BARAZANI KWA AHMED RAJAB
ALHAMISI iliyopita Rais Jakaya Kikwete alikutana na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame mjini Kampala, Uganda. wapiga picha walipokuwa wakisukumana kupata nafasi nzuri ya kuwapiga picha, marais hao hawakuvimbiana mashavu.
Badala yake walifanya uungwana wa kupeana mikono. Yaliyokuwa nyoyoni mwao hatuyajui. Wala hatujui nini na nini kikiwaenda akilini mwao.
Wawili hao walikuwako Kampala kuhudhuria Mkutano wa Saba wa Kimataifa Kuhusu Eneo la Maziwa Makuu uliojadili hali ya usalama mashariki mwa Congo-Kinshasa.
Walichukua fursa hiyo kujaribu kuyatanzua matatizo yao. Hivyo, walijitenga kwa muda wa saa nzima wakila chakula cha mchana wao peke yao na kuyazungumza ya baina yao.
Huo ulikuwa mwanzo mwema. Bahati mbaya si wengi wetu wenye kujua nini hasa wakuu hao wawili walichokizungumza huku visu na nyuma zikizoa kilichokua kwenye sahani zao. Wala hatujui walikubaliana nini.
Siri ya mazungumzo yao wamebaki nayo wao wenyewe Kikwete na Kagame watu ambao wametoka mbali na wenye kujuana kwa muda mrefu. Kabla ya kukaa kula walikuwa wamekwishapimana na, kwa vile wote walianzia jeshini, kila mmoja wao alikuwa tayari anazijua nguvu na udhaifu wa mwenzake.
Kwa muda wa miezi mitatu hadi waliposalimiana Alhamisi iliyopita Kagame alikuwa akitoa matamshi ya hanjamu ya kumtishia Kikwete. Inavyoonyesha ni kwamba Kikwete, ingawa naye alijaribu kujikakamua na kumjibu Kagame, alitikisika kiasi cha kumfanya amuombe kaka yao Yoweri Museveni, Rais wa Uganda, aingilie kati kuwapatanisha.
Hatua nyingine alioichukua Kikwete ni kuwatimua maelfu ya wachungaji wa mifugo wenye asili ya Rwanda kutoka eneo la Kagera. Serikali ya Tanzania ilisema walikuwako nchini kinyume cha sheria.
Kuna mengi tulioweza kuyang’amua kutokana na mkasa huo wa JK na PK. Kwa mfano, ombi la Kikwete kwa Museveni tunaweza kulifasiri kama kukubali kwa Kikwete kwamba Museveni ndiye kubwa lao katika Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye jumla ya wakaazi wasiopungua watu milioni 135.
Hakuona kwamba Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya, au Pierre Nkurunzinza, Rais wa Burundi, wanafaa wawe wasuluhishi kati yake na Kagame.
Hilo si la ajabu kwani, kwa kadri nimjuavyo, kwa kawaida Kikwete ni mtu mwenye adabu zake, mwenye kuwaheshimu waliomzidi kwa umri.
Bila ya shaka, katika siasa hasa siasa za uongozi wa urais kuwanyenyekea wakubwa kwa sababu wao ni wakubwa wa umri tu kunaweza kuzusha matatizo. Hata hivyo, nadhani kwa hili la kumstahi Museveni, Kikwete hakukosea japokuwa kuna wataosema kwamba Museveni na Kagame ni ‘dugu’ moja na kwamba Museveni atampendelea tu Kagame.
Lakini, kwa kweli, tukiwaangalia viongozi wa sasa wa kanda hii ya Afrika Mashariki Museveni ndiye anayechomoza kuwa aliyebobea kuwashinda wenzake, licha ya taksiri zake za utawala bora.
Hivyo, endapo Shirikisho la Afrika Mashariki litaundwa kesho basi kiongozi wa mwanzo, Rais wa mwanzo, wa Shirikisho hilo huenda akawa Museveni, japokuwa anaweza akawa Rais wa mpito.
