|
KULWA Mirobho (39), maarufu kwa jina la Jogoo la Mara, mkazi wa
Kijiji cha Nambaza wilayani Bunda amekufa baada ya kulewa pombe na dawa
za kulevya kisha kujimwagia mafuta aina ya petroli mwili mzima na
kujilipua moto.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nambaza, Alfred Taganga alisema tukio hilo
lilitokea kijijini kwake Machi 5, mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni.
Alisema kuwa mwanaume huyo baada ya kutumia dawa za kulevya aina ya
bangi na pombe aina ya gongo, alichukua mafuta ya petroli yaliyokuwa
yanauzwa kwenye kituo kijijini hapo na kujimwagia mwili mzima na kisha
kuwasha kibiriti na kujilipua kwa moto.
Ilielezwa kuwa baada ya kujilipua kwa moto alianguka chini na ndipo
wananchi wakammwagia mchanga ili wauzime moto huo. Baada ya kufanikiwa
kuuzima walimpeleka hospitali.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Misheni Kibara, Dk. Cosmas Fabian alisema
mwanaume huyo alifariki dunia kesho yake majira ya saa 12:00 asubuhi,
kutokana na kupata majeraha makubwa yaliyosababishwa na moto huo.
|