NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

Mahali: TAG Ushiri Rombo: Tarehe 28:2:2019. Na Mwalimu Oscar Samba.
.

Mwanzo 2:18 Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.
Mwanamke ni msaidizi, andiko hilo lipo kabla ya dhambi kuingia ulimwenguni, hakukuwa na mfumo wa kanisa ama kuabudu kama leo, au kama baada ya dhambi, kusudio la ndoa, au familia ni ili liwe kanisa, yaani tuliumbwa kwa ajili ya ibada !

Kwa hiyo, kanisa, lina mukutadha wa ndoa, kwa hiyo, dhima ya mwanamke kindoa au kifamilia, ina mashabihiano na ile ya kikanisa !

Waefeso 5:23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.
24 Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.

Kama ndivyo, mwanamke ameumbiwa kulichukulia kanisa kama anavyomchukulia mumewe, utendaji wa usaidizi kwa mume, ama kumuheshimu, uwe vivyo hivyo kwa kanisa, maana Kristo u kichwa huku.
Kumbuka hili Daima: Kuwa ni yule amchaye Mungu ndie asifiwaye: Mithali 31:30 Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa.

Jambo hili, likupe kuhakikisha una sifa ya uchaji, kama kweli unadhamiria kusifiwa na Kristo ambaye ndie kanisa, na hakika ukijipatia kibali au sifa njema kutoka kwa Bwana Yesu, ni umejipatia kutoka kwa kila mtu, jifunze kwa wakina Debora,Dorkasi, na wengine akiwemo yule Mariamu aliyempaka yale mafuta, hadi leo tukio hilo lingali likikumbukwa, sasa utafahamu kuwa utendaji wao mwema uliotokana na uchaji ndio uliopeleke kujizolea sifa hizo.

Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili ! Kwa hiyo ni hatari mno kujisifia vya mwilini, ila sifa zitokane na uchaji, ambao huzaa kazi njema !
MAJUKUMU YAKE KATIKA NAFASI KWENYE KANISA:

1.  Ni Mueneza Habari Njema, sifa njema kuhusu Mchungaji wake, kanisa lake, huduma ya kanisani, watumishi wa kanisani, na kila wasifu mzuri kulihusu.

Ni jukumu lake pia kumuelezea Kristo Yesu kwa wasio mjua, huyu ni mjumbe mzuri sana, maana mwanamke amepewa kinywa chenye uwezo wa kuzalisha maneno mengi, adui amekuwa akiwahi hili na kulitumia vibaya kwa umbea na misuto, ukizingatia pia amepewa uwezo wa kutoka mji huu ama nyumba hii na kwenda kwa ile, nia ni ili aeneze mema, ila adui amewatumia vibaya.

Mfano wa dhima hii kibiblia ni mwanamke yuke wa kisima cha Yakobo Msamaria: ( Yoh 4:7-42.) 

Alipofahamu uzuri wa Yesu, moja kwa moja aliacha mtungi wake na kwenda kueneza wema wake!

Yohana 4:28 Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu.

Kuna wakina mama au mabinti unakuta anafua nguo,au kukatakata kitunguu jikoni, ghafula huepua sufuria na kwenda mbio kwa jirani baada ya kusia umbea fulani, huku ni kukosa kujitambua ! Akisikia neno mbio ataaga na kutoka kanisani mapema utazani anawahi mtoto nyumbani, kumbe kuna sumu anaenda kumwaga kwa mpendwa ambaye hajaja kanisani. 

Huyu Msamaria, kaacha mtungi, na kwenda kueneza habari za Yesu, wewe je unaacha na kwenda kueneza nini? Aibu ya kanisa, udhaifu wa mama mchungaji wako, udhaifu wa kiongozi wako wa idara, ama unapeleka madhaifu ya kikanisa kwa wapendwa na mbaya zaidi hata kwa wasio wapendwa yaani kwa watu wa mataifa ! Ila huyu, hakufanya hivyo!

