuzo ya Rais ya wazalishaji bora wa viwandani kwa mwaka 2015 zilizofanyika jijini Leo Dar es Salaam.
Kwa ufupi

Rais Magufuli ameyasema hayo leo kwenye hafla ya utaoji wa Tuzo ya Rais ya wazalishaji bora wa viwandani kwa mwaka 2015 zilizofanyika jijini Dar es Salaam.By Raymond Kaminyoge, Mwananchi rkaminyoge@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali yake itaendelea kupambana na wanaoingiza bidhaa zilizochini ya kiwango na wale wanaokwepa kodi.

Amesema kwa kufanya hivyo, wanachangia kuviua viwanda vya ndani ya nchi.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo kwenye hafla ya utaoji wa Tuzo ya Rais ya wazalishaji bora wa viwandani kwa mwaka 2015 zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Tuzo hizo zimeandaliwa na Shirika la Wenye Viwanda Nchini (CTI).

Rais amesema pia hatawavumilia watendaji wote watakao wakwamisha wafanyabiashara wenye nia ya kuanzisha viwanda nchini kwa sababu zisizo za msingi na kuwaahidi kuwasaidia waweze kufanikisha ndoto zao.

Pia, amesema ni vizuri wafanyabiashara wote nchini wakatumia fursa zipatikanazo katika awamu hii ya uongozi wake, ili wasije kuzijutia baadaye.

“Nasema kwa dhati kutoka moyoni, you have my support, mkishindwa katika kipindi cha awamu ya tano basi hamtaweza tena,” alisema.

Rais Magufuli alisema nchi inapokuwa na viwanda vingi vitatoa ajira kwa Watanzania, vitaongeza mapato kwa Serikali na kuingiza fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa nje ya nchi.

“Nina dhamira ya dhati ndani ya moyo wangu kuwasaidia wenye nia ya kuanzisha ya viwanda, siwachukii matajiri nawapenda matajiri,” alisema.

Rais Magufuli aliwapa moyo wafanyabiashara wenye viwanda kuanzisha vingine ili Serikali iweze kunufaika zaidi.

Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi kama maliasili na madini na akawahakikishia wawekezaji kuwa lipo soko kubwa la bidhaa watakazozitengeza lenye watu milioni 160 katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Magufuli alisema sekta ya viwanda ni muhimili mkubwa wa uchumi katika nchi huku akitolea mfano wa nchi za China, India, Korea Kusini, Malaysia, Thailand na Vietnam ambazo zimekuwa kwa kasi kwa sababu ya uwepo wa viwanda.

Alisema viwanda vinapoanzishwa nchini badala ya kuuza mali ghafi kwa bei ndogo zitatengenezwa bidhaa ambazo zitauzwa nje ya nchi na kutoa ajira kwa Watanzania.

“Badala ya kuuza ngozi tutengeneze viatu hapa hapa nchini au badala ya kuuza ng’ombe Comoro tumepeke nyama iliyosindikwa,” alisema.

Alisema nchi kama ya Sudan Kusini ina mahitaji makubwa ya unga wa mahindi.

“Lakini wanaofaidika na soko hilo ni Wakenya ambao wanakuja nchini wananunua mahindi, wanasaga na kuyapeleka huko,hivi wafanyabiashara tunashindwa hata kuanzisha viwanda vya kusaga mahindi,” alisema

Alisema Mkoa wa Arusha una ng’ombe wa maziwa lakini yananunuliwa na Wakenya ambao wanayasindika kwenye viwanda vyao na kuja kuyauza hapa nchini.

Hata hivyo, alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha benki ya maendeleo ya viwanda kwa lengo la kutoa mikopo yenye masharti nafuu na riba ndogo.

Kuhusu kuondoa kwa changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo ya viwanda nchini, Magufuli alisema Serikali imeshatenga Sh1trilioni katika mwaka wa fedha ujao kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.

Pia, Serikali imeunda kamati maalumu itakayoangalia mazingira ya ufanyaji biashara nchini ikiwamo kodi na tozo mbalimbali.

“Nchi yetu inakuwa na kodi za ajabu ajabu, mfano zao la kahawa kulikua na zaidi ya kodi 30. Haya ndiyo tunayoyaangalia,” alisema.

Kuhusu upatikanaji wa mitaji na riba kubwa zinazotozwa na benki, alisema katika kukabiliana na matatizo hayo Serikali inajiandaa kuanzisha benki ya viwanda itakayowasaidia wenye wawekezaji.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema Serikali imejikita katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda vingi zaidi nchini.

“Tumeandaa mkakati wa pamba hadi inakuwa nguo, alizeti hadi mafuta na tunaendelea kufufua viwanda vilivyokufa,” alisema.

Akizungumzia changamoto zinazowabiri wenye viwanda nchini, mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Samuel Nyantahe alisema uchakavu wa miundombinu ya umeme na miundombinu ya barabara imekuwa ikiongeza gharama za uzalishaji.

Pia, alilalamikia uwapo wa utitiri wa kodi, mamlaka za usimamiaji biashara na uwapo wa bidhaa bandia zinazotishia bidhaa za ndani.



0 Toa maoni yako.

WWF:Mbuga ya Selous Tanzania kupoteza Tembo wake

Rushwa ni moja ya sababu iliyochochea vita dhidi ya ujangili kutokwisha

Hifadhi ya wanyama pori ya taifa ya Selous Kusini mwa Tanzania inatajwa kuwa huenda ikapoteza tembo waliosalia ndani ya miaka sita ijayo iwapo hali ya ujangili itaendelea kwa kiwango kilichopo sasa.

Ripoti ya mfuko wa hifadhi ya wanyamapori na mazingira duniani,wwf imesema hifadhi Selous imepoteza asilimia tisini ya tembo wake,ambapo miaka 40 iliyopita kulikuwa na maelfu ya tembo.

Mahitaji makubwa ya nyara hizo na nchi ya China,kwa mjibu wa ripoti hiyo inatajwa kuwa ni hali inayochochea ujangili na mauaji ya idadi kubwa ya tembo.

Rais wa awamu ya tano wa Tanzania John Pombe Magufuli katika utawala wake ametanga kukomesha rushwa ambayo ndiyo imekuwa ikichangia kukua kwa vitendo vya ujangili.

"hifadhi hiyo ya Selous ni moja kati ya urithi wa dunia kufuatia kuwa na eneo kubwa la wanyama pori lililosalia Barani Afrika.
0 Toa maoni yako.

Ukawa kuzunguka nchi nzima

Na Khamis Mkotya, Dodoma

VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vinakusudia kufanya ziara ya kuzunguka nchi nzima kuwaeleza wananchi kilichotokea bungeni hadi wabunge wa upinzani wakafukuzwa.

Mpango huo ulitangazwa jana na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe katika viwanja vya Bunge alipozungumza na waandishi wa habari.

Alifanya hivyo ikiwa ni siku moja tangu wabunge saba wa upinzani wasimamishwe kuhudhuria vikao vya Bunge, baada ya kukutwa na makosa ya kudharau kiti na kufanya fujo bungeni.

Uamuzi huo wa Bunge ulitolewa kwa kuridhia mapendekezo ya adhabu yaliyotolewa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, baada ya kuwahoji wabunge hao kutokana na kufanya vurugu katika mkutano wa pili wa Bunge wa Januari 27, 2016 kuhusu matangazo ya Bunge ‘Live’.

Wabunge waliowekwa kifungoni kwa vipindi tofauti ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee wote kutoka Chadema na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe wa Chama cha ACT- Wazalendo.

Mbowe alisema baada ya kutoka bungeni, wabunge wa kambi hiyo watakutana kujadili na kupanga mikakati ya pamoja kufanya siasa nje ya Bunge, kutokana na mwenendo wa kiongozi huyo wa Bunge na hatua ya wabunge wa upinzani kufukuzwa.

“Siasa haifanywi ndani ya Bunge pekee, siasa inafanywa pia nje ya Bunge na tutafanya siasa nje ya Bunge, tutakwenda kuwashitaki kwa wananchi juu hiki kilichotokea bungeni wananchi waelewe,” alisema.

Alipoulizwa anazungumziaje habari ya kufanya siasa bungeni wakati kinachopaswa kufanywa ndani ya Bunge ni hoja, Mbowe alisema: “Mimi sijui hoja ni nini na siasa ni nini? Lakini kwangu mimi kinachofanyika bungeni ni siasa kwa asilimia 100, tunakwenda kukutana na wenzetu kupanga,” alisema.

Hiyo itakuwa mara pili kwa vyama vya upinzani kwenda kwa wananchi. Mwaka 2007 aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wakati huo akiwa Chadema, aliwahi kusimamishwa kwa miezi mitatu kuhudhuria vikao vya Bunge kutokana na hoja ya Buzwagi.

Kutokana na adhabu hiyo, Chadema kwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kiliratibu na kufanya ziara nchi nzima kuwaeleza wananchi kuhusu adhabu ya Zitto.

Zitto aliibua hoja binafsi akituhumu liyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kwamba alisaini mkataba wa Buzwagi hotelini Uingereza kinyume na utaratibu.

Waanza kumsusia Dk. Tulia

Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni jana ilianza kutekeleza azimio lake la kutokuwa na imani na Naibu Spika, Dk. Ackson Tulia.

Hatua hiyo ilijitokeza jana asubuhi wakati wabunge wa kambi hiyo walipotoka nje baada ya Naibu Spika kumaliza kusoma dua ikiwa ni ishara ya kuanza kwa shughuli za Bunge.

Juzi kambi hiyo ilitangaza kutokuwa na imani na Naibu Spika kwa kile kilichoelezwa kuwa kiongozi huyo analiyumbisha Bunge katika kutekeleza majukumu yake.
0 Toa maoni yako.

Mawaziri Yona na Mramba Waanza Kutumikia Kifungo cha nje...Wakabidhiwa Vifaa vya Usafi

Mawaziri wa zamani Basil Pesambili Mramba na Daniel Yona wameripoti leo katika hospitali ya Sinza Palestina na kukabidhiwa vifaa kwa ajili ya kufanya usafi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliridhia Mawaziri hawa wastaafu kutumikia adhabu ya kifungo cha nje kwa kufanya usafi katika maeneo ya kijamii ikiwemo Hospitali ya Sinza Palestina.
0 Toa maoni yako.

Dk. Manyaunyau Ahukumiwa Jela Miaka 3 Kwa Kushindwa Kufufua Maiti

Mkazi wa Dar es Salaam, Dunia Salumu maarufu kwa jina la Dk. Manyaunyau, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na kulipa fidia ya Sh milioni 10 baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha Sh milioni 29.6 kwa njia ya udanganyifu.

Manyaunyau anadaiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji, Tekra Modesta kama malipo ya kazi ya kumfufua marehemu kaka yake aliyefahamika kwa jina moja la Modest ambaye alifariki dunia miaka kadhaa iliyopita.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Flora Haule, alisema mtuhumiwa huyo ametiwa hatiani baada ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka kujitosheleza.

“Mahakama inatoa hukumu kwa mtuhumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa fidia ya Sh milioni 10 baada ya kumaliza kutumikia kifungo chake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,” alisema Hakimu Flora.

Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne ambao wote waliithibitishia mahakama juu ya mtuhumiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa njia za udanganyifu.

Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Estar Kyala, aliiambia mahakama kuwa hakuna kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa na hivyo kuiomba kutoa adhabu kali ili kuwa fundisho kwa wote wenye tabia kama hizo.

Katika maelezo ya awali, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mlalamikaji kama malipo ya tukio la kutaka kumfufua kaka wa mlalamikaji.

Ilielezwa kuwa mtuhumiwa alipokea fedha hizo kwa awamu mbili tofauti ambapo awali Mei 2007 jijini Dar es Salaam alipewa kiasi cha fedha ambacho hakikufahamika.

