Na Mwandishi Maalumu, Guangzhou
SERIKALI ya Tanzania imeingia mikataba saba na kampuni sita za China yenye thamani ya Sh trilioni 2.72, zitakazowekezwa katika ujenzi wa miradi ya umeme na nyumba za makazi na biashara. Makubaliano ya uwekezaji huo yameingiwa jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mawaziri wengine wa Serikali baada ya kusainiwa kwa mikataba saba ya uwekezaji katika sekta hizo muhimu kwa uchumi wa nchi.
Utiaji saini huo ulifanywa baada ya Pinda kufungua Kongamano la Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na China (Tanzania China Business Forum), uliofanyika katika Hoteli ya Dong Fang, Guangzhou jimboni Guangdong, China.
Kongamano hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Baraza la Biashara la China Afrika (China Africa Business Council-CABC), linashirikisha wafanyabiashara wa China na Tanzania.
Mikataba iliyosainiwa ni kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Tabiau Electric Apparatus Stock Co Ltd (TBEA), ambao ni kwa ajili ya ujenzi wa njia ya umeme ya msongo mkubwa wa 400kV katika Gridi ya Taifa inayotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kaskazini Mashariki hadi Arusha.
Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba, ndiye aliyesaini mkataba huo wenye thamani ya Dola milioni 692.7 za Marekani, pia alisaini mkataba mwingine na Kampuni ya Shanghai Electric Power ambayo ndio itajenga mtambo wa Kinyerezi III.
Mkataba mwingine uliotiwa saini na Mramba ni kati ya Tanesco na Kampuni ya China Gezhouba Group Corporation (CGGC), ambao wamekubali kuendeleza mradi wa umeme unaotokana na nguvu ya maji wa Rumakali, ambao uko katika mikoa ya nyanda za juu kusini.
Miradi hiyo miwili bado iko katika hatua ya upembuzi yakinifu, hivyo gharama zake bado hazijajulikana.
Kampuni ya Mkonge Energy Systems Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Tanzania, Salum Shamte, ilitiliana saini mkataba na Kampuni ya Sino Hyro Resources Ltd, kwa ajili ya kuendeleza umeme wa nguvu za maji wa Masigira. Mradi huo unagharimu kiasi cha Dola milioni 136 za Marekani.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu, aliweka saini mkataba baina ya NHC na kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE) kwa ajili ya kuliwezesha kifedha shirika hilo liweze kujenga nyumba mbalimbali za makazi na biashara nchini. Mradi huo una thamani ya Dola milioni 500 za Marekani.
Aidha, aliwekeana saini mkataba mwingine na Kampuni ya Poly Technologies (POLY) wa kuwa na uhusiano kifedha na kiufundi kati ya kampuni hizo kwa ajili ya kujenga nyumba za makazi na biashara huko Masaki wilayani Kinondoni, Dar es Salaam na gharama za mradi huo ni Dola milioni 200 za Marekani.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Gideon Nassari, aliingia mkataba na Kampuni ya China ya Dalian International Economic & Technical Gooperation Group (CDIG) na Kampuni ya Hydro China Kunming Engineering Corporation kwa ajili ya kujenga kituo cha utafiti na mafunzo ya nishati mbadala na mradi huo una thamani ya Dola milioni 136 za Marekani.
Mramba na Mchechu kwa nyakati tofauti walisema utekelezaji wa miradi hiyo utaanza wakati wowote, kwa kuwa mambo mengi walishayakamilisha katika mazungumzo.
Pinda ambaye yuko katika siku ya nane ya ziara yake ya kikazi kwa mwaliko wa Serikali ya China, bado anaendelea na mikutano mbalimbali.
CHANZO: RAI