“Viongozi wa kisiasa wamekuwa hatari, wanajitahidi kutafuta uongozi kwa gharama yoyote ile, hasa kwa kuwarubuni wananchi kwa kuwapa zawadi jambo ambalo si jema na mtu anayefanya hivyo hafai kuwa kiongozi kwa taifa na mbele za Mungu,” Askofu Zacharia Kakobe
Na Aidan Mhando, Mwananchi
Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe amesema mawaziri mizigo ni matunda ya uteuzi mbovu unaofanywa na mamlaka husika ambao hauzingatii vipawa vya uongozi.
Pia ameonya ukabila na kuvitaka vyama vya siasa vinavyodaiwa kuendeshwa kwa misingi hiyo vifutwe haraka kabla havijachafua hali ya hewa. Akizungumza jana kwenye ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika kanisa hilo Mwenge, Dar es Salaam, Askofu Kakobe alisema si rahisi kwa mtu ambaye hana kipaji cha kuongoza akawa kiongozi, kwani hataweza kumudu nafasi atakayopewa.
“Siku zote uongozi ni kipaji, sasa matatizo yanayotukumba ya kuwa na viongozi mizigo ni kutokana na uteuzi mbovu ambao hauangalii suala la vipaji vya watu,” alisema na kuongeza: “Tumekuwa tukijichagulia tu viongozi tena kwa kuangalia maeneo wanayotoka jambo ambalo siyo jema na la hatari, mifano hai tunaiona sasa. Wanachokifanya viongozi mizigo ni kujihudumia wao na kuwatelekeza wananchi ambao ndiyo wangekuwa wa kwanza kuhudumiwa.”
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CCM na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye walitaja orodha ya mawaziri wanaoelezewa kuwa mizigo. Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake Adam Malima.
Orodha hiyo iliongezeka baada ya Bunge kumtaja Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Hawa Ghasia pamoja na Manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kupima na kutafakari kama wanatosha kusimamia wizara hiyo baada ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufichua ufisasi kwenye wizara hiyo.
Viongozi wanaotoa zawadi
Akizungumzia suala la viongozi wa kisiasa kutoa zawadi kwa wananchi alisema ni hatari, kwani ipo siku watataka kurudisha walichokitoa. Alisema wananchi wamekuwa wakirubuniwa kwa khanga, vitenge, fulana na chakula cha siku moja ili kuwapa watu hao nafasi ya uongozi, lakini baada ya hapo kinachofuata ni mateso, kwani wananyonywa na maisha yanazidi kuwa magumu kwao.
“Viongozi wa kisiasa wamekuwa hatari, wanajitahidi kutafuta uongozi kwa gharama yoyote ile, hasa kwa kuwarubuni wananchi kwa kuwapa zawadi jambo ambalo si jema na mtu anayefanya hivyo hafai kuwa kiongozi kwa taifa na mbele za Mungu,” alisema Askofu Kakobe.
Alisema wananchi wanatakiwa kuwakataa viongozi wa aina hiyo, kwani hawana vipaji vya uongozi, bali wanatumia fedha kutafuta nafasi wanazozitaka na kwamba wakipata watawatelekeza kwa kurudisha walichokitoa.”
Ukabila.
Akizungumzia ukabila, Askofu Kakobe alisema miaka ya nyuma taifa lilikuwa halina vitendo vya ukabila, lakini kwa sasa hali imekuwa mbaya, kwani unaonekana waziwazi.
Alisema baadhi ya vyama vya siasa nchini vimekuwa vikidaiwa kuendeshwa kikabila, huku sheria za nchi zikikataza... “Kama kuna chama cha siasa kinaendeshwa kikabila kifutwe haraka, kwani ni hatari kwa nchi na taifa kwa jumla.”
Aidha, Askofu Kakobe alisisitiza kuwa ni aibu kwa kiongozi wa chama cha siasa kuendekeza ukabila na kwamba hawawezi kukubali kuona mtu ambaye ni mkabila anakuwa kiongozi wa nchi.