Nisikilize, hakuna mtumishi aliyekamilika, wapo mbinguni, hakuna kanisa lililokamilika, hoja ni pale unapoona madhaifu unafanya nini? Unapaswa kuomba, ukiona doa kwenye koti langu, kachukuwe sabuni na maji uliondowe, sio kulipiga picha na kusambaza doa langu, hujanisaidia, na ukitangaza aibu ya mtumishi ni umeanika aibu ya Yesu, huko ni kulivua nguo kanisa, na kanisa ni Kristo, uwe na uhakika adhabu inakuhusu siku ile ya mwisho ! Jifunze sana kwa huyu mwanamke, nawe uwe ni mueneza habari njema kwa majirani zako, marafiki, usikubali kukaa nao na kujadili yasiyofaa, bali mjadili mema, mkiongea kumi kuhusu VIKOBA, na VIBATI, au mchezo wa fedha,basi wewe weka hapo mawili ya Yesu, anza tu stori kuwa nilipokuwa sijaokoka jamani nilikuwa na sumbuliwa na hili au lile, ila toka nimeokoka, naona nimepokea mujiza, usishangae jirani yako akikwambia, jamani nipelekeni na mimi hapo !

Ama, mchungaji wetu akikuombea, Mungu aliyeko ndani yake atakufungua haraka sana, hapo unafahamu kuna mgonjwa, hata kama hatatoa jibu muda huo uwe na hakika kuwa punde, au baada ya muda, Kuna siku atakutafuta tu, maana ulipanda mbegu, maneno ni mbegu !
(Mithali 6:19 Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.)

Sasa ikupe kujiuliza sana, huwa unapanda mbegu ipi uwapo kanisani, au na wapendwa, kama unamsema vibaya mchungaji, au kanisa, ama mpendwa, uwe na hakika, unapanda pando baya, na apandaye magugu ni mwana wa Ibilisi !

Tuendelee na utendaji wa mwanamke huyu, aliyemtengenezea Yesu mazingira mazuri ya kuifanya kazi yake !

Yohana 4:29 Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?
Na wewe tafuta ulilotendewa na Yesu, lipo, ( Kila aliye na Mwana hakosi ushuhuda, kama huna, tazama vyema kiroho chako kama kweli unaye Mwana !)

30 Basi wakatoka mjini, wakamwendea.
39 Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda.

40 Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili.
:41 Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake.
42 Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.

Yesu alikuwa na kazi nyepesi sana huku, hakukuwa na haja ya kulipia matangazo ya mkutano, au kusambaza vipeperushi, maana kuna mtangazaji, na msemaji wake, alimtangulia, nawe una hiyo dhima, hakikisha unatumia vyema nafasi hii!

Kumbuka hili siku zote, kuwa Mungu asiponufaika na alichoweka ndani yako, basi adui atakitumia, huamini, acha kumsema Yesu, usipojikuta unawasema watu ! Kanisani utakuwa mkosoaji na kuchambua mabaya kana kwamba hakuna jema hata moja, kiongozi wa migomo baridi ni wewe, mbeba maneno utakuwa ni wewe, kwa nini, chai iliyopoa au supu, ndipo nzi hutua ! Kama kinywani mwako Yesu habebwi, Ibilisi atabebwa, utashangaa kila baada ya maneno yako unasema lakini tumuombee, lakini kiukweli huwa hauombi ! 

2. Ni Muombaji; Yohana 2:3 Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai.
4 Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.
:5 Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni.

Sijajua ni kwa nini, ila wanawake wamepewa nafasi ya maombi yao kuwa na wepesi na kibali cha haraka sana, labla kwa kuwa ndani yao uombolezaji ni mwepesi zaidi, ila ninachonuia kukwambia hapa ni kwamba uonapo tatizo au upungugufu kanisani, sio muda wa vikao, na kuchambua, bali ni muda wa kufanya maombi, au dua, ama toba, lishike hili siku zote !

