AL SHAABAB NA CHIMBUKO LA UGAIDI ( VIII)




Kwa nini Rais wa Eritrea anaweza kukamatwa na kufikishwa Mahakama Ya Kimataifa Ya Uhalifu?

Ni Rais Isaias Afeworki. Rais huyu wa nchi ndogo sana ya Kiafrika ameonyesha jeuri kubwa dhidi ya Marekani kuhusiana na hoja ya yeye kujihusisha na kuwafadhili Al Shaabab.

Afeworki anawasaidia Al Shaabab kwa kuzingatia nadharia ya adui wa adui yako ni rafiki yako. Kwamba Eritrea ina uhasama wa muda mrefu na jirani zake Ethiopia. Na kwa vile Ethiopia ni adui namba moja wa Al Shaabab, basi, Eritrea chini ya Afeworki imeamua kuwa mshirika namba moja wa Al Shaabab.

Taarifa za jana Jumamosi, zinabainisha, kuwa Marekani, kwa kutumia kikosi chake maalum cha makomandoo wakishirikiana na CIA na FBI wameingia Tripoli na kumkamata kiongozi wa Al qaida katika Libya Anas Al Liby. Kiongozi huyu wa kigaidi amekuwa akitafutwa na anahusishwa na mashambulizi ya kigaidi kwenye balozi za Marekani mwaka 1998.

Wakati huo, Makomandoo wana maji wa Marekani wamefanya shambulizi katika mji wa Berewa ndani ya Somalia kumlenga kiongozi wa kigaidi wa kikundi cha Al shaabab. Hata hivyo, shambulizi hilo halikufanikiwa kwa vile makomandoo hao walishindwa kumpata mtu waliyemlenga.


Matukio haya mawili yaliyotokea kwa karibu kwa wakati mmoja na yakiongozwa na Marekani yanaashiaria uamuzi wa Marekani wa kutumia mbinu zote kuhakikisha wanaingia kwenye ngome za Al qaida na Al Shaabab katika ardhi ya nchi yeyote ile, iwe ni kwa kutoa au bila kutoa taarifa kwa nchi husika.

Hivyo basi, Rais Isaisa Afeworki wa Eritrea, kwa kuendelea kwake kuwafadhili Al qaida, yuko kwenye hatari hata yeye mwenyewe kukamatwa na kufikishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

Kiongozi mwingine, ambaye naye yuko kwenye hatari hiyo ni Omar Al Bashir wa Sudan anayeonyesha kuwa karibu sana na Afeworki na hata kumuunga mkono katika harakati zake. Wote hawa wawili; Afeworki na Al Bashir, wanakabiliwa na tuhuma za kuvunja haki za kibinadamu na hata kuwatesa na kuwaua wapinzani wao wa kisiasa.

Marekani inaamini kuwepo kwa nchi zenye kuwahifadhi na kuwafadhili magaidi
wenye kutishia maslahi ya Marekani. Marekani inaamini, kwa kuwaacha viongozi wa Al shaabab kujiimarisha na kuendelea kupanga mipango yao ndani ya ardhi ya Somalia.

Na katika hili, uamuzi wa Kenya wa kuendelea kubaki Somalia na vikosi vyake utabaki kuungwa mkono na Marekani. Ni kwa vile, uwepo wa vikosi vya Kenya ndani ya Somalia kunasaidia kazi ya vikosi maalum vya makomandoo wa Kimarekani kwenye mbinu mpya ya kupambana na magaidi kwa kuwalenga viongozi wake kwa kutumia vikosi maalum vya makomandoo.

Na kwa Rais Afeworki, yuko hatarini kwa vile, katika orodha ya Pentagon, Eritrea imeshaingizwa kama nchi yenye kufadhili ugaidi. Na ili tuelewe kwanini Marekani inapambana na ugaidi kwa mbinu hii mpya ni vema tukarudi nyuma kukumbuka kile kinachoitwa "The Bush Doctrine" kwa maana ya imani au kanuni za Rais Bush ambazo pia ndio msimamo wa Marekani kama taifa. Itakumbukwa baada ya shambulizi la kigaidi la Septemba 11 ambapo Osama Bin Laden na Al Qaida walihusika moja kwa moja, Rais Bush alitangaza rasmi sera hii ya
Marekani alipolihutubia Baraza la Congress.

Itakumbukwa, kuwa Rais George Bush alipotangaza rasmi vita dhidi ya ugaidi alitamka kuwa Marekani haitatofautisha kati ya magaidi na wale wenye kuwahifadhi magaidi. Kauli hii ilifuatiwa na uvamizi wa kijeshi dhidi
ya Afghanstan.

Kanuni ama imani hii ya Bush imekuja pia kuongezewa na sera ya "Vita ya Kumwahi anayedhaniwa anaweza kuwa adui kabla hajaivamia Marekani" (pre-emptive war against potential aggressors before they are capable of
mounting attacks against the United States).

Ni katika mtazamo na sera za namna hii ndipo Marekani kwa namna moja au nyingine ilifikia uamuzi wa kuivamia Iraq mwaka 2003. Katika hili, Israel kwa namna moja au nyingine na kwa kuitumia Mosad, Shirika lake la masuala ya ujasusi, nayo imekuwa ikufuata nyayo za Marekani. Israel Wamepata kuivamia na wanaishambulia Lebanon kwa kisingizio cha kujihami. Au hata hapa inaweza kusemwa; kumwahi unayemdhani anaweza kuwa adui kabla hajakuvamia. Ni kwa mantiki hiyo hiyo, Kenya kuingia Somalia kijeshi kunaweza kutafsiriwa hivyo. Hivyo basi, Kenya kwa sasa, inaamini, kuwa haina namna nyingine yeyote isipokuwa kubaki Somalia kwa muda wote ambapo Al shaabab wataendelea kuwepo na kubaki kuwa tishio kwa Kenya.

Katika hili la sera za Bush na Marekani katika kukabiliana na maadui, miongoni mwa waliopata kupinga misimamo au sera hizi za kumvamia adui kabla hajakuvamia ni pamoja na Rais wa zamani wa Marekani Abraham Lincoln.

Mwaka 1848, Lincoln aliandika barua kwa mshirika wake wa masuala ya sheria kupinga hatua ya Rais wa Marekani wa wakati huo Bw. Polk kutaka kuivamia Mexico kama hatua ya kumwahi unayemdhania kuwa adui kabla hajakuvamia.
Lincoln anaandika;
"Kumruhusu Rais kuivamia nchi jirani pale tu anapoona ni muhimu ili kuondosha uvamizi. Na unamruhusu kufanya hivyo kila atakapochagua kusema anaona ni muhimu kwa dhumuni hilo, na unamruhusu kuamrisha vita kama jambo la kujifurahisha.... Kama leo atachagua kusema anafikiri ni muhimu kuivamia Canada kuzuia Waingereza kutuvamia, ni kwa jinsi gani mtamzuia asifanye hivyo? Unaweza ukamwambia, "sioni uwezekano wa Waingereza kutuvamia," lakini yeye atakwambia" Nyamaza; mimi naona, kama wewe huoni" (Abraham Lincoln).

Itaendelea...

Maggid.
0754 678 252www.hakileo.blogspot.com
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company