Mapigano yaibuka upya Kongo

Mapiganao yameibuka upya kati ya wanajeshi wa serikali na waasi kaskazini-mashariki mwa Kongo, zimesema pande mbili na Umoja wa Mataifa, siku chache baada ya kushindwa kwa ya mazungumzo ya amani mjini Kampala.


Waasi wa kundi la M23.
Msemaji wa waasi wa M23 Vianney kazarama alisema mapigano hayo ambayo yaliwalaazimu maelfu ya raia kuyakimbia makaazi yao, yalitokea umbali wa kilomita 25 kaskazini mwa Goma, mji muhimu wa wakaazi milioni moja uliyopo katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini la mashariki, lakini linalokabiliwa na machafuko ya mara kwa mara.

Rwanda yatishia kujibu mapigo
Nchi jirani ya Rwanda iliwashtumu wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa kurusha makombora matatu ndani ya mipaka yake na kutishia kujibu iwapo mashambulizi yataendelea. Kazarama alisemam jeshi lilishambulia ngome za waasi mapema siku ya Ijumaa, lakini jeshi hilo lilisitiza kuwa lilishambuliwa kwanza -- madai yanayoungwa mkono na duru kutoka ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO.

Taarifa ya MONUSCO, ambayo ilishiriki mapigano hayo sambamba na jeshi la Kongo, ilisema ghasia ziliendelea kwa siku nzima. MONUSCO ilisema ilikuwa na wasiwasi mkubw ajuu ya kuanza tena kwa uadui, na kuwatolea wito waasi wa M23 kurudi kwenye meza ya mazungumzo. "Niko makini katika juhudi zetu za kuwalinda raia na kuyatangua makundi yote yenye silaha ili kurejesha amani na utulivu," alisema mkuu wa MONUSCO martin Kobler.
Mkuu wa MONUSCO, Martin Kobler.

Mwanaharakati wa haki za binaadamu katika eneo hilo aliziona helikopta za Umoja wa Mataifa zikiruka juu ya kijiji cha Kibumba, ambacho ni ngome ya M23 iliyoshambuliwa, na alisema kuwa raia walikuwa wanakimbia kuelekea mpaka wa Rwanda.

Baraza ya usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Machi liliidhinisha kupelekwa kwa kikosi maalumu cha Afrika chenye wanajeshi 3,000 chini ya MONUSCO, ambacho kinaongozwa na Jenerali kutoka Tanzania, kikiwa na mamlaka ya kufanya mashambulizi dhidi ya makundi ya waasi nchini Kongo.

Jeshi la Rwanda lilisema kuwa makombora matatu yaliangukia katika ardhi yake, na kumjeruhi raia. "Kama hawako tayari kusitisha hili, tutajibu mara moja na itauma," alisema balozi w arwanda katika Umoja wa Mataifa Eugene Richard Gasana baada ya mazungumzo ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na wasiwasi uliyoongezeka. Wizara ya wakimbizi ya Rwanda ilisema kati ya watu 2,500 na 3,000 wamekimbilia nchini humo kupitia mipaka miwili.

Hujuma dhidi ya mazungumzo ya amani
Siku ya Jumatatu, makundi hasimu yalitangaza kuwa yanasitisha mazungumzo ya amani yanayofanyika katika mji mkuu wa Uganda Kampala, licha ya shinikizo kutoka kwa Umoja wa Mataifa kukomesha uasi huo wa miaka miwili na nusu unaosababisha uharibufu mkubwa mashariki mwa Kongo.

Kwa mujibu wa serikali ya Kongo, mazungumzo hayo yalisitishwa kutoka na tofauti ju ya msamaha kwa wanajeshi walioasi na kurejeshwa kwao katika jeshi la taifa. Ikiungwa mkono na jamii ya kimataifa, serikali ya Kongo inakataa kutoa msamaha kwa karibu viongozi 80 wa kundi la M23, na kuwarejesha tena katika vyeo vya kijeshi.
Rais Joseph Kabila wa Kongo, na Paul Kagame wa Rwanda.

Katika taarifa siku ya Ijumaa, msemaji wa upande wa kisiasa wa M23 Amani Kabasha aliituhumu serikali mjini Kinshasa, kwa kuyahujumu jumla mazungumzo ya amani mjini Kampala. Wengi wa wajumbe wa kundi la M23 ni Watutsi kutoka kundi la awali la waasi amabo waliingizw akatika jeshi la taifa mwaka 2009, na baadae kuasi mwaka 2012, wakidai kuwa Kinshasa ilishindwa kusimamia sehemu yake ya makubaliano.

Waasi walichukuwa udhibiti wa mji wa Goma, ambao ndiyo mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kaskazini kwa zaidi ya wiki moja mwishoni mwa uliyopita, kabla ya kujiondoa kutokana na shinikizo la kimataifa. Serikali ya Kongo kwa muda mrefu imeishtumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi, na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa kamandi ya kundi la M23, iliongozwa na waziri wa ulinzi wa Rwanda.

Mwanaharakati wa haki za binaadamu alisema kuwa katika eneo la Kabagana, karibu na mpaka wa Rwanda, aliwaona wanajeshi wa Rwanda wakiingia kuwasaidia M23. Kigali imekanusha vikali tuhuma kwamba ilikuwa inawapatia silaha na kuwafadhili waasi -- na hata kuwasaidia kwa kutumia vikosi vyake yenyewe.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company