3. Ni Chanzo cha Utatuzi wa Migogoro au Matatizo Sugu maana amepewa Busara na Hekima; Mfano 1, Abigaeli; ( 1 Samweli 25:4-35.)
1 Samweli 25:23 Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi.

24 Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.

25 Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma.

32 Naye Daudi akamwambia Abigaili, Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye amekuleta hivi leo kunilaki;

33 na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe.
Mfano 2, Kisa cha Seba aliyemuasi mfalme Daudi ! 

Baada ya tukio hili, Yoabu alinuia kuleta maangamizi makubwa kwa mji wao wote, na tayari alishaanza kuuvunja ukuta, nasi twafahamu huluka ya Yoabu, katika hiyo sura tu alikuwa ametoka kumuangamiza mtu kwa kukita upanga tumboni mwake, Abineli aliuawa naye, japo alikuwa ameshatengeneza, pia Absolum aliuawa, japo mfalme aliachilia rai ya kumtaka aishi ! Kwa hiyo, sio ajabu kuwa mji huo,ungedhuriwa !

Ila kwa hekima ya huyu mwanamke atwajaye kama mwenye akili, huku biblia nyingine za kingereza na zile za kiswahili rahisi kutumia neno mwenye busara,aliweza kuuokoa mji huo, sasa kanisa likiwa na mama mchungaji makini, na mumewe kujua kumtumia vyema, kwa kumsikiliza na kumpa nafasi, uwe na uhakika atafanikiwa kupindua maamuzi ambayo yangeweza kuleta madhara kwa kanisa, kama Abigaili na huyu waliweza, ni fika hata wewe wa weza !

Kuna ina fulani ya hekima, na busara, na uwezo wa ushawishi waliopewa wanawake, sasa adui akiuwahi, hapo huzalisha wakina Delila,ila Kristo kiuwahi, huzalisha wakina Abigaili, sijui wewe u wapi, au umempa nafasi adui au Kristo Yesu ! 
Tuuone mfano wetu : 

2 Samweli 20:15 Na hao wakaja wakamhusuru katika Abeli wa Bethmaaka, wakafanya chuguu mbele ya mji, nayo ikasimama kuielekea ngome; na watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakavunja-vunja ukuta, wapate kuubomoa.

:16 Ndipo akalia mwanamke mmoja mwenye akili toka mjini, Sikieni, sikieni; mwambieni na Yoabu, aje hapa karibu, niseme naye.
:17 Basi akamkaribia; na yule mwanamke akasema, Ndiwe Yoabu? Akajibu, Ndimi. Ndipo akamwambia Sikia maneno ya mjakazi wako. Akajibu, Mimi nasikia.

18 Kisha akanena, akisema, Watu hunena zamani za kale, wakisema, Wasikose kuuliza huko Abeli; ndivyo walivyomaliza shauri.
:19 Mimi ni wa hao wenye amani, walio waaminifu katika Israeli; wewe unatafuta kuuharibu mji, na mama wa Israeli; mbona wataka kuumeza urithi wa Bwana?

:20 Yoabu akajibu, akasema, Isiwe, isiwe kwangu, niumeze wala kuuharibu.
21 Neno hili silo hivyo; lakini mtu mmoja wa milima ya Efraimu, Sheba, mwana wa Bikri, jina lake, ameinua mkono wake juu ya mfalme, naam, Daudi, basi mtoeni yeye tu, nami nitaondoka katika mji huu. Basi yule mwanamke akamwambia Yoabu, Tazama, kichwa chake utatupiwa juu ya ukuta.

:22 Ndipo yule mwanamke akawaendea watu wote katika akili zake. Nao wakamkata kichwa Sheba, mwana wa Bikri, wakamtupia Yoabu huko nje. Ndipo akapiga tarumbeta, nao wakatawanyika kutoka mjini kila mtu hemani kwake. Naye Yoabu akarudi mpaka Yerusalemu kwa mfalme.

