Polisi yawapiga ‘stop’ tena Ukawa huko Zanzibar

Na Ibrahim Yamola na Peter Saramba, Mwananchi
Dar/Arusha. Jeshi la Polisi Zanzibar limeendelea kuuchelewesha mkutano wa wanachama wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa madai kwamba hakuna askari wa kutosha kuulinda.


Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema mkutano huo utafanyika leo katika uwanja huo. PICHA|MAKTABA

Awali, mkutano huo ulipangwa kufanyika Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Kibandamaiti, Unguja lakini jeshi hilo liliuzuia kwa madai ya kuwapo kwa habari za kiintelijensia dhidi ya tishio la maisha ya watu.

Awali, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema mkutano huo utafanyika leo katika uwanja huo.

Ukawa ni muungano wa vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, DP na wajumbe 25 kutoka kundi la wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.

Hata hivyo, Msemaji wa Polisi Zanzibar, Mohamed Mhina alisema baadaye kuwa mkutano huo hautafanyika hadi Aprili 30, mwaka huu.

Alisema umezuiwa kwa sababu askari na maofisa wa polisi wanaotakiwa kuusimamia wako Dar es Salaam katika maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Tumekutana nao (CUF walioomba kibali kwa niaba ya Ukawa) na kukubaliana kwamba mkutano huo ufanyike Aprili 30 kwani askari waliopo hivi sasa ni wachache hawawezi kutosha kusimamia ulinzi kutokana na aina ya mkutano wenyewe. Hata hiyo siku hiyo hakutakuwapo na maandamano, bali wataruhusiwa kufanya mkutano pekee na siyo vinginevyo.”
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company