Mei Mosi, mwaka 2008 mtuhumiwa alipokea kiasi kingine cha fedha kama malipo kwa ajili ya kumalizia kazi yake ya kumfufua marehemu ambaye ni ndugu wa mlalamikaji jambo ambalo alishindwa kulitekeleza.

Manyaunyau amejizolea umaarufu mkubwa katika maeneo mengi nchini kwa kile kinachodaiwa kuwa anao uwezo wa kutibu na kuwafichua wachawi popote walipo sambamba na staili yake ya kunyonya damu ya paka akiwa katika shughuli zake za uganga.

Katika tukio lililovuta wakazi wengi wa Dar es Salaam, Manyaunyau anadaiwa kumwibua nyoka ambaye alikuwa tishio na kuzusha hofu kubwa kwa wakazi wa maeneo ya Manzese Midizini ambapo ilidaiwa kuwa alikuwa akiwagonga watu katika mazingira ya kutatanisha katika njia inayopita kwenye makaburi.

Inaaminika kuwa baada ya kuitwa, Dk. Manyaunyau aliweza kumuibua nyoka huyo na kuonekana hadharani tukio lililohisiwa kuwa ni la kimazingara zaidi.
0 Toa maoni yako.

Kesi ya Ubunge wa David Kafulila Yaahirishwa Hadi Jumatatu Novemba 30 Baada ya Mlalamikiwa Kutofika Mahakamani

Kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila, kupinga matokeo ya ubunge yaliyomtangaza mshindi Husna Mwilima, katika jimbo hilo, imeahirishwa hadi Novemba 30, mwaka huu.
Kesi hiyo ipo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, John Utamwa.

Jaji Utamwa alisema mlalamikiwa (Mwilima), katika madai hayo, hakupelekewa wito wa mahakama, hivyo anaamuru wito utolewe ili mlalamikaji aende mahakamani kujibu madai hayo ambayo anatetewa na mwanasheria wa serikali, Juma Masanja.

Akizungumza baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili wa mlalamikaji, Daniel Rumenyela, alidai mlalamikiwa (Mwilima), hakupatikana kwa ajili ya kuitwa shaurini hata akipigiwa simu hapokei.

“Kutokana na mlalamikiwa wa kwanza kutopatikana, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora inatoa siku tatu hadi Novemba 30, mwaka huu, (Jumatatu), ajibu madai hayo,” alisema Rumenyela.

Kesi hiyo namba 2 ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo, pia ina washtakiwa wengine ambao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza ambaye alikuwa Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hii ndogo ya awali kabla ya kesi ya msingi, Mahakama itaamua gharama ambazo Kafulila atatakiwa kulipa kama gharama za dhamana ambayo kisheria kwa washtakiwa watatu haizidi Sh. milioni 15.

Katika kesi ya msingi, Kafulila anaomba Mahakama imtangaze mgombea aliyepata kura nyingi kwani aliyetangazwa siye mbunge halali kutokana na kupata kura chache.

Katika shauri hilo, Kafulila alimtaja Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mrisho Gambo, kama wahusika waliofikisha ujumbe huo toka juu Oktoba 28, mwaka huu, saa 8:00 mchana kwa Msimamizi wa Uchaguzi kushinikiza matokeo batili kutangazwa.
0 Toa maoni yako.

MAZISHI YA MAWAZO BADO KIZUNGUMKUTI. CHADEMA KUTINGA MAHAKAMANI.

Na:George Binagi-GB Pazzo @BMG
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kimesitisha shughuli za mazishi ya aliekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoani Geita marehemu Alphonce Mawazo, baada ya jeshi la polisi Mkoani Mwanza kuzuia zoezi la kuuaga mwili wake lililokuwa limepangwa kufanyika juzi jumamosi Jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe alibainisha hayo jana wakati akizungumza na Wanahabari Mkoani Mwanza, ili kutoa msimamo wa Chama baada ya kuwepo kwa mazungumzo baina yake na familia ya marehemu Mawazo.

Alisema kuwa baada ya mazungumzo hayo, Chadema pamoja na familia ya marehemu Mawazo wamekubaliana kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kufungua shauri la kuomba tafsiri ya Kimahakama juu ya zuio hilo la jeshi la polisi kuzuia mwili wa marehemu Mawazo kuagwa Jijini Mwanza kabla ya Kwenda kuzikwa Kijijini kwake Chikobe katika Wilaya ya Busanda Mkoani Geita.

Nae Mchungaji Charles Lugiko ambae ni baba mlezi wa marehemu Mawazo, alisema anasikitishwa na hatua iliyochukuliwa na jeshi la polisi ya kuzuia mwili wa marehemu Mawazo kuagwa Jijini Mwanza ambapo ameeleza kuwa na matumaini makubwa ya kwamba mahakama itatenda haki juu ya suala hilo.

Frederick Sumaye pamoja na Edward Lowasa ambao ni Viongozi Waandamizi wa Chadema, walisema hatua ya jeshi la polisi kuzuia mwili wa Mawazo kuagwa Jijini Mwanza si sawa na kwamba inaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kupitia kwa Kamanda wake Charles Mkumbo, lilizuia zoezi la mwili wa marehemu Mawazo Kuagwa Jijini Mwanza, kwa madai kwamba limepokea taarifa za kiitelejensia za kuwepo baadhi ya vikundi vya watu kutumia mwanya huo kufanya fujo na hivyo kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

Aidha Kamanda Mkumbo aliitaja sababu nyingine kuwa ni uwepo wa mlipuko wa Ugonjwa wa Kipindupindu Mkoani Mwanza, ambao umesababisha jeshi hilo kutoruhusu mikusanyiko ya aina yoyote inayoweza kusababisha ugonjwa huo kuenea zaidi kwa mjibu wa wataalamu wa afya ambapo lilishauri zoezi la kuaga mwili huo kufanyika Mkoani Geita ambapo mazishi ya marehemu Mawazo yatarajiwa kufanyika.

Katika uchaguzi uliomalizika hivi karibuni, marehemu Alphone Mawazo alikuwa mgombea ubunge Jimbo la Busanda Mkoani Geita kupitia Chadema, akiwa pia ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo ambapo aliuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na mashoka na watu wasiojulikana jumamosi iliyopita ya Novemba 14 mchana huku kifo chake kikihusishwa na uhasama wa kisiasa.
0 Toa maoni yako.

Saed Kubenea Kumburuza Mahakamani Spika wa Bunge Job Ndugai Kwa Kuvunja Kanuni Na Kuwaruhusu Polisi Kuingia Bungeni

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema atamfikisha mahakamani Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kuvunja kanuni baada ya kuwaingiza polisi ndani ya ukumbi wa chombo hicho.

Polisi hao waliingia ndani ya ukumbi huo wiki iliyopita wakati Rais John Magufuli alipofika kwa ajili ya kuhutubia Bunge.

Kubenea alisema kitendo cha askari kuingia ndani ya Bunge kwa mara ya mwisho kilitokea nchini Uingereza mwaka 1930 na hakijawahi kutokea tena isipokuwa nchini.

Alisema kuwa kesi hiyo anatarajia kuifungua Mahakama Kuu wiki ijayo kwa ajili ya kutaka tafsiri ya kanuni hiyo.

Hata hivyo, mkurugenzi wa shughuli za Bunge, John Joel alisema hakuna kanuni iliyovunjwa kwa askari hao kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge.
   Wakati Kubenea akiandaa mpango huo, Kamati ya Wabunge CUF imesema Spika Ndugai ndiye chanzo cha yaliyotokea bungeni.

Ijumaa wiki iliyopita wakati Rais akiingia kutoa hotuba ya kuzindua Bunge, wabunge hao walipiga kelele wakitaja jina la mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuonyesha msimamo wao dhidi ya uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa visiwa hivyo.

Walipiga kelele hizo wakati Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein akiingia kwenye ukumbi huo na baadaye wakati Dk Magufuli akiingia ukumbini na wakagoma kunyamaza hadi walipotakiwa kutoka nje na askari kuitwa ndani.

Wabunge wa upinzani wanadai kuwa Dk Shein si Rais wa Zanzibar, wala makamu wake wa pili, Balozi Seif Ali Iddi na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho kwa madai kuwa muda wao uliisha Novemba 2, baada ya Uchaguzi Mkuu.

Jana wabunge wa CUF chini ya Mwenyekiti wake, Juma Hamad Omary walitoa tamko lililokemea na kutoa tahadhari kwa mambo mawili huku wakimtaka Ndugai kutoyumbishwa na Serikali.

Katibu wa Umoja huo, Hamudu Hassan Bobal alisema vurugu zisingetokea endapo Bunge hilo lingezingatia tamko la barua ya Ukawa na kusikilizwa hoja ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyeomba mwongozo akitaka kujua Dk Shein na wenzake wanaingiaje bungeni wakati madaraka yao yaliisha tangu Novemba 2.
0 Toa maoni yako.

Wabunge Wagonga Mwamba Kwa Rais Magufuli......Agoma Kuwaongoza Hela Ya Posho,Apunguza Mikopo Ya Mashangingi

Wakati Serikali ikihaha kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zake, wabunge wameingia kwenye mvutano na ofisi ya Bunge kuhusu fedha ambazo wanastahili kupewa kwa ajili ya kununulia magari yao.

Mwaka 2010, wabunge walilipwa Sh90 milioni kwa ajili ya ununuzi wa magari hayo aina ya Toyota Land Cruiser (hardtop), ambayo ni vitendea kazi vyao. Wabunge hutakiwa kulipa nusu ya fedha hizo wkati nyingine ni mchango wa Serikali.

Lakini wakati gharama za maisha zikipanda huku thamani ya Shilingi ikiporomoka kulinganisha na Dola ya Marekani na hivyo kusababisha bidhaa kupanda bei, wabunge wamekataa kulipwa kiasi hicho cha fedha mwaka huu na badala yake wanataka walipwe kulingana na bei ya sokoni ya magari aina hiyo.

Wabunge wanataka walipwe Sh130 milioni ambazo wanasema ni bei ya magari hayo kwa sasa baada ya kupanda bei. Hata hivyo ombi hilo limegonga mwamba

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina, baadhi ya wabunge walisema mara baada ya kujisajili bungeni kwa ajili ya uzinduzi wa Bunge la Kumi na Moja, katibu wa chombo hicho, Dk Thomas Kashililah alifanya kikao na wabunge wote ili kuwapa taratibu lakini pia kuwafahamisha stahili wanazopaswa kupata kama wabunge.

“Katibu alitujulisha kuwa hakuna ongezeko lolote la posho, hivyo tunapaswa kulipwa kiasi kilekile cha Sh300,000 kwa siku .

"Lakini pia alisema tutapewa Sh90 milioni kwa ajili ya mkopo wa garibadala ya milioni 120 ,” alisema mmoja wa wabunge hao.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, suala hilo liliibua mjadala na kusababisha wabunge kuhoji iweje kiwango hicho kitumike katika Bunge la Kumi na Moja, miaka mitano baada ya wabunge wa Bunge la 10 kupewa kiasi hicho.

“Unajua magari tunayotakiwa kununua ni Toyota Land Cruiser Hardtop, na ukweli sasa thamani ya magari hayo imepanda sana huwezi kuifananisha na mwaka 2010 wakati wa Bunge la 10,” alisema mbunge mmoja.

Wabunge hao walitaka walipwe kiasi cha Sh130 milioni kwa madai kuwa ndiyo bei ya sokoni ya magari aina hiyo.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Anatropia Theonest amesemahawajakataa fedha hizo, lakini thamani ya Dola imepanda hivyo kusababisha thamani ya magari hayo kupanda pia.

