NA BASHIR NKOROMO
KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi
CCM, Nape Nnauye amesema
amepokea kwa faraja kubwa, hatua
ya mawaziri wanne kuenguliwa
nyadhifa zao kwa ridhaa ya Rais
Jakaya Kikwete.
"Najisikia vizuri, maana kwa kitendo
cha mawaziri hao wanne kuchuliwa
hatua, ninaamini kitasaidia wale
wengine waliolala nao waamke. Bila
shaka sasa hakuna atakayelala na
akilala anajua itakula kwake.",
alisema Nape akijibu swali la
mtangazaji wa Kituo cha Televisheni
cha ITV, Emmanuel Buhohela, kwenye
kipindi cha 'mahijiano' cha
televisheni hiyo, mjini Dar es
Salaam, leo asubuhi.
Mtangazaji huyo alitaka kujua, Nape
kama kiongozi wa ngazi ya juu CCM,
amejisikia au kupokeaje hatua ya
Bunge
kumuomba Rais kuwawajibisha
mawaziri hao wanne na kisha Rais
kuridhia ombi hilo kwa kutengua
uteuzi wake wa nafasi za mawaziri
hao jana.
Mawaziri waliofutiwa uteuzi wao na
Rais na nafasi walizotoka zikiwa
kwenye mabano ni, Dk. Emmanuel
Nchimbi (Waziri wa Mambo ya
Ndani), Shamsi Vuai (Waziri wa
Ulinzi), Mathayo David Mathayo
( Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na
Khams Kagasheki (Maliasili na
Utalii) ambaye ndiye pekee pamoja
na uteuzi wake kutenguliwa na Rais
lakini alitangaza kujiuzulu akiwa
Bungeni, jana.
Kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri
hao kulitangazwa rasmi Bungeni
jana jioni, na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, hatua inayoaminika kuwa
imetokana na shinikizo la bunge,
baada ya Kamati yake ya Kudumu
ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
kubaini 'uozo' katika operesheni
iliyofanyika hivi karibuni ya
tokomeza ujangili.
Chini ya Mwenyekiti wake, James
Lembeli, Kamati hiyo ilieleza
kwamba pamoja na mambo kadhaa
iliyoyaeleza kuwa ya hovyo
yaliyojitokeza kwenye operesheni
hiyo, vitendo vingi ikiwemo ubakaji
na udhalilishaji vilifanyika ambapo
ni kinyume na utu na haki za
binadamu.
Kufuatia kadhia hiyo, Kamati hiyo
kupitia kwa Lembeli, iliwataka
mawaziri wanaohusika kutazama
kama wanafaa kuendelea na
nyadhifa zao au wajiuzulu, na pia
Kamati hiyo ikaenda mbali zaidi kwa
kumuomba Rais Jakaya Kikwete
kuchukua hatua ya kuwawajibisha.
Akizungumzia zaidi hatua hiyo, Nape
alisema, pamoja na mawaziri hao
kuwajibika, lakini ipo haja ya
kwenda mbali zaidi kwa kutazama
mifumo na sheria zilizopo sasa kwa
kuwa inaonekana navyo ni miongoni
mwa vyanzo vya vikwazo katika
utekelezaji wa utawala bora.
"Kwa mfano leo hii, mawaziri
wameng'oka, sawa ni jambo jema,
sitetei, lakini inawezekana kabisa
kuna mifumo na sheria ambazo
zilimkwaza Waziri huyu kutimiza
wajibu wake. Mfano, alihitaji
kumfukuza mtu kazi kwa kuzembea
jambo fulani, lakini malmaka ya
kufukuza kazi mtumishi yapo kwa
Katibu Mkuu wa Wizara, hapa
atafanyaje!", alisema Nape na
kuongeza;
"La msingi hapa ni lazima sasa
hatua hizi ziende mpaka chini huku
kwa watendaji, ili isiwe mawaziri
wanawajibishwa tu kwa sababu ya
dhamana zao za kusimamia kisiasa,
huku watendaji wanazidi kuvuta
shuka bila hofu wakati baadhi yao ni
sehemu ya matatizo".
Akijibu swali kuhusu ziara za Katibu
Mkuu na sekretarieti ya CCM
mikoani, Nape alisema, ziara hizo
ndiyo kwanza zimeanza, na mado
moto wake mkubwa zaidi unakuja
hasa itakapokaribia uchaguzi mkuu
wa 2015.
Nape alisema, ziara hizo,
zimeonyesha matunda makubwa
sana, klwa kuwa zimesaidia
kupunguza kero nhyingi katika
maeneo zilikofanyika.
Alitoa mfano wa ziara hiyo
ilivyoweza kuondoa msongamano wa
malori wilayani Tunduma mkoani
Mbeya, akisema kwamba wakati
Kinana na msafara wake wanaingia
tunduma walikuta msongamano ni
mkubwa sana kutokana na
wafanyakazi wanaohudumia malori
hayo kufanya kazi kwa mda mfupi.
"Baada ya kuiagiza serikali isimamie
wafanyakazi wa eneo hilo wafanya
kazi kwa saa 24, kwa zamu, siku ya
pili yake ya agizo hilo, msongamano
ulionekana kupungua sana na kuleta
nafuu kwa madereva na wafanya
biashara kwa jumla pale Tunduma",
alisema Nape.
Nape alisema, pia kutokana na ziara
hizo, mgogoro uliokuwa mkubwa
baina ya wananchi na wenye mgodi
wa machimbo Nyamongo,
umepungua kwa asilimia 90 sasa, na
hali imekuwa ya kuridgisha sana.
Akizungumzia wabunge wanaodaiwa
kulipwa posho bila kuzifanyia kazi,
Nape alisema, kurudisha fedha pekee
hakutatosha, kwa upande wa CCM
ambayo ndiyo yeneye wabunge wengi
itabidi ichukue hatua zaidi dhizi ya
waliohusika na kadhia hiyo bila
kuoneka mtu.
Kuhusu ajira kwa vijana, Nape
alaisema ili kutimiza hilo, ni lazima
viwanda vifufuliwe kwa dhati
kabisha, ikiwa ni kuchukua hatua za
kuwanyang'anya wawekezaji
waliochukua viwanda mbalimbali
kwa lengo la kuviendeleza lakini
baadhi yao majengo ya viwanda
hivyo wakayafanyia shughuli zingine
tofauti ikiwemo kuyageuza maghala.
Nape aliitaka pia serikali kupunguza
au kuondoa kabisa urasimu katika
kupokea wawekezaji katika sekta
mbalimbali za uchumi hapa nchini
akisema, kwamba, kwa sasa vikwazo
na urasimu bado ni vingi sana kiasi
kwamba wawekezaji waanakwazika
na hivyo kupunguza kasi ya
uwekezaji ambao wakiongezeka
haraka ajira kwa vijana nazo
zitakua haraka.
Alisema, hatua ya sasa inayofanywa
na CCM kusimamia serikali ni ya
kawaida kabisa kwa kuwa kazi hiyo
haipaswi kufanya na wapinzani kwa
kuwa sera inayotekelezwa siyo yao,
na wahaijui.
Nape aliahidi kwamba katika
uchaguzi zijazo CCM itakomba viti
vyote vya ubunge na udiwani
vililivyopo sasa chini ya wapinzani,
akisema, kwamba, baada ya
wapinzani kujaribiwa wameshindwa
kuonyesha matunda yoyote ya
kusaidia wananchi na hivyo
kutokuwa mbadala wa CCM .