Matukio ya baadhi ya wanawake kukamatwa, kudhalilishwa mbele ya familia kwa kushikwa sehemu za siri bila ya ridhaa yao, na kubakwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili nchini, ni muendelezo wa madhila mbalimbali yanayoendelea kuwakumba wanawake nchini.
Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoongozwa na mwenyekiti wake James Lembeli iliyosomwa bungeni hivi karibuni.
Operesheni hiyo ilifanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi iliyoongozwa na wizara tatu za Maliasili na Utalii, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Lengo la operesheni hiyo ni kuwatafuta, kuwakamata na ikibidi ‘kuwaua’ kama si kuwachukulia sheria majangili wanaoua tembo kwa ajili ya kupata meno yake na vifaru kwa ajili ya vipusa, badala yake baadhi ya waliopewa dhamana hiyo wakaacha lengo la msingi na kujikuta wakiwakamata wanawake, kuwachomea nyumba, kuwadhalilisha kwa kiwango cha kutisha na kuwabaka.
Mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa) wilayani Babati alivuliwa nguo na kulazimishwa kufanya mapenzi na wakwe zake kisha kuingizwa chupa sehemu zake za siri.
Mama mwingine mkazi wa Kata ya Matongo wilayani Bariadi, alibakwa na askari watatu huku akiwa ameshikiwa mtutu wa bunduki.
Tukio la kuuawa kinyama kwa Emiliana Gasper Maro lilipotolewa na vyombo vya habari, Serikali kupitia Mkurugenzi wa Wanyama Pori ilitoa taarifa kwa umma ikipinga taarifa iliyorushwa kwenye vyombo vya habari Oktoba 19, mwaka huu kuhusu mauaji ya kutisha yaliyofanywa na askari wa kupambana na ujangili.
Serikali iliwatetea askari wa Operesheni Tokomeza Ujangili kuwa hawahusiki na kifo cha Emiliana.
Hata hivyo, taarifa ya utetezi ilizungumzia majina mawili tofauti ya Evelyn Gasper na Mariana Gasper Mallo wa eneo la Olongadiola wakati muathirika halisi ni Emiliana Gasper Maaro mkazi wa kijiji cha Omgadida, Gallapo.
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA),Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela) na Kituo cha Usuluhishi cha Tamwa (CRC), inatekeleza mpango wa kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto (Gewe II) katika wilaya 10 za Tanzania Bara na Zanzibar.
Ili kufanikisha mpango huo wa miaka miwili (2012-2014) Tamwa iliongoza uundaji wa kamati katika wilaya 10 kwenye vijiji 60 vya Tanzania Bara na Zanzibar zenye jumla ya wajumbe 720.
Kazi kubwa ya kamati hizo ni kufuatilia masuala ya ukatili unaofanywa dhidi ya wanawake na watoto wa kike kwenye maeneo yao.
Taarifa ya Ripoti ya Kamati ya Bunge iliyochunguza sakata hilo, yawezekana imepita sehemu ndogo ya hali halisi ya matukio yalivyokuwa nchini kutokana na muda iliopewa, uchache wa wajumbe ambao siyo rahisi kupita kila kijiji na kila sehemu, hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa baadhi ya matukio haya kubainishwa wazi licha ya kuathiri wanawake na watoto.
Hivyo ni muhimu kwa wanaharakati popote walipo ikiwa ni pamoja na Kamati zilizoundwa na Tamwa katika maeneo mbalimbali ya nchi kuendelea kufichua madhila mbalimbali yaliyowapata watu kutokana na operesheni hii ambayo baadhi ya watu wamepata vilema vya kudumu na vifo wakiwamo baadhi ya wanaume na watoto.
Baadhi ya wananchi waliopoteza maisha katika operesheni hiyo na vijiji vyao kwenye mabano ni Wegesa Kirigiti (Remagwe), Peter Masea (Mrito-Tarime), Mohamed Buto, Massi na Gervas Nzoya (Kasulu-Kigoma).
Utekelezaji wa Operesheni hiyo ni dhahiri umekiuka sheria hasa ibara ya 14 ya Katiba isemayo “Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kutoka kwa jamii kwa mujibu wa sheria” na ibara namba 15 (1) isemayo “ kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru”.
Inatisha kuona askari wa Jeshi la Wananchi na Jeshi la Polisi walioiva kimafunzo kuthamini ustaarabu, kujali utu, kuheshimu na kuzingatia haki za binadamu wanageuka na kufanya unyama kama huo dhidi ya maisha ya raia na mali zao ambao walipaswa kutumia mafunzo yao kuwalinda.
Tayari mawaziri wanne wamejiuzulu kutokana na kadhia hiyo ambao ni Mawaziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki, Mambo ya Ndani Dk. Emmanuel Nchi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Shamsi Vuai Nahodha na wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk. Mathayo David.
Sasa inasubiriwa kuundwa Tume ya Kimahakama ili matokeo ya kina zaidi yapatikane na hatua zaidi zichukuliwe kwa wahusika wote.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
#USOPEN_VIGOGO CHALI
-
SIKU Safi kwa Muaustralia Nick Kyrgios baada ya ushindi dhidi Johnson na
kutinga raundi ya Pili.
- Rafael Nadal akimchapa Millman Seti Tatu zote mfululi...
5 years ago