NI HOJA,CCM IUNGANE NA VYAMA VYA UPINZANI;

HABARI ZETU
ccmmiaka31pemba4_964e7.jpg
Tangu kuanza kwa mchakato wa kupata katiba mpya, mengi yamekuwa yakizungumzwa, mazuri na mabaya pia. Matukio makubwa yanayokumbukwa ni kupitishwa kwa sheria ya kuanza mchakato wa katiba, marekebisho ya sheria hiyo yaliyoletwa bungeni baadaye baada ya sheria kupitishwa na bunge, na kasha kugomewa na wabunge wa CHADEMA, na safari hii sheria ya uundwaji bunge la katiba.
Kwa nadharia ya haraka ilitegemewa mchakato huu ungefanywa kwa busara na hekima na kuwa ungetuunganisha Watanzania wote kwani ni mwongozo wa Taifa letu sote tukiwa kama raia wa kawaida, wanachama na wapambe wa vyama vya siasa, viongozi, wazee, vijana, wenye dini na wasio na dini, bara na visiwani.(P.T)

Ni wakati ambao Watanzania walistahili kuongozwa na tafakari ya maisha ya sasa na ya vizazi vingi vijavyo. Tungekuwa ni wenye hekima, kila taasisi kama bunge, serikali, mahakama; wananchi katika makundi mbalimbali kama vile dini, NGOs, wakulima, wafanyabiashara, vyama vya siasa, vyama vya kitaaluma, n.k.; kila kundi lingejiuliza tunataka Tanzania yetu iweje sasa, miaka ya karibuni ijayo na mingi ijayo. Matakwa na matamanio yetu ya Tanzania ya sasa, siku za karibuni zijazo na miaka mingi ijayo, vingetusaidia sana kupata mwongozo sahihi wa kuifikia Tanzania tuitakayo, ni mwongozo huo ni katiba.WWW.HAKILEO.BLOGSPOT.COM
Sijui kama Rais Kikwete aliporidhia matakwa ya Watanzania ya kutaka kupata katiba mpya alitaka tupate katiba mpya ya namna gani. Lakini sidhani kama alimaanisha katiba yenye mwelekeo huu tunaoenda nao. Kuna ule msemo usemao gabbage in gabbage out. Ukiingiza takataka lazima utapata takataka, hapa nikimaanisha kuwa mchakato wetu wa kutengeneza katiba mpya kwa maana ya mchakato wenyewe, sheria zinazosimamia, watu wanaosimamia na wanaowakilisha, hivyo vyote vikiwa ovyo na katiba yetu ni lazima iwe ovyo.
Kosa kubwa linalofanyika sasa ni pale ambapo wanasiasa wanaona katiba ni yao. Viongozi na wabunge wa CCM wanaona katiba ni lazima ikidhi matakwa yao ya kuendelea kutawala, huku vyama vya upinzani navyo vinaona kuwa katiba itasaidia kuiondoa CCM madarakani. Mawazo haya yanavuruga kabisa dhamira ya kupata katiba iliyo bora. Hatutaki tuandae katiba inayokusudia kumweka mtu au chama madarakani milele wala yenye nia ya kukiondoa chama fulani madarakani. Tukiandaa katiba yenye kuhakikisha chama tawala kinabaki madarakani milele au yenye kuhakikisha chama tawala kinaondolewa madarakani, baada ya hilo kukamilika, tutaenda vipi mbele ya safari?
Nimesoma kwenye magazeti kuwa viongozi wakuu wa chama cha CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi, walikutana Dar es Salaam na kufanya mkutano wa pamoja kuhusiana na mchakato wa katiba, na kauli kuu waliyotoka nayo ni kuwa watahamasisha watu wakatae mchakato wa katiba kuhodhiwa na CCM. Lakini mimi nasema waende kwa wananchi na ujumbe kuwa mchakato wa katiba usihodhiwe na kikundi chochote, chama chochote cha siasa wala kiongozi yeyote bali uhodhiwe na wenye nchi ambao ni watanzania wote kwa ujumla wetu. Kauli ya namna hiyo inastahili kuungwa mkono na vyama vyote vya siasa, asasi zote za kiraia, taasisi zote za dini na watanzania wote. Tukiwa wote na mtazamo huo, wala kusingekuwa na haja ya maoni ya CCM au CHADEMA bali tungekuwa na maoni ya vyama vya siasa. Tume ya Warioba ingeviataka vyama vya siasa kwa ujumla wao, watoe maoni ya pamoja juu ya nini kiwekwe ndani ya katiba ili vyama vyote viweze kuendesha siasa kwa usawa, haki na amani.
