Kufutwa kodi ya simu, Bunge aibu tupu



Rais Jakaya Kikwete
Na Mwananchi
Hatua ya Rais Jakaya Kikwete kutia saini hati ya dharura ili Muswada wa Fedha wa mwaka 2013 ufanyiwe marekebisho na kuondoa tozo ya kodi kwa laini za simu imeliacha Bunge katika fadhaa na fedheha kubwa.
Bunge la Bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2013 lilishuhudia wabunge wa chama tawala wakitumia wingi wao bungeni kupitisha kodi hiyo ambayo iliamsha hasira na vilio kutoka kwa wananchi kutoka kila kona ya nchi.
Tunasema hatua hiyo ya Rais imeleta fadhaa na fedheha kwa Bunge kutokana na kuwapo matukio mengi ya aina hiyo katika kipindi kifupi, ambapo Bunge limekuwa likipitisha miswada mingi muhimu kwa ushabiki wa kisiasa badala ya kuangalia masilahi mapana ya taifa. Rais kwa kuwasitiri wabunge wa chama chake amekuwa akitia saini miswada hiyo na kuwa sheria, lakini baadaye amekuwa akisikiliza hoja za wapinzani na kulazimika kurudisha sheria hizo bungeni ili zifanyiwe marekebisho.


Siyo nia yetu hata kidogo kuorodhesha hapa sheria zote ambazo Rais amezirudisha bungeni kufanyiwa marekebisho katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo, wasomaji wetu watakumbuka kuwa, moja ya sheria nyeti zilizorudishwa bungeni ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo hasa iliyoanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya yapata miezi 18 iliyopita. Kama tulivyosema hapo juu, muswada wa sheria hiyo na miswada mingine mingi muhimu ilipitishwa na Bunge kwa ushabiki wa kisiasa na kiitikadi, kwa maana ya hoja za wabunge wa upinzani kuzimwa au kujadiliwa kwa kejeli, vijembe na matusi na hatimaye kupuuzwa.


Ni katika muktadha huo, Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 iliyoanzisha tozo ya kodi kwa laini za simu inapaswa kuangaliwa. Bunge kwa staili hiyohiyo ya ushabiki wa kisiasa na kiitikadi lilipitisha muswada wa sheria hiyo, huku wabunge wa upinzani wakipinga na kuainisha athari zake kwa wananchi na uchumi wa taifa. Ni kweli Rais alisaini muswada huo na kuwa sheria, lakini kutokana na athari zake kwa uchumi na wananchi kwa jumla, sasa ameirudisha bungeni kwa hati ya dharura akitaka ifanyiwe marekebisho na kuifuta kodi hiyo mara moja.


Ni aibu kwa Bunge, Serikali na Kamati ya Bajeti iliyobuni tozo hiyo kutoona mapema madhara ambayo yangesababishwa na kodi hiyo ya Sh1,000 (kwa kila laini ya simu kila mwezi) kwa wananchi maskini ambao wanahangaika kupata mlo mmoja kwa siku. Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kutojua hali halisi ilivyo, hasa vijijini walikaririwa bungeni wakitetea kwa nguvu hoja ya kuwekwa kwa tozo hiyo, wakidai kila mwananchi anao uwezo wa kuilipa kila mwezi.


Kutokana na utata uliosababishwa na tozo hiyo, kodi hiyo ilikuwa haijaanza kulipwa mpaka sasa, licha ya Bunge kupitisha muswada huo Julai, mwaka huu. Rais Kikwete baadaye aliingilia kati kwa kuagiza mamlaka zote husika kukutana mara moja kumaliza mvutano wa kodi hiyo kwa kutafuta vyanzo mbadala vya kodi ili kuziba pengo la Sh178 bilioni ambazo zingetokana na kodi kwenye laini za simu. Ni matarajio yetu kwamba Bunge letu litakuwa limepata somo la kutosha, hivyo litakuwa makini siku zijazo kwa kuhakikisha linapitisha miswada pasipo hila wala ushabiki wa kisiasa.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company