Aliyekua makamu wa rais nchini Sudan Kusin, Riek Machar(Photo : AFP)
Na
Flora Martin MwanoMaelfu ya vijana watiifu kwa Makamu wa Rais wa zamani wa Sudani Kusini Riek Machar wameripotiwa kuandamana katika mji mkuu wa jimbo la Jonglei, Bor ambao kwa sasa unadhibitiwa na majeshi ya serikali, hatua ambayo inafifisha matumaini ya kusitishwa kwa mapigano ya takribani majuma mawili.
Serikali ya Juba imeahidi kusitisha mapigano, lakini msemaji wa Jeshi amethibitisha kuwa bado vikosi vyao vinaendeleza mapambanao katika eneo la Kaskazini lenye utajiri wa mafuta.
Wakati hayo yakijiri Rais Salva Kiir na hasimu wake ambaye alitimuliwa katika wadhifa wa Umakamu wa Rais Riek Machar wametakiwa kuanza haraka mazungumzo ya amani ili kutafuta suluhu ya mapigano hayo.
Viongozi wa nchi wanachama wa IGAD waliokutana jijini Nairobi siku ya ijumaa wametoa muda wa siku nne kwa Rais Kiir na Bwana Machar kuanza mazungumzo ya uso kwa uso juu ya mzozo huo.
Tayari Rais Salva Kiir amekubaliana na wazo hilo ingawa tarehe rasmi ya kuanza majadiliano bado haijabainishwa.
Mpinzani wake Riek Machar nae amekubali ingawa bado anaendelea na shinikizo la kutaka kuachiwa huru kwa wanasiasa wanaoshikiliwa na serikali kabla ya kushiriki mazungumzo hayo.
Watu zaidi ya elfu moja wameuawa toka kuanza kwa mapigano hayo na wengine zaidi ya laki moja na ishirini wameyakimbia makazi yao.
Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vimeendelea kuwasili nchini humo kusaidia jitihada za kuimarisha usalama ulizoroteshwa na machafuko hayo yenye mizizi ya siasa za kikabila.