Tungeyataka madhehebu ya dini pia yatuambie wanataka haki gani zilindwe na katiba ili waweze kuwapeleka waumini ahera au mbinguni bila bugdha; wasomi wa taaluma mbalimbali wanataka katiba izingatie nini ili usomi wao uwe na tija kwa Taifa wao wenyewe binafsi na familia zao; hata waganga wa jadi nao watuambie nini wanataka kizingatiwe kwenye katiba ili tiba zao ziwe na manufaa kwa watanzania badala ya kuchochea mauaji ya walemavu wa ngozi, wanaume wenye vipara au uchunaji wa ngozi za binadamu; halikadhalika iwe hivyo kwa wakulima, wafanyabiashara, walemavu, wanaofanya kazi nje ya nchi, n.k. Maana hawa wote wanataka haki zao zianishwe kwenye katiba. Lakini pia tuna yale mambo ya msingi ya jumla ambayo ni kikwazo kwa kila kundi yasipodhibitiwa. Hayo yangeweza kujadiliwa na makundi yote. Tunataka katiba yetu iwe na misingi imara itakayoondoa na kuzuia rushwa, upendeleo, ubadhirifu, manyanyaso, biashara haramu, n.k.
Mchakato wetu wa kupata katiba mpya umekosa dira baada ya kuufanya kuwa ni mashindano badala ya kuufanya kuwa ni mchakato wa maridhiano ya kitaifa. Tumeufanya mchakato wa katiba kuwa ni mashindano kati ya wananchi wa Zanzibar ambao wengi hawapendi muundo wa Mwungano wa sasa na watawala wa serikali na viongozi wa CCM wanaotaka mfumo wa sasa uendelee; na kwa upande mwingine ni mashindano kati ya CCM na vyama vya upinzani ambavyo vinataka ushiriki zaidi wa wananchi wakati CCM ikitaka uwe ni mchakato wa wateule wachache.
NINI CHA KUFANYA
  • Kwa kuwa CCM ndiyo inayoshutumiwa kuhodhi mchakato, itoe tamko la wazi na kwa vitendo la kutokuwa na tamaa wala kusudio la kuhodhi mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya. CCM iungane na vyama vingine vya siasa kuhamasisha watu kupinga njama zozote za kikundi au chama chochote kuhodhi mchakato wa katiba.
  • Tume ya katiba ielekeze vyama vya siasa kupeleka maoni yao kama taasisi moja ya kisiasa kuliko kuchukua maoni ya kila chama. Uchukuaji wa maoni ya chama kimoja kimoja kumeongeza ushindani usiokuwa na tija. Vyama vya siasa vikishindwa kuridhiana juu ya maoni ya pamoja, tume itumie maoni ya wananchi kuhusu vyama vya siasa ndani ya katiba.
  • Rais Kikwete atamke wazi kuwa katiba iliyo bora itapatikana kwa ushiriki mkubwa wa wananchi wote, siyo viongozi wa vyama au bunge. Katiba ya Watanzania kuanzia mchakato wa kuipata mpaka upatikanaji wake uakisi ushiriki mkubwa wa Watanzania wote. Pia atamke wazi kuwa hana nia yoyote ile kwa namna yoyote ile kushinikiza matakwa yake binafsi au ya chama chake kuwa ndiyo mwongozo wa katiba mpya. Jukumu la serikali yake litakuwa ni kujenga mazingira ya ushiriki mpana wa kila Mtanzania katika kupata katiba mpya.
