WAKATI polisi wakiendelea kukalia jalada la Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), anayetuhumiwa kubaka na kutishia kuua binti wa miaka 16, sasa suala hilo limefikishwa katika ubalozi wa Marekani.
Mbali na hatua hiyo, binti huyo pia amelifikisha jambo hilo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Amiri Manento akitaka msaada zaidi.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumatano, binti huyo na dada yake, walisema wameamua kuomba hifadhi katika ubalozi wa Marekani kwa madai ya kuhofia usalama wao kutokana na vitisho wanavyozidi kuvipata kila kukicha.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, binti huyo alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP), hawataki kulifikisha suala lao mahakamani wanakoamini haki yao itapatikana.
Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakisikia kuwa Marekani ni vinara wa utawala bora na demokrasia, hivyo aliamua kwenda ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini wasaidiwe.
“Kapuya inaonekana anatisha au analindwa sana, lakini sisi tutahakikisha haki yetu tunaipata kwa njia zozote,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa serikali imeshindwa kuwapa hifadhi kutokana na vitisho wanavyovipata, na wanahofia kuuawa hali inayowafanya wawe waangalifu zaidi.
Tanzania Daima Jumatano limedokezwa kuwa mabinti hao walikwenda ubalozi wa Uingereza kuomba hifadhi hiyo ambako walielekezwa kuwa wakienda katika ubalozi wa Marekani shida yao itatatuliwa.
Mmoja wa mabinti hao alithibitisha kwenda katika balozi hizo ambako waliamini wangepata hifadhi waliyoihitaji.
“Tulienda ubalozi wa Uingereza tukaambiwa tuende ubalozi wa Marekani ndio tungeweza kupewa hifadhi, lakini tulipoenda tuliambiwa tupeleke barua kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani au kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ndipo tupokelewe,” alisema.
Tanzania Daima Jumatano liliwasiliana na ofisa mmoja wa ubalozi wa Marekani ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, ambaye alikiri suala hilo kulisikia katika viunga vya ofisi zao.
“Huyo binti mmoja alikuja hapa, lakini baada ya kubanwa na walinzi alishindwa kujieleza fresh… wakamwambia Marekani haihusiki na hilo tukio hivyo hawana msaada kwao.
“Si kweli kuwa ubalozi wa Marekani tulimuambia akalete barua hizo anazozisema ili tumpe hifadhi,” alisema.
Alibainisha kuwa suala hilo halikufikishwa kiofisi.
Katika hatua nyingine, mtoto huyo amelalamikia mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuwatelekeza licha ya mwanzoni kuwaahidi kushirikiana nao.
Alisema sasa mashirika hayo yanaonekana kuogopa vitisho vinavyotolewa na Kapuya.
Binti huyo alisema anakusudia kushirikiana na jamaa, ndugu na marafiki kufanya maandamano hadi mlangoni katika ofisi ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Alisema lengo la maandamano hayo ni kutaka kujua kwanini waziri huyo na polisi wanamlinda Kapuya katika tuhuma hii.
Tanzania Daima Jumatano, lilimtafuta Waziri Nchimbi, kuhusu malalamiko hayo, lakini simu yake ilikuwa ikiita muda mrefu pasi majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu.
Manento ashauri
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, Jaji mstaafu Amiri Manento, alikiri kulisikia jambo hilo kwa muda mrefu, lakini hajui kwanini halijafikishwa mahakamani.
Jaji Manento alibainisha kuwa jambo hilo lipo wazi kwakuwa pande hizo mbili zipo, hivyo ni kazi ya polisi na Mwendesha Mashitaka (DPP) kulifikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Aliongeza kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, haiwezi kuchunguza suala hilo kwakuwa binti anayelalamikiwa kufanyiwa vitendo hivyo yupo na mlalamikiwa wake (Profesa Kapuya) yupo, hivyo mamlaka zinazohusika zifanye kazi yake.
Akizungumzia hatua wanazopaswa kuchukua kuhusu suala hilo, Jaji Manento alisema malalamiko hupelekwa kwa tume, kisha inachunguza na kumpa ushauri anayehusika.
“Sisi hatuna mahusiano na ubalozi wala hatuwezi kuandika barua kushauri ubalozi upokee watu, hayo ni mambo ya ndani ya nchi, ambayo mabalozi hawapaswi kuyaingilia.
“Tunachoshauri sasa kwa kuwa suala la kubaka ni suala la jinai, na kama aliyebakwa anaona kuwa Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka hawataki kumshitaki Kapuya, basi watafute waendesha mashitaka binafsi kesi ifunguliwe mahakamani moja kwa moja bila kutegemea uamuzi wa mwendesha mashtaka (DPP) wa kukubali au kukataa suala hilo lifikishwe mahakamani.
“Kwa utaratibu huo, mtuhumiwa atafika mahakamani, na waliomlalamikia watatoa ushahidi, hata kama katika hatua hii mwendesha mashitaka anaweza kuifuta kesi mahakamani kwa ‘nole’ watu watakuwa wameshajua kama serikali inalinda wahalifu au la,” alisema.
Polisi wazungumza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alipoulizwa juu ya hatua waliyofikia katika kupeleka kesi hiyo mahakamani, alisema bado wanaendelea na uchunguzi.
Alipoulizwa ni uchunguzi wa namna gani wanaoufanya na kama wameshapata maelezo ya Profesa Kapuya, Kamanda Wambura alisema miongoni mwa hatua za uchunguzi ni pamoja na kumuhoji mtu anayetuhumiwa.
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago