Zitto apasua jipu

NA TANZANIA DAIMA.
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema hana chuki na yeyote ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Zitto, alisema baadhi ya watu wanafikiri ana chuki na viongozi wenzake baada ya Kamati Kuu ya CHADEMA kumvua nyadhifa zake kwa madai ya usaliti.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwandiga mjini Kigoma.

Katika mkutano huo ambao ni wa kwanza kuufanya mkoani Kigoma tangu alipovuliwa nyadhifa zake ndani ya CHADEMA, alisema baadhi ya wabunge walikuwa wakisubiri waone namna atakoavyoshirikiana na wenzake bungeni.

“Nilipoingia bungeni kwa mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa yanayoendelea ndani ya chama chetu, nilikaa pamoja na Mbunge Tundu Lissu. Wabunge wengine walidhani tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni vicheko na mazungumzo.

“Hii ni kwa sababu sina chuki na mtu yeyote yule. Nimejifunza kutojenga chuki na watu na badala yake kuchukua kila tukio kama changamoto ya maisha,” alisema.

Zitto alisema siasa inakabiliwa na tatizo kubwa la kutoaminiana jambo linalozalisha kutokuvumiliana.

Alibainisha kuwa kwa sasa kuwa na mawazo tofauti katika vyama vya siasa au katika asasi za kijamii kunatafsiriwa kuwa ni uhaini.

Alisema bila ya kuwa na tofauti za mawazo kamwe taifa na vyama haviwezi kuwa imara.

“Demokrasia imara ni zao la tofauti za mawazo na uhuru wa mawazo. Kama hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha uhuru wa mawazo na tofauti za mawazo, tutajenga taifa lenye watu wenye kuogopa na waliojaa woga,” alisema Zitto.

Alisema wanachama wanapoogopa uongozi badala ya kuuheshimu ni udikteta na uongozi unapoogopa wanachama una tafsiri ya demokrasia.

Aliongeza kuwa bila demokrasia ya uwazi na kuvumiliana kutakuwa na taifa la kidikteta na kwamba ni lazima vyama vya siasa viongozwe kwa namna ile ile ambayo taifa litaongozwa.

Alisema ni vema viongozi wakaruhusu mawazo tofauti na hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja huku akieleza kuwa siasa ina misingi yake ambayo wanasiasa walio wengi wanasahau kwa makusudi.

Akizungumzia mabilioni ya Uswisi, aliwaambia wana Kigoma kuwapuuza watu wanaodhani anatafuta umaarufu binafsi.

“Wanaposema ninatafuta umaarufu, ni uongo, mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu ni uongo! Kinachonisukuma kufanya vyote hivi ni ninyi. Ninasukumwa kila ninapowaona watoto bado wanatembea bila viatu, kila ninapoona akinamama.

wanapoteza maisha yao katika uzazi, kila ninapoona vijana ambao hawana uhakika wa kupata hata mlo mmoja kwa siku kwa kukosa kazi; ninapoona wazee wa Kigoma kukosa hata shilingi mia moja kununua chai asubuhi. Ninawaona si wanaKigoma bali mamilioni ya Watanzania wakiishi katika hali hii,” alisema Zitto.

Alisema kutokutaja kwake majina ya watu walioficha fedha nje ya nchi haimaanishi kuwa hana majina ya watu hao, na kwamba mwanasheria mkuu wa serikali aliamua kutumia fursa ya Bunge kuudanganya umma.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company