  • Kutolewe muda tena kwaajili ya kujadili suala la mwungano bila uzuizi wa namna yoyote ile. Inaonekana watu wanahitaji mjadala mkubwa zaidi na huenda itakuwa busara CCM na serikali iwaache Wazanzibari na viongozi wa Zanzibar wajadili kwa uwazi wanataka mwungano wa namna gani na watoe uthibitisho ni namna gani mwungano huo utakuwa bora kuliko tulio nao. Watanganyika nao wana haki ya kuujadili mwungano. Suala la mwungano na muundo wake inaonekana lina uzito wa pekee kwa Watanzania wengi, na tusipokuwa makini tunaweza kujikuta katika rasimu yote ya katiba tunajadili mwungano tu na wakati kuna mengi mengi yanayogusa maisha yetu ya kila siku hatujua hata kama yapo au yanahitaji michango yetu.
  • Kwa kuwa kuna tuhuma zilizothibitishwa na jaji Warioba za CCM kuingilia mchakato wa upatikanaji wa wajumbe wa mabaraza ya katiba, kuna umuhimu mkubwa zaidi wa kuongeza wabunge wa bunge la katiba maana uwakilishi wa mabaraza ya katiba unatiliwa mashaka. Kimsingi mapendekezo ya mabaraza ya katiba yapewe uzito mdogo kutokana na uwakilishi uliokuwa na walakini.
  • CCM itamke wazi kuwa haitawatisha wala kuwafukuza uongozi au wanachama wake kwa vile tu mawazo yao kuhusu mambo gani yawepo kwenye katiba yametofautiana na mawazo ya viongozi wa chama au ilani ya chama. Katiba hii tunayoiandaa ni kwaajili ya Taifa letu wala siyo manifesto ya uchaguzi. Kumfukuza au kumtisha mtu yeyote kwa sababu ya mawazo yake ni kutokumtendea haki.
KWA RAIS KIKWETE
napenda kumwambia kuwa, sisi kwenye makampuni tunasema, 'failure of the company is failure of the management'. Katiba tunayoiandaa sasa ikiwa mbaya au ikaleta mfarakano mkubwa ni 'failure' yako Rais maana ndiye uliyeridhia, kuanzisha na kusimamia upatikanaji wake. Na pia nakukumbusha kuwa 'a good leader is that who can define a goal and mobilize others to rally behind'. Rais kwenye hilo inaonekana hujafanikiwa kikamilifu, hujaweza kuwafanya wanachama wa chama chako kukuunga mkono kikamilifu, wakakufuata nyuma, kukuunga mkono na kukupa nguvu ya kupata katiba nzuri. Wanayoyafanya kwa macho ya juu yanaonekana kama ni wana heshima na imani kubwa kwako lakini kwa undani kuna uharibifu mkubwa kwa chama na serikali yako. Hakuna jambo baya watu wakaamini kuwa kwenye mchakato huu kuna hila, ikiaminika hivyo, mchakato wote utakuwa mgumu. Wewe ni sehemu ya bunge, lakini kiuhalisia mamlaka yako pekee yako yanazidi ya bunge, mchakato huu ukiharibika mzigo utakuwa wa kwako, na wale ambao hawakupenda uamuzi wako wa kuridhia kuundwa kwa katiba mpya watakuwa wameshinda, wewe na wananchi mtakuwa mmeshindwa.
Rais barabara unazojenga zitachakaa miaka si mingi ijayo, halikadhalika vyuo, mashule, mahospitali, n.k. lakini katiba ikitengenezwa vizuri inaweza kudumu hata miaka mia ijayo. Kwaajili ya umuhimu na jukumu kubwa kama kuna umuhimu wa pekee kuwa na watu wenye dhamira na mtazamo wa kitaifa katika kulismamia hilo. Mimi siamini kama Mwanasheria wako Mkuu na Waziri wako wa sheria wana mtazamo na dhamira hiyo. Mtazamo wetu wananchi wa kawaida ni kuwa au Mwanasheria hapendi tuwe na katiba nzuri au Rais pia ana nia iliyofichika! Kama si hivyo kwa nini Mwanasheria Mkuu kila wakati anapeleka bungeni miswada yenye utata kuhusiana na katiba na bado Rais anamwona anafaa?
Na Bart Mkinga
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company