WAFUGAJI WAPIGANA DODOMA

HABARI ZETU

VURUGU zimetokea katika Kijiji cha Zajilwa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, huku baadhi ya wanakijiji wakichomewa nyumba zao. Vurugu hizo zilizotokea mwishoni mwa wiki iliyopita, zimewahusisha Wagogo na wafugaji wa jamii ya Kimasai, ambao chanzo chake ni ugomvi wa kugombania maji ya mifugo. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Elizabeth Kaganda, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na bado wanaendelea kuwasaka wahalifu wengine.
Alisema wanawashikilia watu saba ambao tayari wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuharibu mali na kufanya fujo, huku wengine wakiendelea kusakwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Zajilwa, Juma Sendalo, alisema vurugu hizo zilitokea mwishoni mwa wiki baada ya Wagogo na Wamasai kupigana.
“Vurugu hizo zilianza baada ya kutokea hali ya kutoelewana katika malambo ya kunyweshea mifugo maji wakati wakinywesha mifugo yao.
“Baada ya kutoelewana, Wagogo ambao walijiita ni sungusungu walipiga yowe na kwa pamoja wakaelekea katika maboma ya Wamasai ambako walichoma moto na kuharibu vibaya mali za mfugaji, Ngaralai Sogoeti.
“Hao Wagogo hawakuwa sungusungu bali ni kikundi cha wahuni wachache ambao walikuwa na lengo la kuleta machafuko kijijini kwetu,” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, Mzee Sogoeti aliyeharibiwa mali zake, alisema yeye na familia yake hawakuhusika na ugomvi huo lakini alishangazwa na kitendo cha kuchomewa nyumba yake na kuteketeza mali zake.
“Kilichoniponza ni kwa sababu mimi ni Mmasai, nimepata hasara kubwa, hata hivyo niliwaambia vijana wangu hakuna sababu za kulipiza kisasi tumuachie Mungu,” alisema Sogoeti.
Alivitaja baadhi ya vitu vilivyoungua katika chumba chake kuwa ni pikipiki moja, magunia 30 ya mahindi, ndama wawili, kuku saba, ngozi 10 za ng’ombe na Sh 2,722,000.
CHANZO: RAI
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company