HABARI ZETU
KATIKA mambo ya kusikitisha ninayoyaona na kuyadurusu ni jinsi tulivyokubali kujidhalilisha mbele ya wenzetu. Kwa mfano, tumekubali kwamba sisi tutakuwa watu dhaifu katika nyanja fulani fulani tukilinganishwa na wenzetu waliotuzunguka, na hatukosi visingizio vya kuhalalisha udhaifu huo.www.hakileo.blogspot.com
Mojawapo ya ishara za udhaifu huo ni ule unyonge tuliojivisha kwa kuendelea kuamini kwamba hatuwezi kushindana na majirani zetu (hasa Wakenya na Waganda) katika soko la ajira. Ni kama vile tumekwisha kukubali kwamba hatuwawezi wenzetu na hatuna la kufanya juu ya hilo.
Siku zote nimejiuliza ni nini kimetufanya kama taifa kufikia hatua hii ya kukata tamaa, kiasi kwamba hata wenzetu nao wamefikia hatua ya kututambia wazi wazi kwa kutuambia kwamba wanajua kwamba sisi ni dhaifu mno na hatuwezi kushindana nao.
Tunapopata matokeo ya mitihani kama haya tunayoyajadili leo ndivyo tunavyozidi kunyong’onyea na kujihurumia, si kuchukua hatua madhubuti, kujihurumia na kuzidi kujiona wanyonge, dhalili. Na wenzetu nao wanapata sababu nyingine ya kuzidi kutuzomea kimya kimya.
Majuzi nilikutana na kijana wa Kenya tukiwa tunahudhuria mkutano mjini Mombasa. Huyu ni kijana anayeijua kidogo nchi yetu, amewahi kufanya kazi mara kadhaa hapa na anajuana na vijana wenzake wengi wa Kitanzania. Fikra zake ni kwamba labda kinachofanywa na watawala wetu ni kuwadumaza wananchi katika ujinga kwa kuwa watoto wa watawala hawasomi shule za wananchi, lengo likiwa ni kuwatawala kirahisi walio wengi wenye elimu duni.
Alinipa mfano wa ndugu yake wa kike anayefanya kazi Unguja na ambaye amelazimika kumrudisha mwanawe wa miaka mitano akaishi na dada yake Kenya kwa kuwa hakuwa na shule ya kumsomesha Unguja wala Dar es Salaam. Maelezo yake ni kwamba shule binafsi hazikamatiki kwa gharama na shule za umma hamna kitu kinachofundishwa.
Sote tunajua kwamba wazazi wa nchi hii wenye uwezo kidogo (uwezo halali na uwezo haramu pia) wanawasomesha watoto wao katika shule binafsi nchini ama ughaibuni, wengi wakiwa wanawapeleka Kenya au Uganda. Siku hizi ni kawaida kuwasikia vijana wakijitapa kwa shule walizosoma Kenya na Uganda na kuwakoga wenzao waliosoma nchini Tanzania.
Mara nyingi nawasikia wanaosema eti tatizo letu ni Kiingereza, kwa sababu lugha hiyo inatupiga chenga, imetushinda na hatuiwezi. Sasa tumeifanya lugha hii kama jambo jingine ambalo sisi hatuna uwezo nalo. Ni katika muendelezo ule ule wa kurefusha orodha ya mambo tusiyoyaweza (pamoja na kilimo, viwanda, soka, riadha, uadilifu….) Tunapenda mno kutokuweza.
Kiingereza tungeweza kusema, “We are compulsive underperformers” ikiwa na maana kwamba tunao utashi mkubwa mno wa kutenda chini ya viwango.
Lakini najiuliza, kama ni Kiingereza, lugha ya wakoloni ndicho kinatupa taabu, mbona hata Kiswahili kinatushinda? Mbona ni Wakenya ndio wanapata nafasi za kufundisha Kiswahili duniani, kama nilivyotabiri katika safu hii hii miaka ya 90? Kwamba, sipati faraja yoyote katika usahihi wa utabiri wa aina hii; ni usahihi unaoumiza.