Mwanamke ! Mumeo akiwa mkali, akiwa na hasira kama simba, ni hatari wewe ukiwa kama mbuzi, ila ukiwa kama kondoo, utafanikiwa kuituliza, huyu mwanamke kama naye angeinuka na kujibizana, hakika angechochea ghadhabu ya Yoabu, ila alitumia busara, sasa wanawake wengine, nao hupanda juu, hawajui Mithali 15:1 husemaje ? Kuwa jibu la upole hutuliza hasira, ila la kinyume chake huchochea !
Biblia nyingi za kingereza zimetumia neno ulimi laini, au mzuri, kwa hiyo, ukitaka kutenda vyema, dhidi ya mumeo mwenye hulika kama ya Yoabu, hakikisha unakuwa na ulimi laini, maana hata vyuma bila mafuta husagika.

Akikuudhi na wewe ukisema naenda kwetu, usishangae akiwa wa kwanza kukutolea begi nje!

Sio kwamba hakupendi, ila umechochea ghadhabu, ndio maana ukiondoka, baada ya siku mbili tatu, anakufuata, hapo uwe na hakika, hasira imeisha ! Sasa unaweza kuituliza kwa akili, sio kwa kushindana, huyu mwanamke na Abigaili wawe ni somo tosha kwako !

Muone Ambaye anatumiwa na Ibilisi, ni Mvunjaji, ni mbomoaji, nyundo, huweza kujenga ikitumiwa katika dhamira hiyo, ila ikitumiwa vibaya hubomoa pia, kwa hiyo chombo hakina shida, mtumiaji ndie mwenyewe shida: Kwa hiyo kama kuna mwanaume anaoma huu ujumbe, ajuwe sasa kumuombea mwenzie ! Na kama ni mtumishi, ukiwa na wanawake waharibifu, jifunze kuwabadili au kubadili nia zao kupitia maombi na mafundisho !

Mithali 14:1 Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

Ona hapa: 

Mithali 27:15 Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa;

Oanisha na : Mithali 19:13 Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye; Na ugomvi wa mke kama kutona-tona daima.

4. Hutunza Watumishi; 1. Yule Mshunami; 2 Wafalme 4:9 Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu.

10 Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.

Kuna mzigo wa kipekee ambao Mungu ameweka kwa wanawake kuhusu kuwahudumia watumishi, na kanisa lenye wanawake wenye kujitambua kama hawa, moja kwa moja, hutimiza dhima hii vyema sana !

Mfano 2, Mwanamke wa Serepta, 1 Wafalme 17: 10-16. 

Mfano 3, Enzi za Yesu, japo hata kwa Paulo Mtume ama kqnisa la kwanza walikweo wakina Lidia, tumuone Yesu; 

Luka 8:2 na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba,

3 na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.

Yesu alihudumiwa kwa mali zao, wewe jiulize, mtumishi wako unamuhudumia kwa mali zako ! Na Yesu wa leo ni huyo mlawi wako, ama mtumishi wake !

Na kama hujaokoka na unataka kufanya hivyo sasa tafadhli kwa imani kubwa nakuu kabisa fuatisha pamoja nami maneno haya, au sala hii ya toba ili uweze kuokoka, Sema;

BWANA YESU, NIMETAMBUA KUWA MIMI NI MWENYE DHAMBI, NATUBU MBELE ZAKO LEO, NISAMEHE NA NINAKUOMBA UFUTE JINA LANGU KWENYE KITABU CHA HUKUMU, TAFADHALI LIANDDIKE KWENYE KITABU CHA UZIMA, NINAKUKIRII NA KUKUPOKEA MOYONI MWANGU KAMA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YANGU, HAKIKA WEWE NI MUNGU NA ULIFUFUKA KATIKA WAFU, Amen.

Hongera kwa kuokoka na tafuta kanisa la watu waliokoka ukasali hapo, kwa maombi, sadaka kwa njia ya M-Pesa, kupiga simu au Wasats App, ni +25559859287. Tupo Arusha Tanzania.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company