Rais Francois Hollande akiwa na mateka waliachiwa huru baada ya kuwasili jijini Paris
Na
Victor Melkizedeck AbusoRaia wanne wa Ufaransa waliokuwa wametekwa nyara na kundi la Al Qeada lenye makao yake Kaskazini mwa Afrika nchini Niger wamewasili salama jijini Paris na kupokelewa na familia zao pamoja na rais Francois Hollande.
Raia hao walitekwa na kundi hilo mwaka 2010 nchini Niger na habari ya kuachiwa kwao ilitangazwa na rais Hollande ambaye aliahidi kuwapokea katika uwanja wa ndege.
Paris inasema kuwa haikulipa kikombozi kuwakomboa raia wake ambao wote ni wa kiume baada ya kusakwa kwa miaka mitatu bila mafanikio.
Kundi hilo la al Qaeda linaloendeleza oparesheni zake Kaskazini mwa Afrika lilidai kuwa mwaka 2010 liliwateka Wafaransa hao wakati likipanga mashambulizi katika kampuni inayosimamiwa na serikali ya Ufaransa nchini Niger.
Rais Hollande amesema kuwa mateka hao waliachiwa bila ya nguvu zozote za kijeshi kutumiwa na kuongeza kuwa alipewa habari hizo na rais wa Niger Mahamadou Issoufou.
Aidha Hollande ameisifu serikali ya Niger kwa juhudi zake za kuhakikisha kuwa mateka hao wanaachiwa salama bila ya madhara kutoka mikononi mwa magaidi hao.
Ripoti zinasema kuwa raia hao wa Ufaransa waliachiwa baada ya msuluhishi Mkuu wa Niger ambaye wakati mmoja alikuwa mwaasi wa kundi la Tuareg Mohamed Akotey anayeheshimika sana nchini humo kuingilia kati.
Raia hao wa Ufaransa ambao wametajwa kama Thierry Dol, Daniel Larribe, Pierre Legrand na Marc Feret wameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa wamefurahi mno kuwa huru lakini maisha yao chini ya mateka hayakuwa rahisi.
Wakati wa Oparesheni ya kijeshi katika nchi jirani ya Mali, mateka hao wanasema walikuwa wanahofia maisha yao kwa sababu walifikiri wangeuliwa kama njiamojawapo ya kulipiza kisasi.
Hadi kutekwa kwao, raia hao wa Ufaransa walikuwa wameajiriwa na kampuni ya Uranium ya reva nchini Niger.