|
“KAKA poleni sana kwa tukio la Absalom Kibanda. Daima msiwaogope
wawezao kuua mwili ila yule awezaye kuuwa mwili na roho pia. Sina
ushahidi ndugu yangu ila naamini kabisa hivyo ni vitisho vinavyotolewa
na magenge ya watu wenye nia mbaya na nchi yetu tukufu.
“Naomba niwatie moyo waandishi wa habari endeleeni kupambana kwa
kutumia kalamu yenu, waacheni wao waendelee kutumia bisibisi, mapanga,
marungu na risasi za moto ila mwisho wa siku mkweli atabaki salama.
“Watamuua Kibanda atabaki Edson, watamuua Edson atakuja mwingine,
daima hawataisha wote. Si siri tukio alilofanyiwa Kibanda
limenisikitisha sana, limenisononesha sana, limenihuzunisha sana na
mwisho wa siku moyo wangu umejaa ghadhabu, hasira na chuki kubwa sana.”
Haya ni maneno ya faraja kutoka kwa rafiki yangu wa mkoani Tanga, siku
moja baada ya mwenzetu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006)
Ltd ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Rai, Mtanzania, Dimba na
Bingwa, Absalom Kibanda kuvamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake
eneo la Mbezi Beach nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kisha kupigwa na
kujeruhiwa vibaya.
Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
alipigwa na kitu kizito chenye ncha kali kichwani, kutobolewa jicho la
kushoto, kunyofolewa ukucha na kukatwa kidole cha mkono na kung’olewa
meno mawili.
Hakika ni tukio la kuhuzunisha, kutisha na zaidi ni unyama unaotendwa
na binadamu wenzetu ili kuendelea kukidhi ajenda zao binafsi. Niseme
kuwa Mungu ni wetu sote na hivyo iko siku makatili hawa wataumbuliwa.
Hili ni tukio la kutia hofu na kuacha mashaka mengi kwani linakuja
ikiwa ni miezi takriban tisa tangu kutekwa, kuteswa, kuumizwa vibaya,
kung’olewa meno na kucha na kutelekezwa msituni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, usiku wa Juni 26, mwaka jana.
Tangu kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka katika mazingira
yanayofanana na tukio la Kibanda, Jeshi la Polisi nchini limekuwa
likitupiana mpira katika kueleza hatua zilizofikiwa kuwasaka
waliohusika.
Licha ya mtuhumiwa pekee raia wa Kenya, Joshua Mulundi kufikishwa
mahakamani akidaiwa kuhusika na tukio hilo, bado polisi imeshindwa
kumhoji Dk. Ulimboka wala watuhumiwa aliowataja kwa majina kuwa
walihusika kumteka na kumtesa.
Kibanda kwa sasa amehamishiwa katika Hospitali ya Milpark nchini
Afrika Kusini kujaribu kuokoa maisha yake, madaktari wamemfanyia vipimo
mbalimbali vikiwamo CT Scan na X-ray hasa kichwani na sehemu nyingine za
mwili ambazo zilipata majeraha.
Tumeelezwa kuwa imebainika kwamba mfupa laini (fizi) uliopo kati ya
pua na mdomo ni kama umekatika. Hii inatokana na nguvu na nyenzo
walizotumia watesaji kumng’oa meno. Kutokana na hali hiyo ana maumivu
makali sana kwenye kinywa chake.
Pia imebainika kwamba meno kama sita hivi katika kinywa chake
yamelegea. Kwamba haya ni tofauti na yale mawili yaliyong’olewa katika
tukio la awali.
Narudia tena kusema kuwa ni unyama na mkakati wa binadamu wenzetu
wasiothamini uzalendo na uhai wa wengine. Hawa wako tayari kufanya
lolote ili mradi mambo yao yanyooke. Wataendelea kututesa kama
walivyofanya kwa Kibanda lakini watambue huo si mwisho wa mapambano.
Tunahuzunika, tunalaani tukio la Kibanda lakini shaka haituishi kwani
hatuoni juhudi za kukomesha vitendo vya mateso na mauaji kwa waandishi
wa habari.
Mara kwa mara tunasikia salamu za pole na rambirambi zikipitishwa
kwetu kwenda kwa watu mbalimbali waliopata matatizo lakini kwa mwandishi
mwenzetu marehemu Daudi Mwangosi hizo salamu hazikuwepo na sasa Kibanda
naye hali ni hiyo hiyo. Magwiji wa kufariji kila tukio wamekaa kimya
kama hawapo.
