Utapeli wa kutisha Kinondoni

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imeingia katika kashfa nzito ya kuwaidhinishia fomu za mikopo watu wasio watumishi wake, kwa kutumia risiti za malipo ya mishahara ya baadhi ya wafanyakazi wake, Tanzania Daima imebaini.

Mbali na manispaa, pia baadhi ya wafanyakazi wa moja ya benki jijini Dar es Salaam, Tawi la Magomeni, wanadaiwa kuhusika katika kashfa hiyo kwa kuwasaidia matapeli hao kutekeleza uhalifu huo.
Mpaka sasa jina la Selemani Kizito, Mwalimu wa Shule ya Msingi Pius Msekwa limeshatumika kukopa kiasi cha sh milioni 6.9 katika Benki ya Wananchi wa Dar es Salaam (DCB) bila mwenyewe kuwa na taarifa.

Idara zinazodaiwa kuhusika katika mkakati huo ni Utumishi na ile ya Elimu ya Msingi, ambapo wakuu wa vitengo hivyo kwa nyakati tofauti wamewezesha mbinu hiyo kufanikiwa.

Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa risiti za malipo ya mishahara ya mwalimu Kizito zilianza kupotea tangu Mei hadi Julai mwaka huu, na mchakato wa wahusika kujipatia mkopo kwa kutumia risiti hizo ulianza Juni 27 kwa mtu aliyejitambulisha kama Kizito kutafuta wadhamini wanaofanya kazi katika manispaa hiyo.

Katika harakati hizo za kutafuta wadhamini, wahusika wa hujuma hiyo walidhaminiwa na Godluck Sabuni na Noel Adam, ambao ni watumishi wa manispaa hiyo kwa ajili ya kwenda kukopa katika Benki ya DCB.

Pia Ofisa Elimu Msingi, aliyefahamika kwa jina la F. Kikove na Ofisa Utumishi aliyefahamika kwa jina moja la Alute, kila mmoja kwa wakati wake alisaini fomu namba 29324 za kumtambua mkopaji huyo bandia kuwa ni mfanyakazi wa manispaa hiyo.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili limezipata, ni kazi rahisi kupata risiti za malipo ya wafanyakazi wa Idara ya Elimu katika manispaa hiyo kutokana na mfumo usio na ulinzi wa risiti hizo.

Hali inaonesha kuwa baada ya mishahara ya walimu kulipwa, risiti za malipo ya walimu wote wa manispaa ya Kinondoni hutoka kwa Mkurugenzi kwenda katika ofisi ya Masjala.

Kutoka katika ofisi ya Masjala, risiti hizo hukusanywa sehemu moja na kisha kupelekwa katika Shule ya Msingi Ali Hassan Mwinyi, iliyo katika manispaa hiyo.

Baada ya risiti kufika katika shule hiyo, kila shule iliyo katika Manispaa ya Kinondoni inatakiwa kumtoa mwalimu mmoja kwa ajili ya kwenda kuzifuatilia na kufikisha katika shule yake.

“Tukisema kila mwalimu akafuate risiti yake manispaa, itatulazimisha tuache kufanya kazi kwa siku nzima ili kushughulikia hali hiyo, ndiyo maana tukaona hili suala tulielekeze sehemu moja na wenyewe wapangiane utaratibu wa kuzipata,” kilisema chanzo chetu.

Katika kufanikisha mkopo huo, mkopaji aliyejitambulisha kwa jina la Kizito, alifanikiwa kufungua akaunti namba 20502517596 katika Benki ya NMB, huku akiwa na ATM kadi yenye jina la Seleman Kizito Said, ambalo ni jina la mwalimu aliyeibiwa risiti za malipo ya mishahara kwa muda wa miezi mitatu.

Wakati kadi hiyo ya ATM ikionesha jina la Saidi, namba ya siri ya benki inaonesha kadi hiyo inamilikiwa na mtu mwenye jina la Joseph Mathew Said, hata hivyo akaunti hiyo inafanana kwa kiasi kikubwa na akaunti ya Kizito (mwalimu) iliyo katika Benki ya NMB, hali iliyotaka kumletea matatizo wakati akifuatilia namna fedha zake zilivyokuwa zikikatwa.

“Kama hawa wafanyakazi hawahusiki na huu mchezo, unadhani huyu angeweza vipi kufanikiwa, kwa kuwa na ATM card yake ina jina la mwalimu mwenzetu kama siyo ile namba ya kompyuta, mbona angeambiwa ni yeye aliyekopa?” alisema mwalimu mmoja wa Shule ya Pius Msekwa.

Wadhamini

Wafanyakazi walioweka dhamana katika fomu ya kuomba mkopo huo walipozungumza na gazeti hili kila mmoja alikiri kuhusika na kumdhamini mkopaji kwa maelezo kuwa walimtambua kama mfanyakazi mwenzao katika manispaa hiyo.

Godluck Sabuni, alisema kutokana na kumuona mhusika kila wakati katika manispaa yao hakuweza kumfikiria kama ni mtu anayeweza kufanya udanganyifu huo.

“Mimi sasa nipo likizo ila hilo suala ninalijua lakini kwanini tuongee kwenye simu, si unisubiri baada ya siku mbili nitakuwa hapo kazini,” alisema Sabuni.

Kuhusu kumfahamu Kizito, Sabuni alisema mtu huyo alimuomba amdhamini kwa ajili ya kuhamisha akaunti yake kutoka Benki ya NMB kwenda DCB kwa madai ya kuepuka foleni katika Benki ya NMB.

Mfanyakazi mwingine, Noel Adam, anayedaiwa kuwa dereva wa Manispaa ya Kinondoni, alikataa kuzungumza katika simu huku akibainisha kuwa kwa sasa si mfanyakazi wa manispaa hiyo tena.

“Nimeshaacha kazi lakini kama utaweza kunitafuta baada ya siku mbili, tatu tunaweza kuongea kwa kina na ukajua kila kitu juu ya hali ilivyokuwa,” alisema Adam.

Kwa upande wao, Kikove na Alute, ambao ni maofisa wa manispaa hiyo walipoulizwa juu ya kadhia hiyo walitaka kujua sehemu taarifa zilikopatikana, huku Kikove akitaka habari hizi zisiandikwe kwa kuwa zitaharibu mipango iliyopo.

“Mimi sikusaini lakini habari zingine zikitoka zinaathiri hali iliyopo, katika hatua hii itamgharimu mwalimu aliyekupa hizi taarifa,” alisema Kikove.

Alute alikataa kuzumgumzia hali hiyo na kutaka atafutwe Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kwa kile alichoeleza kuwa ndiye anapaswa kuongea kuhusu masuala ya Kinondoni.






Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company