“Hakuna asiyejua kwamba thamani ya Dola imepanda na kwa kawaida kila Bunge kunakuwa na ongezeko la Sh30 milioni. Mfano Bunge la Tisa walipewa Sh60milioni la 10 wakapewa Sh90milioni, hivyo ilipaswa sasa iwe Sh 120mililioni ili kuendana na soko,” alisema mbunge huyo.

Akizungumzia sakata hilo,naibu katibu wa Bunge, John Joel alisema jukumu la ununuzi wa magari ya wabunge, lipo chini ya Serikali na siyo ofisi yake hivyo ni bora wangeulizwa wenye jukumu hilo.

“Tunachofamu sisi mbunge anatakiwa apewe vitendea kazi likiwemo gari, lakini wanaohusika na hilo ni Serikali,” alisema.

Alisema ofisi ya Bunge hushauriana na Serikali namna ya kutoa huduma kwa wabunge na kwamba kwa jinsi anavyofahamu, mpaka jana watunga sheria hao walikuwa hawajapewa fedha yoyote ya kununua magari kwa awamu hii, hivyo wanasubiri utaratibu.

Wakati Joel akisema Serikali ndiyo inahusika, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue aliurudisha mpira kwenye ofisi hiyo ya Bunge, akisema uongozi wa bunge umekwisha pewa maelekezo yote na serikali juu ya ununuzi wa magari hayo, hivyo akamtaka mwandishi akawaulize wao ( uongozi wa bunge)

Katika kukusanya fedha za kuwezesha kutekeleza mipango ya Serikali na ahadi alizotoa wakati wa kampeni, Rais John Maguguli alitangaza hatua mbalimbali za kudhibiti matumizi, na akawaeleza wabunge mwishoni mwa wiki kuwa hataweza kufanikiwa iwapo hatapata ushirikiano wao.

Katika kuonyesha kuwa anatoa kauli thabiti, Dk Magufuli aliagiza fedha ambazo zilichangwa na taasisi mbalimbali za fedha kwa ajili ya hafla za kuwapongeza wabunge, zielekezwe kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Tayari Rais ameshafuta safari za nje isipokuwa kwa kibali cha Ikulu baada ya mtu anayetaka kusafiri kutimiza masharti kadhaa, likiwamo linalomtaka aeleze faida ya safari yake na kama iwapo hatasafiri, nchi itaathirika vipi.
0 Toa maoni yako.

Utata Watawala Kifo cha Ghafla Cha Msemaji Wa Madereva, Rashid Saleh

Aliyekuwa Katibu na Msemaji wa Chama cha Madereva, Rashid Saleh amefariki dunia ghafla huku chanzo cha kifo chake kikizua utata miongoni mwa wananchama wa chama hicho na wananchi.

Taarifa za awali kifo cha Rashid Swaleh zilielza kuwa alifariki baada ya kuugua ghafla ugonjwa ambao bado haujabainika.

Madereva na wananchi wengine walifika katika hospitali ya Muhimbili wakiwa na majonzi makubwa huku wakisubiri mwili huo wa marehemu upimwe ili kubaini chanzo cha kifo chake.

Baadhi ya madereva waliozungumza na waandishi wa habari walieleza kusikitishwa na msiba huo wa ghafla na kueleza kuwa huenda msemaji wao aliyekuwa anapigania kwa nguvu zote haki zao amenyamazishwa.

“Sisi kama madereva hatutakubali, kama kosa lake yeye ni kutetea haki za watu, hili ni tatizo,” alisema mmoja wa madereva hao aliyejitambulisha kwa jina la Shaban Mdem.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alifika katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuwataka madereva hao kutokata tama bali waendelee kudai haki zao huku wakisubiri majibu ya madaktari kubaini chanzo cha kifo cha msemaji wao.

“Hii isiwakatishe tamaa kuendelea kudai haki zenu ambazo ni za msingi kutoka kwa ajili wenu,” alisema huku akiwasihi kutofifishwa moyo katika kutafuta haki zao za msingi.
0 Toa maoni yako.

Mmoja wa Watano Waliookolewa Mgodini Baada ya Kufukiwa Kifusi Kwa Siku 41 Afariki Dunia

MMOJA wa majeruhi watano waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kutokana na kufukiwa na kifusi cha mchanga na kukaa siku 41 chini ya mgodi na kuokolewa, Onyiwa Kaiwao (55) amefariki dunia.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Joseph Ngowi amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema kuwa chanzo cha mauti hayo ni kutokana na majeruhi huyo kutapika akiwa amelala hali ambayo ilifanya matapishi hayo kuingia katika njia ya hewa.

Dk Ngowi alisema Kaiwao alifariki jana saa sita mchana na kuongeza kuwa pia alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa nimonia unaosababishwa na baridi kali hali iliyomfanya kutokuwa katika hali ya kawaida tofauti na wenzake.

Hata hivyo, Dk Ngowi alisema majeruhi huyo pia alikuwa na matatizo katika utumbo, na hivyo kila akienda haja kubwa alikuwa akitoa magome ya miti waliyokuwa wakiyatumia kama chakula wakati wakiwa chini ya ardhi.

“Jana (juzi) tuliwachukua vipimo waathirika wote watano na kuonesha kuwa hali zao ni nzuri, lakini Onyiwa alionesha kutokuwa na maendeleo mazuri tofauti na wenzake na ghafla akiwa amelala alijitapikia hali ambayo matapishi hayo yaliingia katika mirija ya hewa na kuziba hali iliyosababisha kifo chake,” alisema Dk Ngowi.

Alisema hali za majeruhi wengine wanne zinaendelea vizuri, na wanaendelea na mazoezi huku wakila wenyewe hali ambayo wamepanga kesho kuangalia uwezekano wa kuwafanyia vipimo kwa mara nyingine tena.