Simaanishi kwamba tunahitaji pole zao wakati tunakufa na kuteswa
wakifurahia, isipokuwa nataka umma wa Watanzania tunaoutumikia utambue
kuwa wanahabari wa Tanzania tunafanya kazi hatarini, kifo na mateso yetu
ni wakati wowote. Hatujui nani atafuata baada ya Kibanda.
Kama Kibanda alifanyiwa unyama huo langoni kwake ni dhahiri kuwa
watatuwinda hata barabarani, wakiamua watatufuata ofisini kama
walivyowafanyia Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage wa gazeti la
MwanaHalisi.
Kibanda ameteswa wakati akikabiliwa na kesi ya uchochezi katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Anashitakiwa na Jamhuri akidaiwa
kuchapisha makala katika gazeti hili la Tanzania Daima wakati akiwa
Mhariri Mtendaji wake.
“Baada ya kuona hali hiyo nilitaka kujiokoa kwa kukimbia lakini
nilianguka, hivyo wakaanza kunishambulia kwa kunipiga nondo kichwani na
sehemu mbalimbali za mwili, wakanikata kidole kwa kuing’oa kucha na
kunitoboa jicho la kushoto,” haya ni maneo ya Kibanda akiwa hospitalini
Muhimbili.
Katika masikitiko haya, nafurahi kuwa umma wa wananchi uko nyuma yetu,
unatupa matumaini ili tusife moyo kwa vitisho na vitendo viovu
tunavyofanyiwa. Swali na kujiuliza ni nani wanafanya unyama huu,
wanaatumwa na nani, kwa sababu gani na wanalipwa nini?
Haya ni baadhi ya wasomaji wa gazeti letu, walioguswa na tukio la
kuteswa kwa Kibanda. Kwa kuwa sikuwajulisha kama nitayachapisha,
nitaomba nisiwataje majina yao wala namba zao za simu.
“Ukweli kuhusu kuteswa na kuumizwa kwa jamaa yetu Kibanda kamwe
hauwezi kupatikana kupitia kamati za vyombo vya kiserikali ikiwemo
polisi ambayo mara zote imekuwa mtuhumiwa wa kwanza. Mwangalieni sana au
mchunguzeni huyo wanayemwita …(anamtaja kigogo mmoja).
“Hiyo ni desturi yake hata katika chaguzi za kata huku zimewaacha watu
wengi vilema, kazi yake ni kufadhili ‘janjaweed’ katika miaka yote
anayoshinda, ameumiza sana watu.” 0757******
“Kama kweli polisi wanasema wanahitaji ushirikiano wenu, basi ni
muda muafaka wa kumwambia IGP Said Mwema kuwa kwa vile mbinu za mateso
ni zile zile kama zilizotumiwa kwa Dk. Stephen Ulimboka basi watu
waliotajwa na Ulimboka wawe wa kwanza kukamatwa na kuwekwa ndani wakiwa
wanangojea ushahidi wa Kibanda kutoka hospitali, vinginevyo,
kinachofanyika ni usanii.” 0756******
“Kwanza natoa pole kwa timu nzima ya wanahabari kwa matukio
yanayowakabili ambayo yanatishia usalama wenu katika utekelezaji wa
majukumu yenu, pili niwaombe muwe na ushirikiano katika kipindi hiki
kigumu ili huyu adui anayewaandama apatikane.
“Serikali inawajua ilisajili laini za simu ili kubaini matumizi mabaya
ya simu, hawa wanaowatishia wamiliki wa namba hizo wanatoka Ulaya?
Nimeguswa sana na mateso aliyoyapata Kibanda.” 0718******
“Pole sana kwa yaliyomkuta Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri,
Kibanda. Mimi kama mwananchi ambaye nimekuwa nikifuatilia makala zake
kwa kweli inaniuma na hasa kuona vitendo kama hivi vinazidi kushamili
kwa waandishi wa habari na hatua hazichukuliwi. Tunawaombea uzima bila
shaka atapona.” 0713******
“Poleni jamani, naona hii kazi sasa inakuwa na maadui wengi, kuwa makini kaka yangu.” 0713******
Hii ndiyo Tanzania waliyotuachia wazee wetu Nyerere, Mwinyi na
Mkapa? Tunakwenda wapi kama tumeruhusu kutekana, kuumizana na hata
kuuana? Tafakari!
|