Wanajeshi wa Sudani Kusini mjini JubaREUTERS/Goran Tomasevic
Na
RFISerikali ya Juba inasema waasi wamefanikiwa kuchukua udhibiti wa majimbo ya Joglei na Unity huku maelfu ya watu wakikimbilia katika Mako Makuu ya umoja wa Mataifa kupata hifadhi
Rais wa Marekani Barrack Obama anasema kuwa hatua zaidi zitachukuliwa nchini Sudan Kusini iwapo makabiliano zaidi yataendelea kushuhudiwa nchini humo baada ya ndege yake ya kijeshi kuvamiwa mwoshoni mwa juma lililopita.
Kauli ya rais Obama inakuja kipindi hiki Jumuiya ya Kimataifa ikiendelea na juhudi za Kidiplomasia kujaribu kuleta utulivu nchini humo na Umoja wa Mataifa unaahidi kutuma wanajeshi zaidi wa kulinda amani.
Mataifa ya Uingereza, Marekani, Kenya, Lebanon na Uganda yamekuwa yakiwaondoa raia wake waliopata hifadhi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kutokana na makabiliano hayo ya kijeshi.
Mwishoni mwa juma lililopita jeshi la Kenya limefanikiwa kuwarudisha nyumbani wakenya zaidi ya themanini pamoja na kupeleka msaada wa vyakula na dawa kwa watu waliokimbilia katika kambi ya Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya watu mia tano wameuawa nchini Sudan Kusini tangu yatokeye makabiliano kati ya wanajeshi wa serikali na wale wanaomuunga mkono aliyekuwa Makamu wa rais Riek Machar ambaye anasema anataka kuwa rais wa nchi hiyo.
Juma lililopita baadhi ya mawaziri wa Mambo ya nje kutoka nchi za kiafrika walikuwa jijini Juba kushauriana na rais Salva Kiir kujaribu kupata suluhu la kisiasa kati yake na Riek Machar bila mafanikio.