MAKALA; Pinda amewasaliti mawaziri wenzake


NA TANZANIA DAIMA.
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda juzi aliwasaliti mawaziri wenzake wanne ambao walilazimika kuachia ngazi kutokana na kushindwa kuwachukulia hatua watendaji wa chini yao waliotesa na kuua watu na mifugo kwenye utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.

Pinda alitajwa kuwa waziri mzigo namba moja wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete aliyeshindwa kuwasimamia mawaziri wenzake walioshindwa kuwajibika.

Badala yake Pinda kama mtuhumiwa namba moja, juzi jioni alijigeuza msemaji wa Rais Kikwete akilitaarifu Bunge kuwa mkuu huyo wa nchi ameridhia mawaziri hao wanne wang’oke.

Mawaziri hao ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ambaye baada ya ushauri wa wabunge alikubali kujiuzulu mwenyewe kwa ridhaa yake tofauti na wenzake watatu waliotangazwa kuong’olewa.

Hao ni Dk. Mathayo David wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Emmanuel Nchimbi wa Mambo ya Ndani na Shamsi Vuai Nahodha wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Kamati Ndogo ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira iliyoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli ilionyesha madudu mengi sana yaliyofanywa na watendaji wa wizara hizo wakiongozwa na majeshi yetu.

Hii ni mara ya tatu kwa Baraza la Mawaziri la Kikwete kubomoka, mara ya kwanza ikiwa mwaka 2008 ambapo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alilazimika kujiuzulu kufuatia ripoti ya kamati teule ya Richmond.

Mara ya pili ilikuwa mwaka jana baada ya mawaziri saba kulazimishwa na Bunge kujiuzulu na sasa baraza limebomoka tena mara nyingine na hivyo kuweka rekodi kwa utawala wa Kikwete kubadili mawaziri mara nyingi.

Hii inaashiria udhaifu wa serikali hii ya awamu ya nne, inamaanisha kushindwa, kutokuwa na umakini, ubabaishaji, uswahiba wa wateuliwa kwa mteuzi na kulindana kwa kutochukuliana hatua.

Haya ni maajabu kuona Pinda hadi sasa anapata ujasiri wa kusimama mbele ya Bunge na umma akijifanya kusikitika badala ya kujiwajibisha mwenyewe kama alivyofanya Balozi Kagasheki ambaye kweli alionyesha ukomavu wa uongozi.

Pinda amesimangwa muda mrefu na Bunge hadi kufikia hatua ya wabunge kuanza kujiorodhesha mara mbili wakitaka kupiga kura ya kutokuwa na imani naye, lakini amegoma kujiwajibisha.

Wakati wa kujadili ripoti za kamati tatu za Bunge za Serikali za Mitaa (LAAC), Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC) na ile ya Bajeti, wabunge walimtaka Pinda ang’oke pamoja na mawaziri wengine mizigo, lakini akagoma pia.

Waliopendekezwa kung’oka ni Dk. Mathayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia na Naibu wake, Agrey Mwanri, Waziri wa Kilimo, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima.

Kelele hizo zilipita, mawaziri wakaendelea na kazi, mteuzi wao wala hakushtuka kuona wananchi wanakereka. Hadi rais anaondoka kwenda Marekani hakusema lolote kuhusu malalamiko ya wabunge kwa Pinda na baadhi ya mawaziri.

Nchi hii imekuwa ya ajabu chini ya CCM, viongozi wanalindana, hakuna anayechukuliwa hatua badala yake watu wanalalamika na viongozi wao nao wanalalamika.

Operesheni Tokomeza Ujangili imefeli, hakuna majangili waliokamatwa wala kufikishwa mahakamani ila watu wamekufa na mifugo yao imepigwa risasi na kupigwa mnada.

Leo Bunge limewang’oa mawaziri bila kurekebisha mfumo wa utumishi wa umma na hivyo makatibu wakuu na wakurugenzi watabaki kuwa na pembe mbele ya mawaziri wao kama Lembeli alivyolieleza Bunge kuwa Kagasheki ameponzwa na Katibu wake Mkuu.

Wako wabunge wanatajwa kuhusika na ujangili lakini hawajaguswa, lakini hao hao ndio wamewashambulia mawaziri hadi wakang’oka, kweli vita hii ya ujangili itafanikiwa kweli?

Pinda amewatoa kafara mawaziri wenzake, akaacha kujiuzulu na kukimbilia kumpa rais taarifa za kuridhia kuwang’oa wenzake. Kwa mpango huu hata wakiteuliwa mawaziri wapya kujaza nafasi hizi tutakuwa tumemaliza tatizo katika mfumo mbaya kama huu?

Wala tusishangae kusikia hadithi hii ikawa imeishia hapo bila makatibu wakuu, watendaji wa chini na askari waliohusika na unyama huu kuguswa na mkono wa sheria.

Hii ndiyo nchi yetu, haya mambo yako hivyo na hii ndiyo sababu kubwa ya kushindwa katika vita ya dawa za kulevya kwani wahusika wakuu wa biashara hiyo hawakamatiki bali wanakamatwa ‘dagaa’ wanaobeba dawa hizo.

Huu ni mtego kwa Kikwete, ni mtego kwa CCM kwa sababu hizi ni dalili za anguko la kushindwa. Serikali yake imebakia kuwa ya mawaziri kujiuzulu na kuteua wengine pasipo kurekebisha mfumo.

Mara kadhaa wapinzani wameeleza udhaifu wa mawaziri wa Kikwete, wakafikia hatua ya kuomba iundwe tume huru ya majaji kuchunguza mauaji ya raia, lakini Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema wamekuwa na majibu ya hovyo.

Raia wema wameuawa kwa risasi za polisi kwenye mikutano na maandamano ya vyama, wakulima na wafugaji wameuawa, lakini mawaziri husika akiwemo Dk. Nchimbi dhamiri zao hazikuwasuta wakawajibika hadi maji yalipowafika shingoni Ijumaa. Tafakari!

Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company