Rais wa Sudan Al Bashir akashifu maandamano yanayoendelea na kusema yanalengo la kuzorotesha uchumi



Rais wa Sudan Omar Hassan Ahmed Al Bashir akizungumza na wanahabari na kutetea hatua ya kuongezwa kwa bei ya mafuta
Na Nurdin Selemani Ramadhani

Serikali ya Sudan imetetea uamuzi wa kuongeza ruzuku kwenye bidhaa ya mafuta iliyochangia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo ikisema lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha wanaendelea kukusanya kodi kubwa itakayosaidia kuimarika kwa uchumi wa taifa hilo.
Khartoum imesema kodi ya mafuta ni moja ya kitega uchumi muhimu kwa nchi hiyo katika kuhakikisha inakusanya mapato mengi kitu ambacho kimekuwa kikisaidia kuimarika kwa uchumi wa Taifa hilo.

Rais wa Sudan Omar Hassan Ahmed Al Bashir amekiri nyongeza hiyo ya ruzuku haikuwa na nia ya kuwaumiza wananchi wa Taifa hilo kama ambavyo wapinzani wanavyoeneza uzushi na badala yake ni kwa lengo zuri ya kuimarisha uchumi.

Rais Al Bashir ametetea kwa nguvu zake zote nguvu ambazo zimetumika katika kukabiliana na maandamano yaliyopangwa kushinikiza kupunguzwa kwa bei ya mafuta akisema kungekuwa na madhara makubwa iwapo hatua hizo zisingechukuliwa.

Kiongozi huyo alizungumza kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa maandamano hayo na kuyakashifu vikali huku akisema yamepangwa maalum kwa lengo la kulemaza uchumi wa Taifa hilo.

Al Bashir amesisitiza wapinzani wamekuwa wakifanya kila linalowezekana katika kuhakikisha juhudi za serikali za kukuza uchumi zinakumbana na vikwazo ndiyo maana wameitisha maandamano haya.

Kiongozi huyo hakusita kukiri tangu nchi yao ijitenge na Sudan Kusini kumekuwa na kudorora kwa uchumi lakini amesema hawatakuwa tayari kuona watu wachache wanaendeleza mbinu chafu dhidi ya serikali yake.

Rais Al Bashir amesisitiza maandamano ya amani ni haki ya kila mwananchi lakini anashangaa kuona maandamano hayo yanachukuliwa kama sehemu ya kuleta machafuko na kufanya uharibifu ikiwemo kuchoma vituo kwa kuuzia mafuta na magari.

Serikali ya Sudan imesema haitatetereshwa na mipango hiyo ya Wapinzani ya kutaka kulemaza uchumi wa taifa hilo na badala yake wataendelea kufanya kila linalowezekana lkatika kuhakikisha uchumi wao unaimarika.

Maandamano nchini Sudan yameingia juma la pili kutokana na wananchi kukerwa na hatua ya kupanda kwa bei ya mafuta na wapinzani wamejiapiza kuendelea nayo hadi pale Serikali itakaposikiliza kilio chao.www.hakileo.blogspot.com
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company