Hilo likitokea halitokuwa fanikio dogo kwa Museveni tukizingatia kwamba Kikwete analiongoza taifa kubwa kabisa kwa eneo na kwa idadi ya watu miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
Museveni anampiku pia Uhuru Kenyatta ijapokuwa Kenya ndilo taifa lenye uchumi uliomkubwa na uliomadhubuti kushinda chumi nyingine katika Jumuiya hiyo.
Jengine tuliloling’amua ni kwamba viongozi wakianza kutishana, kujibizana na kusutana hata ikiwa wanaropoka tu wanakuwa wanahatarisha amani na usalama baina ya nchi zao. Na hivyo ndivyo hali ilivyokuwa kwa muda wa miezi mitatu tangu Kikwete alipohisi anatoa ushauri wa maana wa kumshauri Kagame azungumze na kundi la waasi wa Démocratiques pour la Libération du Rwanda (FDLR).
Kagame, kwa upande wake, alihisi kwamba Kikwete alikuwa akimchokoza na kumfanyia stihizai na kejeli.
Mzozo huo lakini haukuwa kitisho kwa amani na usalama wa Rwanda na Tanzania tu bali ulikuwa pia kitisho kwa usalama wa eneo zima la Maziwa Makuu.
Tuling’amua pia kwamba kuna walioingia wasiwasi kwamba mkwaruzano huo wa Rwanda na Tanzania unaweza kuwa na athari ya kuiua Jumuiya ya Afrika Mashariki, ingawa siamini kwamba Jumuiya hiyo itakufa kama ilivyokufa ile ya awali. Hiyo ilikuwa na wanachama watatu tu — Kenya, Tanzania na Uganda —na ilikufa 1977.
Kuna sababu kadha wa kadha zilizosababisha kifo cha Jumuiya hiyo ya awali ya Afrika Mashariki. Miongoni mwazo ni mifumo ya kiuchumi iliyokinzana kati ya ule wa kibepari wa Kenya na wa Tanzania uliokuwa wa kijamaa.
Kadhalika kulikuwako na suitafahamu na dikteta wa Uganda Idi Amin na ukaidi wa Kenya wa kutaka iwe na uwakilishi mwingi zaidi na ule wa Tanzania na wa Uganda katika vyombo vya uamuzi vya Jumuiya hiyo.
Mfano wa mwisho nitaoutoa wa tuliyoyang’amua kutokana na mzozo huo wa Kagame na Kikwete ni jinsi raia wa Rwanda na Tanzania (pamoja na wale wa Kenya na wa Uganda) walivyoukimbilia uzalendo wao, wakauvaa na halafu wakajitosa nao katika bahari iliyochafuka ya huo mzozo ulioanzishwa na marais wa Tanzania na Rwanda.
Yaliyoandikwa na raia wa nchi hizo katika mablogu mbalimbali na katika majukwaa ya mawasilino ya kijamii yanaonyesha wazi jinsi raia hao wa kawaida walivyotupilia mbali mantiki na hoja. Badala yake wamekuwa na jazba kuwatetea marais wao au kuwakabehi wa wenzao.
Hiyo si ishara njema kwa mustakbali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wa umoja wa watu wa nchi zetu. Na si viongozi wala si raia waliopendekeza namna ya kuung’oa ule mzizi wa fitna baina ya Kikwete na Kagame.
Ninachokusudia ni kwamba lile suala lililozusha uhasama baina yao, la waasi wa FDLR, halikuchambuliwa kwa kina ipasavyo na kupatiwa suluhisho. Na suluhisho si kuwatenga na kuwafanya waselelee mashariki wa Congo.
Sululisho litapatikana tu pale viongozi wa eneo hilo watapokuwa na moyo wa kulipigia mbizi suala hilo kuangalia kwa nini waasi hao wanaendelea na uasi wao na nani mwenye kuwasaidia kwa hali na mali
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/kikwete-na-kagame-wapumua-kidogo#sthash.0xZgpL6C.dpuf