HABARI ZETULICHA ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kukiri kuwa Balozi wa China nchini, Lu Youqing, alivunja mkataba wa Vienna wa kidiplomasia na kuahidi kumchukulia hatua, sakata hilo hadi sasa linapigwa danadana.
Septemba 12 mwaka huu, balozi huyo alihudhuria mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika Uwanja wa Shycom mkoani Shinyanga na baadaye katika eneo la Mnada wa Mhunze Jimbo la Kishapu, jambo ambalo ni kinyume na mkataba huo.Kutuatia tukio hilo, serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje chini ya Waziri Bernard Membe, ilitoa onyo kwa CCM na kuahidi kuchukua hatua za kidiplomasia, huku Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi naye akikemea kitendo hicho.

Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa, kwani hata wizara husika imekuwa na kigugumizi kulizungumzia tena sakata hilo.

Mwandishi wa gazeti hili, alifika wizarani wiki hii kupata ufafanuzi wa hatua zilizochukuliwa kwa balozi huyo, lakini wasaidizi wa Waziri Membe walisema kuwa alikuwa amealikwa kwenye kituo kimoja cha redio, na hivyo hakuna mtu wa kutoa ufafanuzi.

Hata ofisa mwandamizi wa wizara hiyo, Mkumbwa Ally alipotafutwa kwa simu na kutakiwa kutoa ufafanuzi, aliomba apewe muda kidogo kwa ahadi kwamba angepiga simu.

Alipotafutwa tena, hakuwa na majibu yenye ufafanuzi wa hatua gani serikali kupitia wizara hiyo ilichukua kwa balozi huyo waliyekiri kuwa alikiuka mkataba wa Vienna kwa kitendo chake cha kujihusisha na siasa za taifa jingine.

“Serikali imeshachukua hatua za kidiplomasia, sio lazima wananchi wazijue, ila ujue tu tumeshachukua hatua,” alijibu Mkumbwa na kisha kukata simu.

Sakata la balozi huyo liliibuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kwa Waziri kivuli wake wa Mambo ya Nje, Ezekiel Wenje.

Na katika kujibu madai hayo ya CHADEMA, wizara ilisema kuwa kitendo cha balozi yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa siyo sahihi na kinakiuka kifungu cha 41(1) cha mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia, na kwamba itamchukulia hatua.

Balozi Youquing alitambulishwa kwa wananchi na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na kisha kuwahutubia akisema China imevutiwa na sera za CCM na hivyo itawekeza katika soko la pamba katika mkoa huo.

Katika mikutano hiyo, balozi huyo alicheza nyimbo za CCM za kubeza vyama vya upinzani huku akiwa amevalia kofia ya chama hicho.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company