Nikiangalia televisheni zetu, nikisikiliza redio zetu, hasa hizo zinazoitwa FM, halafu nikaangalia televisheni za Kenya na nikasikiliza redio zao (katika vipindi vya Kiswahili) nagundua kwamba tatizo letu si Kiingereza bali ni kukosa umakini katika jinsi tunavyofanya mambo yetu. Wakenya wanaotumia Kiswahili wanakitumia vyema zaidi kuliko wenzao wa nchini mwetu.
Najiuliza, hivi hawa vijana wa Kitanzania kwenye hizi redio za FM wanajihisi kwamba ni wajuzi sana kwa kutumia mseto wa lugha mbili ambazo zote hawazijui? “Nilikuwa nahang out na friend mmoja aliyekuja nibetray vibaya mno. Siwezi kumforgive forever yaani!” Ujinga!
Kwa hiyo tatizo letu si Kiingereza. Binafsi mimi ni mmoja wa wale wasioamini kwamba kuzungumza au kuandika Kiingereza vizuri ndiyo elimu. Elimu ni zaidi ya lugha hata kama ujuzi wa lugha bila shaka unasaidia. Yapo mambo mengi mno tunaweza kuyafanya kwa lugha ya Kiswahili, au Kisukuma, au Kinyakyusa, au Kingoni, Kichagga, Kiluguru na kadhalika, na tukayafanikisha kwa kiwango kikubwa. Kilimo ni eneo mojawapo.
Lakini, tuache hilo. Kama bado tunaamini kwamba Kiingereza ni lazima, basi ni kwa nini hatuchukui hatua za kujifunza lugha hiyo na kuifundisha kwa watoto wetu ili waweze kuimiliki vyema? Ni yale yale ya kutokujua ni nini tunataka. Kiingereza kinatushinda, Kiswahili kinatushinda. Hatutaki kujifunza hiki wala kile. Tunabakia kulalamika kwamba Wakenya watatuzidi kete katika kila tunalotaka kufanya.
Tunawapa raha sana Wakenya, nao hawatuachii kwa kututambia kila wapatapo fursa ya kututambia. Fursa hizo tunawapa kila siku, nao wanazitumia kwa sababu hawana ujinga tulio nao, wa kubadhiri kila fursa tuliyo nayo.
Fursa nyingine tumewatupia wakati wa uchaguzi wa wabunge wa kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA). Tunasema eti Wakenya, Waganda, Wanyarwanda na Warundi wanataka kutuzidi nguvu; wanainyemelea ardhi yetu, nasi hatutaki kuwapa ardhi yetu.
Hili tunalisema na kulirudia kila siku, kama aya ya msahafu, mpaka inachosha, na wala hatuzungumzii Makaburu na wageni wengine kutoka nchi za mbali wanaochukua ardhi yetu kila siku. Kisha tunaambiwa tuchague wajumbe wa kutuwakilisha Afrika Mashariki, ambao ndio watatufanyia kazi ya kuchunga ardhi yetu isikwapuliwe na majirani zetu.
Wanakuja watu wasio na sifa, wengine mbumbumbu kama miye; hawana hata chembe ya uwezo, hata wa kujieleza wakaeleweka. Wanahonga, wanasambaza fedha. Wabunge wa Bunge la Taifa wanajipanga, wanajikusanya, wanamwendea mgombea na kumwambia, “Sisi tuko kumi. Ukitupa kila mmoja laki tano utapata kura zetu sote kumi.” Hivyo ndivyo baadhi yao walivyochaguliwa. Sasa wako Arusha wanachunga ardhi yetu isiporwe na Wakenya.
Nielezeni ni ujuha gani mkubwa kuliko huo!- See more at: http://www.raiamwema.co.tz
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago