Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe.
Walisema kushushwa cheo ni adhabu ya kinidhamu na kwamba uamuzi huo
uliochukuliwa na serikali inamaanisha kwamba iliwabaini wana makosa
ndiyo maana ikawashusha vyeo.
Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS), Francis Stolla, alisema
idara ya upelelezi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) na idara ya ukaguzi ya ndani, inatakiwa kutupiwa lawama kwa
kufanya upelelezi dhaifu uliopelekea watuhumiwa kutochukuliwa hatua
zaidi za kisheria.
Stolla alisema ili Watanzania wajiridhishe kwamba hakukuwa na
mpango wa kulindana, iundwe kamati maalum itakayochunguza upya suala
hilo na ikibainika walihusika, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Mwansheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold
Sungusia, alisema kitendo cha kuwashusha vyeo kinamaanisha kuwa mwajiri
wao alibaini kuwa wana kosa.
Alisema kumshusha mtu cheo siyo adhabu inayotambuliwa kisheria na
kwamba tatizo lililopo ni utamaduni uliojengeka wa kuwalinda wahalifu
kwa hofu ya serikali kuumbuka.
“Viongozi waliopewa madaraka waache kulindana, mtu anapofanya kosa
achukuliwe hatu kama wanavyochukuliwa wengine, kuendelea kulindana ni
kuendelea kulea udhaifu ndani ya serikali,” alisema.
Tundu Lissu, alisema suala la ushahidi kuwa hafifu ni jambo
jingine, lakini suala la kupanga njama ya kufanya wizi ni kosa jingine
ambalo watuhumiwa wanatakiwa kufunguliwa mashataka kwa kosa la kula
njama ya kuiba.
“Hata kama hawakushtakiwa kwa wizi kutokana na ushahidi hafifu,
lakini wanaweza kushitakiwa kwa kosa la kula njama, ”alisema Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema).
Nyaronyo Kicheere, alisema bado kuna nafasi ya kuwachukulia hatua
maofisa hao kwa kuwashitaki kwa kosa la kula njama kwa nia ya kutenda
kosa.
Kicheere alisema hata hivyo, haoni ajabu kwa maofisa wa serikali
kutochukuliwa hatua kwa sababu mambo kama hayo yamezoweleka katika
serikali.
“Sishangai watuhumiwa kuachiwa bila kufunguliwa mashtaka na kupewa
adhabu ya kushushwa cheo. Utakumbuka suala la Akaunti ya Malipo ya
Madeni ya Nje (EPA), watu waliiba pesa wakapewa muda wa kurejesha
taratibu,”alisema.
Jumatano ya wiki iliyopita wabunge wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa waliibua tuhuma za maofisa waandamizi wa
Kitengo cha Itifaki cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa waliobainika kutaka kuiba Sh. bilioni 3.5 kutoka Hazina.
Hata hivyo, akijibu suala hilo Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mahadhi
Juma Maalim, aliwaeleza wabunge hao kuwa maofisa waliohusika
wamechukuliwa hatua kwa kushushwa vyeo, wengine kukatwa mishahara na
wengine kupewa onyo.
Alisema maofisa hao walibainika kutaka kuiba fedha hizo, kufuatia
ukaguzi uliofanywa na wakaguzi wa ndani ya wizara hiyo pamoja na
uchunguzi uliofanywa na Takukuru.
Mmoja wa maofisa hao ni aliyekuwa Mkuu wa Itifaki, Balozi Anthony
Itatiro ambaye hatma yake inasubiri mamlaka ya Rais. Hata hivyo, juzi
Rais Jakaya Kikwete alimteua Balozi Mohamed Maharage kushika nafasi
hiyo.
CHANZO:
NIPASHE