Madiwani wafurahia mawaziri kung’oka

 NA TANZANIA DAIMA
MADIWANI wa Wilaya ya Tarime, Mara, wamefurahishwa na taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake James Lembeli bungeni na kusababisha mawaziri wanne kuachia nyadhifa zao.

Taarifa hiyo ilielezea jinsi Operesheni Tokomeza Ujangili ilivyosababisha madhara kwa watu mbalimbali.

Mawaziri waliovuliwa nyadhifa hizo ni Khamis Kagasheki wa Maliasili na Utalii, Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Dk. Emmannuel Nchimbi (Mambo ya Ndani) na Mathayo David Mathayo wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo.

Diwani wa Kata ya Nyarukoba, Mustapha Masian aliyekumbwa na operesheni hiyo kwa kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi katika mahakama ya Bunda, alisema hatua iliyochukuliwa ya mawaziri hao kuachia ngazi ilitokana na wabunge kuchachamaa pamoja bila kugawanyika katika itikadi.

“Tunashukuru hatua iliyochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete, lakini hatua hiyo imekuja baada ya wabunge kuungana kwa kuweka itikadi zao pembeni kuchachamaa baada ya wananchi waliopatwa na madhara hayo kuyawasilisha kwa vielelezo kwa wabunge wao, sasa tunataka Kikwete ahakikishe anawachukulia hatua za kisheria wale wote waliosimamia operesheni hiyo makamanda na kisha serikali iharakishe kutufidia tuliokumbwa na madhara hayo,” alisema Masian.

Diwani Magarya Wambura wa Kata ya Goron’ga aliitaka serikali ihakikishe inawachukulia hatua za kinidhamu Wakuu wa Wilaya zilizopitiwa na operesheni unyanyasaji huo kwa wananchi, mifugo na kuchomewa nyumba na mateso makali wale ambao hawakuwasilisha taarifa zao kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda juu ya ukiukaji huo.

“Hatua nyingine ambayo rais anatakiwa kuifanya ni kuhakikisha anawawajibisha Wakuu wa Wilaya zilizopitiwa na unyanyasaji huo kwa wale ambao hawakuweza kutoa taarifa zao kwa Pinda juu ya kinyume na malengo ya operesheni hiyo,” alisema Wambura.

Diwani wa Kata ya Nyanungu, Man’genyi Ryoba aliitaka serikali kupitia Rais Kikwete kuhakikisha inawaondolea kero za upungufu wa maeneo ya kuchungia mifugo ambayo alidai kuwa haikuweza kuwawekea maeneo ya malisho.

Ryoba alisema hadi sasa wananchi wa vijiji vya Mangucha, Kegonga, Masanga na Gibaso waliouawa, kujeruhiwa na kuharibiwa mazao yao kabla ya operesheni tokomeza ujangili hawajafidiwa na kusaidiwa upungufu wa chakula walionao kutoka Kitengo cha Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu licha ya taarifa za madhara hayo kuwasilishwa mara kwa mara muda wote katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri wilayani hapa.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company