MWANAFUNZI wa darasa la nne shule ya msingi Mji Mpya aliyetambuliwa kwa jina la Doris Samwel (10) amekutwa amekufa ndani ya karo la maji. Maiti ya mwanafunzi huyo ilikutwa jana saa 2:00 asubuhi maeneo ya Majohe Viwege, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Marietha Minangi, alisema maiti hiyo ilikutwa ndani ya karo la maji jirani na nyumba yao.
Inasadikiwa mtoto huyo alitumbukia wakati akijaribu kuchota maji.
Katika tukio jingine, watu wawili wamekufa papo hapo baada ya pikipiki yao kugongana na lori, wilaya ya Temeke.
Ajali hiyo ilitokea juzi saa 2:00 usiku katika Barabara ya Yombo Buza eneo la Mama Kibonge, ambapo gari aina ya Mitsubishi Rosa yenye namba T166 BXN ikiendeshwa na mtu asiyefahamika akitoka Tandika kwenda Buza, alipofika maeneo hayo aligongana na pikipiki yenye namba T849 CSE aina ya Boxer.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema, katika ajali hiyo mwendesha pikipiki na abiria wake waliotambuliwa kwa majina ya Ismaili Hamidu (35) na Twaha Jordan (30) walikufa.
Katika tukio la tatu, mtembea kwa miguu ambaye hajafahamika amekufa baada ya kugongwa na gari akivuka barabara ya Obama eneo la Taasisi ya Magonjwa ya Saratani ya Hospitali ya Ocean Road.
RC aigiza polisi kukamata gari za Serikali Na Khatib Suleiman, Zanzibar POLISI Zanzibar imetakiwa kuzichukulia hatua za kisheria gari zote za Serikali ambazo zitabainika kuendeshwa bila ya kukatiwa Bima.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi mwishoni mwa wiki, wakati alipofungua semina ya siku moja ya Shirika la Bima kwa Jeshi la Polisi la usalama barabarani mjini hapa.
Alisema ni makosa gari za Serikali kuendeshwa bila ya kukatiwa bima kwani agizo la Serikali linazitaka gari hizo kukatiwa bima kama zilivyo gari nyingine za abiria.
Aidha aliwataka askari wa barabarani kupambana na mbinu mbalimbali zinazofanywa na madereva ambao baadhi yao huonesha kadi za bima bandia na kulikosesha taifa mapato.
Mapema Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Bima, Nasir Ahmed Abrahman, alisema Shirika la Bima limejizatiti kuhakikisha linaongeza mapato yake kwa kubuni njia mbali mbali katika vianzio vipya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Mkadam Khamis Mkadam, alisema Polisi imejipanga kuhakikisha inapambana na baadhi ya watu wajanja wenye nia ya kulikosesha shirika mapato kwa kufanya udanyanyifu.
CHANZO:HABARILEO