Na Sharon Sauwa
KWA UFUPI
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu yake, Balozi Mahiga alisema nchi imekuwa katika hatari ya kupoteza umoja jambo ambalo linahitaji kutazamwa upya na kuimarishwa ili iendelee kuwa na amani.
Dodoma. Makada wa CCM, wameendelea kupigana vikumbo katika ofisi za makao makuu ya chama hicho mjini hapa kwa ajili ya kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea urais. Jana ilikuwa zamu ya Balozi Augustine Mahiga na Monica Mbega aliyejitosa kimya kimya.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu yake, Balozi Mahiga alisema nchi imekuwa katika hatari ya kupoteza umoja jambo ambalo linahitaji kutazamwa upya na kuimarishwa ili iendelee kuwa na amani.
“Hakuna muungano wa nchi mbili uliowahi kudumu kama wetu. Nimesafiri kwenda nchi mbalimbali duniani na kuulizwa siri ya muungano huu kudumu hadi leo,” alisema.
Alisema akifanikiwa kuingia Ikulu, ataendeleza tunu hiyo ya Taifa.
Balozi Mahiga alisema kuwa Taifa limeanza kulegalega kutokana na rushwa na ufisadi. “Tusiposhughulika na matatizo haya, Taifa linaweza kuyumba na kupoteza mwelekeo,” alisema.
Alisema tatizo hilo linaweza kumalizwa kwa viongozi kushirikiana na wananchi.
Kwa mujibu wa Balozi Mahiga, ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), imeonyesha kuwapo na upotevu wa mabilioni ya fedha kila mwaka.
Hata hivyo, alisema CAG na Bunge wamekuwa wakipiga kelele, lakini wanaofanya matendo hayo bado wanadunda.
Alipoulizwa atawezaje kuiongoza Tanzania wakati yeye alikuwa nje ya nchi kwa muda mrefu alijibu: “Kama balozi unashindwa kuelezea kilichotokea nchini kwako hufai kuwa balozi…Uongozi wa kimataifa niliupata, sasa naurudisha nyumbani ili kuiunganisha Tanzania na mataifa mengine,” alisema.
Mbega: Nitaendeleza yaliyofanywa na JK
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Monica alisema kuwa endapo atafanikiwa katika kinyang’anyiro hicho, atatekeleza Ilani ya chama na kuendeleza mambo yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya nne.
‘Nitaangalia changamoto gani ambazo hazikuweza kuleta maendeleo na kuzishughulikia,” alisema. Mbega alisema atafanya hivyo kwa kutumia wataalamu wa ndani ya nchi. Nitatumia watalaamu wa kila aina katika kuiendeleza Tanzania, alisema.Mbega alisema Serikali ya awamu ya nne imejitahidi kupambana na tatizo la rushwa na yeye akiingia madarakani, ataangalia chanzo cha tatizo hilo na kuongeza nguvu katika hilo.
Mbega alisema hivi sasa tayari vimejitokeza viasharia vya uhasama, mauaji ya albino, wizi, ubaguzi wa dini na ukabila. Alisema ili kuendelea na amani ni lazima kurejesha vitu vinavyojenga amani.
Kwa nini alikosa ubunge?
Alisema siyo kweli wananchi walimkataa, ila utaratibu wa kumpata mgombea ubunge ndani ya CCM, ndiyo ulikua tatizo.