Aidha, Dk Ngowi alisema endapo hali zao hazitakuwa nzuri na kubadilika, watawahamishia katika Hospitali ya Rufaa kwa ajili ya uangalizi wa juu hali ambayo watapata mabadiliko zaidi ya afya zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shigitwa (SHIGOMIKO), Hamza Tandiko alisema wakiwa wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Nyangalata wamekipokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwenzao na kuwataka waliobaki kutokata tamaa Mungu atawasaidia watapata nafuu.

“Sisi kama wachimbaji hatupingani na Mwenyezi Mungu tulijitahidi kadri ya uwezo wetu kuokoa maisha yao kwa kushirikiana na uongozi wa Hospitali ya Wilaya, lakini kwa mapenzi ya Mungu ameamua kumchukua Onyiwa akapumzike na hakuna mtu anaweza kuzuia kifo,” alisema Tandiko.

Wachimbaji hao wadogo watano waliokolewa kutoka katika mgodi huo wiki iliyopita baada ya kukaa kwa siku 41 kutokana na kufukiwa na kifusi. Mwenzao mmoja alifia mgodini wakati wakisubiri majaliwa ya kuokolewa.
0 Toa maoni yako.

Mke wa Lowassa Akataa Ubunge Wa Viti Maalumu Aliopewa na Chadema

Mke wa aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, Regina Lowassa, ameikataa nafasi ya ubunge wa viti maalum aliyopewa na kamati Kuu ya chama hicho cha upinzani.

Kwa mujibu taarifa wa kutoka familia ya Lowassa iliyotufikia, Regina anaichukulia kwa heshima kubwa nafasi hiyo, lakini anaamini ataweza kushughulikia matatizo ya akina mama na watoto akiwa nje ya bunge.

"Naishukuru kamati Kuu ya chama changu kwa heshima hii kubwa waliyonipa na ninaithamini sana, lakini naamini nitaendeleza mapambano ya kuwaletea akina mama mabadiliko kwa ufanisi zaidi nikiwa nje ya bunge," amesisitiza mke huyo wa waziri mkuu wa zamani katika taarifa hiyo.

Kamati Kuu ya Chadema ilifikia uamuzi wa kumpa Regina nafasi ubunge viti maalum kutokana na mchango mkubwa aliyoutoa wakati wa kampeni ambao kwa kiasi kikubwa ulisaidia upatikanaji wa majimbo mengi tofauti na uchaguzi wa mwaka 2010.
0 Toa maoni yako.

Rais John Pombe Magufuli Afanya Ziara Ya Ghafla Wizara Ya Fedha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.John Pombe Magufuli akisani kitabu cha wageni baada ya kufika Wizara ya Fedha.


...Akikagua utendaji kazi wa wafanyakazi mbali mbali wizarani hapo.

Akitembea kwa miguu na maofisa usalama kuelekea Wizara ya Fedha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza kwa kutembea kwa miguu kutoka Ikulu hadi katika Wizara ya Fedha na kukagua utendaji kazi wa wafanyakazi wa ofisi hizo, hata hivyo alikuta baadhi ya maofisa wakiwa nje ya ofisi zao.
0 Toa maoni yako.

Serikali Yatoa Picha Rasmi ya Rais wa Awamu ya Tano Dk. John Pombe Magufuli

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji wa Serikali Bw. Assah Mwambene akiwaonesha waandishi wa Habari picha rasmi ya Rais wa Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ambayo itakuwa ikitumika katika ofisi za Serikali na Binafsi ambayo inapatikana Idara ya Habari (MAELEZO) kwa gharama ya Shilingi 15,000/=
0 Toa maoni yako.

Masanja Mkandamizaji Kuwania Ubunge Jimbo La Ludewa.

Wagombea tisa akiwemo mdogo wake marehemu Deo Filikunjombe na mchekeshaji Masanja Mkandamizaji wamejitosa kuwania ubunge wa jimbo la Ludewa,Mkoani Njombe kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Uchaguzi wa kumpata Mbunge wa jimbo hilo ulilazimika kuhairishwa baada ya kutokea kifo cha aliyekuwa mbunge na mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM, Deogratius Filikunjombe.

Miongoni wa waliojitokeza kwenye kinyang'anyiro hicho ndani ya CCM ni mdogo wa marehemu, Phillipo Filikunjombe na msanii wa vichekesho na muimbaji wa nyimbo za Injili Emmanuel Mgaya maarafu kwa jina la 'Masanja Mkandamizaji'.

Na wagombea wengine ni Johnson Mgimba, James Mgaya, Zephania Jwahula, Deo Ngalawa, Dk Evaristo Mtitu na Simon Ngatuka.
0 Toa maoni yako.

Lowassa, Sumaye wakosa hafla ya kuapishwa JPM

CHANZO MWANCHI    Kwa ufupi
         Juzi mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema vyama vinavyounda Ukawa havitahudhuria sherehe hizo kwa kuwa vinapinga jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa na kuwataka wananchi wapenda mabadiliko na wapenda haki, viongozi na wabunge wa chama hicho kutohudhuria shughuli hiyo.By Fidelis Butahe, Mwananchi

Dar es Salaam. Mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye jana walikuwa miongoni mwa makada wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao hawakuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais John Magufuli.

Ni kawaida kwa mawaziri wakuu wa zamani kuwa sehemu ya wageni rasmi kwenye sherehe hiyo ya kihistoria, lakini jana wawili hao, ambao walitangazaa kuihama CCM mwezi Julai na kuhamia kambi ya upinzani, hawakuwamo kwenye jukwaa la wageni rasmi.

Juzi mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema vyama vinavyounda Ukawa havitahudhuria sherehe hizo kwa kuwa vinapinga jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa na kuwataka wananchi wapenda mabadiliko na wapenda haki, viongozi na wabunge wa chama hicho kutohudhuria shughuli hiyo.

Ukawa ilimsimamisha Lowassa kugombea urais na kwa mara kwanza mgombea wa upinzani alipata kura milioni 6.07, ambazo ni karibu ya mara tatu ya kura alizopata Dk Willibrod Slaa mwaka 2010.

