Mlipuko waharibu sehemu ya jengo la usalama Misri
Mlipuko mkubwa katika jengo moja la usalama kaskazini mwa Misri umesababisha watu wapatao 14 kuuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa.
Maafisa nchini humo pamoja na vyombo vya habari vya serikali wamesema, mlipuko huo, ambao umeripotiwa kusababishwa na bomu lililotegwa katika gari, umesababisha kuporomoka sehemu ya jengo hilo katika mji wa Mansoura.
Waziri Mkuu wa Mpito Hazem Beblawi ameelezea tukio hilo kama "kitendo cha ugaidi".
Mashambulio dhidi ya majeshi ya usalama na polisi nchini Misri yameongezeka tangu jeshi nchini humo limtoe madarakani rais wa Kiislam Mohammed Morsi mwezi Julai, 2013.
Mpaka sasa hakuna kikundi kilichodai kuhusika na shambulio hilo.
Bwana Beblawi amekiambia kituo cha televisheni cha ONTV: "Serikali itafanya kila iwezalo kuwasaka wahalifu wote waaliotekeleza, kupanga na kusaidia kufanyika kwa shambulio hilo."
Athari za mlipuko huo zilipatika katika maeneo ya umbali wa kilomita 20 kutoka eneo la tukio.
Televisheni ya Misri imewaomba watazamaji wake kwenda hospitali kutoa damu.
Kikundi cha Muslim Brotherhood - kinachomuunga mkono Bwana Morsi na kilichopigwa marufuku na serikali ya mpito ya Misri, kimelaani shambulio hilo.
"Muslim Brotherhood kinachukulia kitendo hiki kama shambulio la moja kwa moja katika umoja wa watu wa Misri," kimesema katika taarifa yake.
Mkuu wa usalama amejeruhiwa'
Mlipuko huo ulipiga jengo hilo Jumatatu usiku wa manane.
Zaidi ya watu 100 walijeruhiwa. Taarifa za vyombo vya habari zinasema mkuu wa usalama wa jimbo ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa.
Mlipuko huo ulivunja vioo vya madirisha ya majengo jirani na athari zake kufika umbali wa kilomita 20 kutoka eneo la tukio.
Mansoura - mji wenye idadi ya watu 480,000 - ni makao makuu ya mkoa wa Dakahliya katika jimbo la Nile Delta.
Tangu kuondolewa madarakani kwa Bwana Morsi - rais wa kwanza wa Misri aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasia - wafuasi wake wamekuwa wakiandaa maandamano makubwa wakitaka kuachiliwa huru kwa kiongozi wao.
Zaidi ya wanachama 2,000 wa Muslim Brotherhood wamekamatwa, na 450 kati yao, siku ya Jumatatu walianza mgomo wa kususia chakula wakipinga kudhalilishwa.".
Bwana Morsi kwa sasa anakabiliwa na kesi tatu tofauti za uhalifu zikihusishwa na nafasi yake akiwa madarakani.
Kesi ya kwanza ilifunguliwa tarehe Novemba, lakini imeahirishwa hadi Januari 8, 2014.