Haya ndiyo malalamiko yaliyoshamiri kila kona hususan kwenye ofisi za umma. Sehemu ya mwananchi kutumia dakika kumi kupata huduma, inamchukua hadi wiki nzima na zaidi akiambiwa njoo kesho hadi anakata tamaa na kuiona serikali nzima haina maana.
Mwishoni mwa wiki Rais Jakaya Kikwete alijionea ukiritimba huo akiwa ziarani mkoni Pwani na hivyo kutumia nafasi hiyo kuwaonya viongozi akiwataka wafanye uamuzi na kuutekeleza haraka.
Kikwete alisema kuwa nchi haiwezi kuendelea kwa mijadala isiyoisha ya vikao vya kulipana posho.
Maendeleo yamechelewa kwa sababu kila mtu anayepewa kazi anataka kwanza kujadili badala ya kuamua na kutekeleza.
Rais Kikwete alishangaa kusikia kampuni mbili zilizoomba ardhi kwa ajili ya kilimo cha kisasa miaka minne iliyopita mpaka leo zinapigwa danadana pasipo kupewa eneo zima kama zilivyoomba.
“Kwa miaka minne sasa tumekuwa tunazungumza jambo hili bila kufikia uamuzi wake. Tumewahi kujadili suala hili pale Ikulu, Dar es Salaam, na kukubaliana. Imetokea nini? Tulikubaliana kutekeleza jambo hilo sasa tunaendelea kujadili nini?”alihoji.
Tunafurahi kwamba Rais kauona mchezo wa wasaidizi wake jinsi unavyowatesa Watanzania na hivyo kushindwa kujifanyia shughuli za kujiletea maendeleo badala yake wanakuwa kiguu na njia kwenye ofisi za umma.
Viongozi wengi wa serikali muda mwingi wako kwenye vikao visivyoisha; wamejifanya miungu watu.
Jumatatu hadi Ijumaa na Januari hadi Desemba wanazunguka. Wanachokijadili wala hakitatui kero za wananchi zaidi wa kuyafanya maisha yao kuwa magumu.
Migogoro ya ardhi ambayo iko kila kona ya nchi hii, ikichunguzwa kwa undani asilimia kubwa imesababishwa na viongozi wa wizara na idara husika kwa kuchelewa kutoa uamuzi.
Viongozi wengi kama alivyosema Rais, wanatumia matatizo ya wananchi kwa ajili ya kujineemesha na posho za vikao, semina, warsha na makongamano wakati jambo husika lilihitaji busara tu kuamuriwa.
Rais Kikwete tayari ameona utendaji huo mbovu unaoiletea sifa mbaya serikali yake, kumbe ni wakati wa kuwapanga upya wasaidizi wake kuanzia mawaziri kushuka chini ili wajitambue kwamba ni watumishi wa wananchi. www.hakileo.blogspot.com
