OPERESHENI KIMBUNGA


KIKWETE

Rais Kikwete: Wahamiaji haramu lazima waondoke
Na Mwandishi Maalumu, Washington
RAIS Jakaya Kikwete ameiambia Kamati ya Bunge la Marekani kuwa lazima wahamiaji haramu waondoke na kwamba Tanzania haijafukuza mkimbizi hata mmoja na wanaondolewa ni wahamiaji walioingia na kuishi nchini bila kufuata taratibu na sheria.
Alisema kuwa kamwe Tanzania ambayo imekuwa kimbilio kubwa la wakimbizi katika historia haiwezi kuwafukuza nchini wakimbizi kwa kuwa haina sababu ya kufanya hivyo, na hata kama sababu ingekuwepo, ingefanya hivyo kwa kufuata taratibu za kimataifa.
www.hakileo.blogspot.com
Msimamo huo wa Tanzania umeelezwa kwa mara nyingine tena, Septemba 18, mwaka huu wakati alipokutana katika mkutano wa kikazi na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Uhusiano wa Nje na Bajeti ya Miradi ya Maendeleo, Kay Granger na baadhi ya wajumbe wa kamati yake.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Bunge la Marekani, mjini Washington D.C., Rais Kikwete alisema umekuwepo upotoshaji kuhusu amri ya Serikali ya kuwaondoa nchini wahamiaji haramu ambao wanaishi nchini kinyume cha sheria.
Akijibu swali ambalo aliulizwa na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Rais Kikwete alisema: “Tuna wakimbizi 264,000 kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambao wote wako katika makambi yao mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ambaye amefukuzwa.
“Hata kama tungetaka waondoke nchini tunajua taratibu za kuwaondoa wakimbizi kwa sababu Tanzania ina uzoefu wa miaka mingi wa kuwapokea, kuwatunza na kuwajali wakimbizi.

“Tungewasiliana kwanza na Umoja wa Mataifa na nchi ambazo walitokea wakimbizi hao kabla ya kuwashauri kurudi makwao. Wote wako makambini na hivyo suala la kuwafukuza nchini halipo.
“Watu ambao tunawaondoa sisi ni wahamiaji haramu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita. Wengine wamekuwa nchini kwa muda. Kuna wakati waliambiwa kuweka vizuri ukaaji wao nchini kisheria lakini hawakufanya hivyo.
“Hawa hatuna jingine la kuwafanyia, ni lazima waondoke. Tuliwapa wiki mbili za kuondoka wenyewe, tuongeza tena muda wa wiki mbili. Kiasi cha wahamiaji haramu 34,000 waliondoka wenyewe, sasa waliobakia tunasaka katika operesheni maalumu,” alisema Rais Kikwete.
Alisema kuwa baada ya kumalizika kwa muda huo, sasa Serikali imeanzisha operesheni maalumu ya kuwaondoa wale ambao hawakuondoka nchini wenyewe.
“Na operesheni hii itaendelea hadi tutakapomaliza tatizo hili la wahamiaji haramu ambao wanashutumiwa kwa vitendo vya ujambazi, utekaji nyara mabasi, uvamizi wa misitu ya asili na hifadhi kwa malisho na kuingiza maelfu kwa maelfu ya mifugo katika maeneno tengefu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita,” alisisitiza.
Baada ya mkutano huo, Rais Kikwete alishiriki chakula cha mchana ambacho kiliandaliwa kwa ajili yake na Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Bunge la Marekani ya International Conservation Caucus Foundation (ICCF) katika ukumbi wa chakula wa wabunge ndani ya Bunge hilo.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi nchini Marekani amewasili mjini Washington D.C akitokea mjini San Francisco ambako alikuwa na ziara ya siku mbili katika Jimbo la California.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company