Mwenyekiti wa Kamati ya Miundo Mbinu ya Bunge, Peter Serukamba
Tumechapisha leo habari kuhusu kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa juzi mkoani Njombe kwamba ni aibu kwa Serikali kudaiwa na wakulima. Kauli hiyo ilifuatia Ripoti ya Maendeleo ya Wilaya ya Ludewa, ambapo aliambiwa kwamba wakulima wa wilaya hiyo pekee wanaidai Serikali Sh3.115 bilioni kutokana na tani 6,231 za mahindi ambazo Serikali ilikopa msimu wa kilimo uliopita.
Rais alikiri awali katika mkutano wa hadhara wa wakazi hao kwamba ni kweli Serikali yake inadaiwa Sh17 bilioni ikiwa ni deni la wakulima wa mahindi katika mikoa mbalimbali nchini, ambao waliuza mahindi yao kwa Serikali kupitia kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), msimu uliopita. Rais aliwaahidi wakulima wilayani humo kwamba Serikali italipa fedha hizo haraka iwezekanavyo.
Hayo ndiyo mazingira tunayoweza kuyaita ya aibu ambayo Rais Kikwete alijikuta juzi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku saba mkoani Njombe. Tunasema hivyo kutokana na Serikali kukusanya kodi, huku ikikopa mahindi ya wakulima wanaoogelea katika madimbwi ya umaskini wa kutupa na kushindwa kuwalipa fedha zao. Hakuna lugha sahihi na stahiki ya kuelezea hali hiyo, isipokuwa kusema kwamba Serikali imewadhulumu wakulima wa mahindi, kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa wakulima wa mazao mbalimbali hapa nchini, wakiwamo wakulima wa korosho.
Wakati Rais Kikwete akitoa kauli hiyo juzi, Kamati ya Bunge ya Miundombinu ilikuwa ikikutana jijini Dar es Salaam na uongozi wa Kampuni ya Simu nchini (TTCL), ambayo iko taabani kifedha kutokana na Serikali na taasisi zake kushindwa kulipa deni la Sh10 bilioni inazodaiwa na kampuni hiyo. TTCL ilizitaja baadhi ya taasisi zinazodaiwa kuwa ni: Ofisi ya Rais (Sh180 milioni); Tamisemi (Sh775.9 milioni); Jeshi la Polisi (Sh1.28 bilioni); na JWTZ (Sh2.1 bilioni).
Tunapata wakati mgumu kuelewa kwa nini Serikali imeendekeza utamaduni na hulka ya kutolipa madeni, hasa madeni ya ndani. Kwa mfano, imetumia ubabe kupora ardhi ya wananchi kwa kisingizio cha uwekezaji. Mfano hai ni maeneo mengi nchini yaliyochukuliwa kwa nguvu na bila fidia kupitia mamlaka ya uwekezaji ya EPZA. Baadhi ya wananchi walilipwa fidia baada ya kufanya maandamano na vurugu, lakini walio wengi bado wanasotea malipo na Serikali inawaongezea uchungu kwa kuwapa ahadi hewa miaka nenda miaka rudi.
Inawezekana Rais Kikwete hajui jinsi Serikali yake ilivyolemewa na mzigo wa madeni kwa kudaiwa kila kona ya nchi. Inawezekana pia kwamba washauri wake hawamwambii kwamba Serikali yake ndiye mdaiwa sugu pekee nchini asiyelipa madeni, pamoja na fedha kutengwa katika bajeti za kila mwaka kulipia gharama za uendeshaji wa Serikali. Nani asiyejua kwamba Serikali hiyo ndiyo mdaiwa sugu katika Mamlaka za Maji, Tanesco, Kampuni ya Simu (TCCL) na makampuni mengi ya umma na watu binafsi? Tunaambiwa kwamba watoa huduma na bidhaa katika taasisi za Serikali kama majeshi, shule, vyuo na hospitali hulipwa fedha zao baada ya mateso ya muda mrefu.
Tungependa kuihadharisha Serikali kwamba kutolipa madeni yake ya nje au ndani ni kujipotezea sifa na uhalali wa kuitwa Serikali. Serikali yoyote duniani isiyolipa madeni yake, tena kwa wakati hujijengea taswira hasi ya kutoaminika na kutoheshimika. Serikali ya Rais Kikwete sasa ijipime na kuchukua hatua.