Hata hivyo, viongozi wa Ukawa walipinga matokeo yaliyokuwa yakitangazwa, wakisema ni tofauti na yale yaliyokusanywa na mawakala wao na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusitisha utangazaji.

Lowassa, ambaye alikuwa akipeperusha bendera ya Chadema, alikuwa akiungwa mkono na NLD, NCCR-Mageuzi na CUF ambavyo vinaunda Ukawa.

Lowassa alihamia Chadema baada ya CCM kutompitisha kuwa mgombea wa urais, baadaye kundi la makada kutoka CCM lilimfuata, akiwamo Sumaye, Dk Makongoro Mahanga, aliyekuwa Waziri wa Kazi na Ajira, na Kingunge Ngombare-Mwiru, mwanasiasa mkongwe na waziri wa zamani. Mbowe alisema juzi kuwa sababu kubwa ya Ukawa kususia sherehe hizo ni kutaka kuonyesha nchi na dunia nzima kuwa hawakubaliani na mchakato wa uchaguzi, hasa matokeo ya urais ambayo kwa mujibu wa Katiba ya nchi, mwenyekiti wa NEC akishayatangaza, hakuna mahali pa kuyapinga.

“Watawala wamechezea haki ya Watanzania ya kupiga kura. Kura zimehesabiwa kama karatasi za kawaida tu. Matokeo ya wagombea wetu yamehujumiwa waziwazi.

“Safari hii hujuma hazikuwa kificho. Kila mtu amejionea matokeo yaliyokuwa yanatangazwa na Jaji Lubuva si yale ambayo yalikuwa yamebandikwa vituoni,” alisema Mbowe juzi.

Ukawa pia ililalamikia kile walichoita “mchezo mchafu” waliofanyiwa wagombea wao wa ubunge katika majimbo mbalimbali, ikieleza kuwa walitangazwa washindi ambao hawastahili. Hata hivyo, juzi jioni Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya aliwaeleza wanahabari kuwa hawakuwa wamepata mwaliko wowote wa kuhudhuria sherehe hizo.


Katika hotuba yake fupi ya shukrani, Dk Magufuli aliwashukuru wagombea wenzake wa urais, akisema wamempa changamoto kubwa na amejifunza mengi kutoka kwao na kuwataka wapinzani washirikiane katika kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo.

0 Toa maoni yako.

Siri ya jina la Janeth kuwa wake wa marais

Ni wa Dk Magufuli, Paul Kagame, Yoweri Museveni
By Suzan Mwillo, Mwananchi
Kila mzazi anapokaribia kupata mtoto, moja ya mambo muhimu ambayo hufikiria juu ya jina la kumpatia baada ya kujifungua na mtoto kuishi duniani. Wazazi wengi huchukua muda kufikiria ni jina gani zuri la kumpa mtoto wao.

Kuna wakati baadhi ya wazazi hufikia hatua ya kuvutana kuhusu jina tu. Kuvutana huko kunatokana na umuhimu wa jina kwa sababu inaaminika kila jina lina maana yake na tabia zake zitaakisiwa nalo.

Kuna majina ambayo hupendwa sana kutokana na dhana kwamba watu wanaopewa majina hayo huwa na tabia nzuri, upeo mkubwa, uvumilivu na wengine bahati.

Je, ikitokea unabahatika kupata mtoto wa kike uliyemtafuta kwa muda mrefu, utampa jina gani?

Huenda jina Janeth likawa miongoni mwa matatu au 10 utakayoorodhesha ili kuchagua moja la kumpa binti yako. Kama halitakuwapo basi fanya mpango wa kuliweka kwa sababu jina hilo ndiyo habari ya mjini kwa sasa.

Kwa nini jina la Janeth ni habari ya mjini?

Siku Dk John Magufuli alipopitishwa na CCM kuwania nafasi ya urais, baadhi ya watu walidai ikiwa angepata nafasi hiyo Afrika Mashariki ingeongeza idadi ya wake wa marais wenye majina ya Janeth. Imekuwa hivyo, mke wa Rais Magufuli aliyeapishwa jana anaitwa Janeth.

Mke wa Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni anaitwa Janet Museveni, na mke wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame anaitwa Jeanette.

Licha ya kwamba jina la mke wa Kagame linaandikwa tofauti na mengine, lakini matamshi ya majina hayo ni sawa.

Kwa mujibu wa kamusi ya Encyclopaedia jina la Jeannette, asili yake ni Ufaransa ndiyo maana linaandikwa tofauti na Janeth ambalo asili yake ni Scotland.

Kama hujui wakati jina Janeth hupewa mtoto wa kike kinyume cha jina hilo ambao hupewa mtoto wa kiume ni John. Kwa hiyo majina ya Janeth na John Magufuli yameshabihiana vilivyo.

Kutokana na utuki huo majina ya wake za marais hao sasa yamekuwa habari ya mjini. Kuna baadhi ya watu wanatamani kuwapa majina watoto wao kwani huenda wakawa ‘ma First Lady’ watarajiwa.

Gumzo kwa sasa au watu wengi wanahoji iwapo marais hao watakutana wakiwa na wake zao, likataitwa jina hilo, itakuwaje?

Maana ya jina Janeth

Kwa mujibu wa kamusi ya tafsiri ya majina, jina Janeth (Kiebrania) ambalo asili yake ni Uingereza linamaanisha Mungu ni mwenye neema.

Sifa za wanawake wenye jina hilo zimedadavuliwa zaidi na tovuti ya ‘sevenreflections’.

Tovuti hiyo inawaelezea wanawake wenye jina hilo kuwa ni waaminifu, wema, wenye vipaji na wavumbuzi wa mambo.

Wanawake wenye majina hayo ni jasiri, wavumilivu, wabunifu, wadadisi, wanafahamu nini wanataka, siyo tegemezi na viongozi wazuri.

Janeth Magufuli

Kitaaluma ni mwalimu. Alikuwa anafundisha Shule ya Msingi Mbuyuni masomo ya Jiografia, Historia na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama). Lakini ameacha kutokana na wadhifa huo mpya aliopata mumewe. Hata hivyo, hakuwa maarufu wakati alipokuwa anafundisha shuleni hapo licha ya kuwa mke wa waziri mchapakazi na sasa rais.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Dorothy Malecela anamzungumzia kama mwalimu mchapakazi na anayefahamu majukumu yake, mwenye upendo, mnyeyekevu na asiye na makuu, sifa ambazo zinaendana na jina lake.


Janet Museveni

Licha ya kuwa Mke wa Rais Museveni tangu mwaka 1986 mumewe alipoingia madarakani, pia ni mwanasiasa, na ni Waziri wa Karamoja.


Jeannette Kagame

Alipata wadhifa wa mke wa rais tangu mwaka 2000, Kagame alipoingia madarakani hadi sasa akiwa pia mwanaharakati, mwanzilishi wa taasisi ya Imbuto inayosaidia katika shughuli za maendeleo katika sekta ya afya, elimu na uchumi.

Mwanamke mwingine maarufu duniani mwenye jina hilo ni Janeth Jagan, aliyekuwa Rais wa Guyana kati ya mwaka 1997 na 1999.

0 Toa maoni yako.

Kikwete Aaga Kwa Kusamehe Wafungwa 4,160

RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,160 katika kuaga na kukabidhi madaraka ya Serikali kwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

Dk Magufuli aliapishwa jana kuwa Rais wa Tano wa Tanzania katika sherehe zilizofana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku Kikwete akimaliza miaka yake 10 ya kuongoza nchi kama ilivyoelekezwa na Katiba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam, kati ya wafungwa hao, wafungwa 867 wataachiwa huru na wafungwa 3,293 watapunguziwa vifungo vyao na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya vifungo vyao vilivyobaki.

“Ni mategemeo ya Serikali kwamba wafungwa watakaoachiwa huru watarejea katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa na watajiepusha na utendaji makosa ili wasirejee tena gerezani,”alisema Chikawe katika taarifa hiyo.

Chikawe aliwataja walionufaika na msamaha huo kuwa ni wafungwa wote wapunguziwe moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika ibara ya 1 (i-xix).

Aliwataja wengine kuwa ni wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu, saratani ambao wako kwenye hatua ya mwisho ambao watathibitishwa na waganga chini ya Mganga mkuu wa mkoa au wilaya.

Pia wazee wenye umri zaidi ya miaka 70, wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya na walemavu wa mwili na akili na ulemavu huo uthibitishwe na jopo la waganga.

Kwa mujibu wa Chikawe, msamaha hautawahusu wafungwa wenye adhabu za kunyongwa, waliohukumiwa kunyongwa na adhabu hiyo baadaye kubadilishwa kuwa kifungo cha maishaau kifungo gerezani.

Wengine ni wafungwa waliotumikia kifungo kwa makosa ya usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya, makosa yanayohusu uombaji, upokeaji na utoaji rushwa, unyang’anyi na kujaribu kutenda makosa hayo, kubaka, kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.

Aidha, makosa mengine ambayo vifungo vyake haviko kwenye msamaha huo ni makosa ya kuwapa mimba wanafunzi, wizi wa magari, pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo, matumizi mabaya ya madaraka, waliowahi kupunguziwa vifungo na Rais.

“Wengine ni waliopatikana na hatia kwa kuwazuia watoto kupata masomo, utekaji watoto, usafirishaji binadamu, ukatili dhidi ya albino, usafirishaji nyara za Serikali na ujangili,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Mengine ni wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi na ubadhirifu wa fedha za Serikali, kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi halali na wafungwa wanaotumikia vifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole Sheria Namba 25 ya Mwaka 1994 ya Sheria ya Huduma kwa Jamii Namba 6 ya Mwaka 2002.
0 Toa maoni yako.

Watu zaidi watoroka mapigano Burundi

Watu wanahofia yatakayotokea baada ya kupita kwa makataa ya kusalimisha silaha Jumamosi

Watu zaidi wameendelea kutoroka mji wa Bujumbura nchini Burundi baada ya kuongezeka kwa mapigano.

Jumatano, watu wanne waliuawa katika mitaa miwili ya mji huo mkuu. Maafisa wa serikali wanasema wawili waliuawa kwenye ufyatulianaji wa risasi kati ya makundi ya watu wenye silaha na maafisa wa polisi usiku.

Mtu wa tatu aliuawa na watu wenye silaha, ambao polisi wamesema walikuwa waasi. Bado haijabainika ni nini kilichomuua mtu wa nne.

Mauaji yamekuwa yakitokea nchini Burundi tangu Aprili baada ya kuanza kwa maandamano ya kupinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.Image copyrightReutersImage captionWatu wengi, akiwemo jenerali mmoja mkuu, wameuawa Burundi

Rais huyo ameahidi kuwasaka na kuwaadhibu wanaosababisha mauaji hayo.

Mitaa ya Mutakura na Cibitoke ilifahamika sana kwa maandamano ya kupinga hatua ya Bw Nkurunziza kuwania urais tena.

Aliapishwa mwezi Julai kwa muhula wa tatu, ambao wapinzani wake wanasema ni kinyume na katiba

Tangu wakati huo, visa vimekuwa vikiripotiwa vya mauaji ya wafuasi na wapinzani wa serikali.

Rais huyo amewapa watu wenye silaya makataa ya hadi Jumamosi kuzisalimisha la sivyo maafisa wa usalama watatumia kila njia kusitisha mapigano hayo.

Mwandishi wa BBC mjini Bujumbura Prime Ndikumagenge anasema wengi wa wanaotoroka makwao walionekana wamebeba godoro na nyungu za kupikia wakiondoka.

Baadhi wanasema wanahofia yatakayojiri baada ya makataa hayo ya rais kupita Jumamosi.
0 Toa maoni yako.
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company