hakileo.blogspot.com
Chadema
kimepinga kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba kuhusu hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kikisema mchakato
wa sasa wa Mabaraza ya Katiba, usiwe kikwazo cha mjadala wa muundo wa
Serikali Tatu.
Mkurugenzi
wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema Dar es Salaam jana kuwa
hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 utakaotokana na mchakato wa mabadiliko
ya Katiba unaoendelea, siyo suala la kusubiri.
Akizungumza
na mwandishi wetu juzi kuhusu kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria
Mathias Chikawe kwamba endapo mapendekezo ya Serikali Tatu yatapitishwa,
kuna hatihati ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kufanyika, Jaji Warioba alisema:
“Tuachieni muda… hayo mengine ni hisia tu. Ni kweli tunayajua lakini
acheni tumalize hili kwanza ( la Mabaraza ya Katiba). Hii ndiyo hatua
tuliyopo sasa.”
Lakini jana
Mnyika alisema: “Hatuwezi kusubiri hadi Mabaraza ya Katiba yakamilishe
mchakato kama alivyoeleza Jaji Warioba katika gazeti lenu la Mwananchi
toleo la leo, (jana),” alisema Mnyika kwa simu.
Jaji Warioba
alitaka suala la muundo wa Serikali Tatu utakavyokuwa lisiwe hoja kwa
sasa kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inachokifanya ni kukusanya
maoni kupitia Mabaraza ya Katiba na kisha kuandaa rasimu itakayopelekwa
bungeni kwa ajili ya majadiliano na kwamba mjadala huo utawachanganya
wananchi endapo utaingizwa katika hatua hii ya ukusanyaji maoni.
Lakini
Mnyika alisema: “Mijadala hii haiwezi kusubiri mpaka hatua ya Mabaraza
ya Katiba, inapaswa kuanza wakati huu kupitia mabaraza yanayosimamiwa na
Tume na Mabaraza yanayoendeshwa na makundi ya kijamii. “Pia, masuala
hayo ya mpito pamoja na marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
ni mambo ambayo yanapaswa kutolewa ufafanuzi wa ziada na Serikali zaidi
ya kauli ambayo Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe ameitoa
kupitia gazeti la lenu la leo (jana).”
Alisema
kimsingi bado kunahitajika mjadala wa masuala ya mpito kwa sababu kuna
uwezekano kwamba Katiba Mpya, ya Muungano au ya Zanzibar na ya
Tanganyika, isiwe tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, endapo suala la
Serikali tatu litapita.
Alisema kwa
upande mwingine, rasimu ya Katiba iliyotolewa imeibua mjadala juu ya
mkwamo wa kikatiba (constitutional stalemate), ambao ni muhimu upatiwe
suluhisho akisema chama chake kinapendekeza mchakato wa Katiba Mpya ya
Tanganyika uanze mara moja ili uende sambamba na huu wa Katiba Mpya ya
Muungano. Alisema ilikuwa vyema yote yakajadiliwa katika Bunge la Agosti
27, mwaka huu.
Waziri
Chikawe alikaririwa na gazeti hili juzi akisema: “Uwepo wa Serikali tatu
utafumua mfumo mzima wa utendaji ndani ya Serikali. Hatuwezi tena
kufanya uchaguzi wa Rais na wabunge 2015, hatuwezi kufanya chochote nje
ya Katiba ya Serikali Tatu kwa kuwa kinachofuata ni kuunda Katiba
nyingine inayohusiana na Serikali tatu.
Waziri Chikawe afafanua
Juzi, Waziri
Chikawe alitoa ufafanuzi juu ya utata wa hoja zake kwa kuipongeza Tume
ya Jaji Warioba kwa kazi inayofanya huku akisema anaunga mkono msimamo
wa CCM wa kutaka kuendelea na muundo wa Muungano wa Serikali mbili.
Alisema mchakato wa kuandika Katiba Mpya unapaswa kuangaliwa kwa jicho pana zaidi ya lile la Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Kuna mambo
mawili hapa. Mosi ni msimamo wa chama changu cha Mapinduzi (CCM) kuhusu
Rasimu ya Katiba na pili msimamo wa Serikali ambayo mimi ni Waziri tena
mwenye dhamana ya Katiba,” alisema na kuongeza:
“Msimamo wa
CCM ni Serikali mbili na wanachama wote nikiwamo mimi tunajua hivyo.
Lakini kuna suala la Serikali ambayo ndiyo iliyoamua kuunda Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Kwa kadri ya uelewa wangu, Serikali haijatoa
msimamo na inaunga mkono kazi inayofanywa na Tume.”
Alisema
mambo hayo mawili hayapaswi kuchanganywa na kuwa kila chombo (CCM na
Serikali) kinaweza kutoa kauli au msimamo kadri kinavyoona inafaa.
Licha ya
kusema kwamba jukumu la kisheria la kuandaa Uchaguzi Mkuu ni la Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, alisisitiza kuwa ili ufanyike mwaka 2015 chini ya
muundo wa Serikali Tatu unaopendekezwa na Tume ya Warioba, basi itabidi
yafanyike mabadiliko makubwa ya sheria mbalimbali kazi ambayo haiwezi
kufanywa kwa kukurupuka.
Hata hivyo,
alisema maoni yake hayana maana kuwa Uchaguzi Mkuu hauwezi kufanyika
mwaka 2015, bali yanalenga kuonyesha kazi kubwa iliyopo mbele.
Butiku
Mjumbe wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku amesema baadhi ya viongozi
wakuu serikalini hawataki tume itoe ufafanuzi kuhusu mapendekezo ya
muundo wa Serikali tatu kwa kuwa unagusa vyeo vyao.
Aidha,
amesema hakuna haja ya kuwa na hofu kwani tayari Zanzibar imekwishaanza
kujitegemea ikiwa na bendera yake, wimbo wake wa taifa na sasa inaidai
Serikali yake kamili.
Butiku
alitoa kauli hiyo juzi wakati wa kikao cha Baraza la Katiba la Wilaya ya
Moshi Vijijini, ambacho kilitawaliwa na mvutano mkubwa miongoni mwa
wajumbe kuhusu suala la kuwapo kwa Serikali tatu, huku wajumbe ambao ni
madiwani, viongozi na wafuasi wa CCM wakitaka Serikali mbili.
Alisema kwa
hali ilivyo sasa, tayari Zanzibar ina Serikali yake yenye mihimili yote
ya dola na tume ilichokipendekeza ni kuiondoa Serikali ya Tanzania Bara
kwenye ‘tumbo’ la Muungano.
Butiku
alisema sababu hasa ya Zanzibar kutaka kuwa na nchi yao ni hofu ya
kumezwa na Tanzania Bara katika Muungano wa Serikali mbili na hofu hiyo
bado haijakwisha na inazidi kukua.
Butiku
aliyataja mambo ambayo Zanzibar iliyafanya kwa baraka za marais wa
wakati huo licha ya kwenda kinyume cha Katiba kuwa ni pamoja na kuwa na
bendera yao pamoja na wimbo wa taifa.
Alisema Baba
wa Taifa, hayati Julius Nyerere alifariki akiwa na imani kuwa Serikali
tatu zitavunja Muungano na alifanya hivyo kwa sababu alitaka kuwapo kwa
nchi moja.
Butiku
alisema hata Mwalimu Nyerere katika kitabu chake alichoandika baada ya
Kundi la Wabunge la G55 kutaka Serikali ya Tanganyika, alizungumzia kuwa
na Serikali moja au Shirikisho.