Bunge la Somalia limempasisha kwa wingi wa kura Abdeweli Sheikh Ahmed kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika akichukua nafasi ya Abdi Farah Shirdon ambaye hivi karibuni aliondolewa katika nafasi hiyo baada ya kupigiwa kura na Bunge ya kutokuwa na imani naye.
Taarifa zaidi kutoka Mogadishu zinasema kuwa, Abdeweli Sheikh Ahmed amepata kura 239 kati ya 275 zilizopigwa Bungeni na alikula kiapo mara tu baada ya kumalizika zoezi la upigaji kura Bungeni. Akihutubia kabla ya Bunge kuanza zoezi la kumpigia kura Waziri Mkuu mpya, Rais Hassan Muhamoud wa nchi hiyo aliwataka Wabunge wa nchi hiyo kumpigia kura ya kuwa na imani naye Abdeweli. Kwa mujibu wa Katiba ya Somalia, Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo ana muda wa mpaka siku thelathini wa kuunda serikali mpya. Kwa kuzingatia kwamba, Abdiweli Sheikh Ahmed ni mchumi na wala hana uzoefu wa kutosha katika uga wa siasa ana kibarua kigumu kutokana na nchi hiyo kukabiliwa na changamoto nyingi likiwemo suala la usalama. Imeelezwa kuwa, Waziri Mkuu mpya wa Somalia ameshawahi kuhudumu kwa miaka kadhaa kwenye mashirika kadhaa ya kimataifa na Benki ya Kiislamu ya Maendeleo.