Watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya mlemavu wa ngozi, Zawadi Magimbu (32) wakiwa ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita baada ya kuhukumiwa kunyongwa. Kutoka kushoto ni Nasoro Charles, Singu Siantemi, Masaru Kahindi na Ndahanya Lumola. Picha na Jackline Masinde.
Watu wanne wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na kosa la kumuua Zawadi Magindu (32) mwenye ulemavu wa ngozi, mkazi wa Kijiji cha Nyamaruru, Wilaya ya Geita mkoani hapa.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Joacquine De-Mello wa Mahakama Kuu, ambaye alisema alisema Mahakama imeridhika pasi na shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kwamba walihusika moja kwa moja na kifo hicho.
Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Nassoro Charles mkazi wa Kijiji cha Beda mkoani Kagera, Masaru Kahindi mkazi wa Kijiji cha Nyamaruru, Ndahanya Lumola na Singu Nsiantemi wakazi wa Kijiji cha Kakoyoyo, Wilaya ya Bukombe.
Jaji De-Mello alisema washtakiwa walifanya kosa hilo Machi 11, 2008 saa 1:00 usiku nyumbani kwa akina Zawadi wakati wakipata chakula cha usiku, walimkata kwa shoka na panga miguu yote na mkono wa kulia.(P.T)
Alisema Masaru Kahindi aliyekuwa jirani na Zawadi, Nassoro Charles aliyekuwa mume wa marehemu walivamia nyumbani kwao wakati wanapata chakula cha usiku, huku wakiwa na panga na shoka kisha kumkata miguu na mkono wa kulia .
"Watu hao walikwenda na shoka na panga, walitumia shoka kumkata Zawadi huku mama yake Magdalena Mashimba na mjukuu wake, Semen Hamisi wakipigwa na kutupwa nje na wauaji hao," alisema Jaji De-Mello.
Aliendelea kusema kuwa, wakati wanamkata Zawadi, mtoto wake Semeni alijibanza mlangoni na kuwatambua wauaji hao kuwa mmojawapo alikuwa mume wa mama yake na mwingine jirani yao.
"Walionwa na shahidi Magdalena na Semeni waliwatambua kwa sauti na mwonekano, kwani wakati wanafanya hivyo kulikuwa na mwanga wa mbalamwezi," alisema.
Pia, Jaji De-Mello alisema washtakiwa Ndahanya na Nsiantemi walikuwa wafanyabiashara wa viungo vya albino, walikamatwa na polisi baada ya kutegewa mtego.
"Polisi walikuwa kwenye operesheni ya kuwatafuta watu wanaojihusisha na vitendo vya kuua albino, walipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna watu wanataka viungo vya albino ndipo walipotafuta albino wawili, mmoja akiwa mtoto na mwingine mtu mzima," alisema.
Alisema baada ya kutegwa mtego huo walikamatwa washtakiwa wawili; Ndahanya na Nsiantemi ambao walikiri kuhusika na mauaji ya Zawadi na kuchukua viungo hivyo, kisha kuvipeleka kwa mganga wa jadi, Mussa Ally mkazi wa Katoro ambaye alihusika kuvipima ili kujua iwapo vina ubora.
"Wakati watu hawa wanahojiwa na polisi waliwataja wenzao wengi ambao hapa mahakamani hawapo sijui ni kwa nini... wakiongozwa na Robert Kagoma ambaye ndiye alikuwa wakala wa kulangua viungo hivyo na kuvipeleka kwa mganga wa jadi aliyetajwa kwa jina la Gerald Mazuri ambaye pia huviuza kwa 'wazungu' Geita," alisema Jaji De-Mello.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago