John Magufuli rais mteule wa Tanzania
REUTERS/Sadi Said
Na Victor Melkizedeck Abuso
Tume ya uchaguzi nchini Tanzania imemtangaza mgombea wa Chama Cha Mapinduzi CCM, John Pombe Magufuli kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais mwaka 2015.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva ametangaza kuwa Magufuli alipata ushindi kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58 huku mpinzani wake wa karibu Edward Lowasa akipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39 nukta 97.
Magufuli mwenye umri wa miaka 56 anatarajiwa kukabidhiwa cheti cha ushindi siku ya Ijumaa jijini Dar es salaam na kuapishwa rasmi baadaye mwezi huu.
Tume ya uchaguzi imesema imetangaza matokeo kama ilivyoyapokea na kusema kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na haki.
Hata hivyo, Edward Lowasa amesema hatambui ushindi wa John Pombe Magufuli.
Muda mfupi kabla ya John Pombe Magufuli kutangazwa mshindi, Edward Lowasa alijitokeza katika Ofisi ya muungano wa UKAWA jijini Dar es salaam na kutangaza kuwa yeye ndiye mshindi wa uchaguzi huu.
“Nimejiridhisha kuwa mimi ndiye mshindi wa uchaguzi huu baada ya kupata kura Milioni 10 nukta 6 sawa na asilimia 62 na hivyo naitaka Tume ya Uchaguzi kunitangaza mimi Edward Ngoyai Lowasa kama mshindi,” alisisitiza Lowasa.
Akiwa pamoja na viongozi wengine wa upinzani wa vyama vya NCCR Mageuzi, CUF, NLD na chama chake cha CHADEMA, Lowasa amesema ataendelea kupigania haki yake.
Viongozi wa UKAWA walikuwa wanaendelea kukutana kujadili mustakabali wao baada ya John Pombe Magufuli kutangazwa mshindi wa uchaguzi huu.
TAIFA STARS HAZARANI
-
Kaimu kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Etiene Ndairagije ametangaza
kikosi cha timu ya taifa chenye wachezaji 30 ambao wanajiaandaa na mchezo
wa kuwania ...
5 years ago