Leo siku ya mapumziko

RAIS Jakaya Kikwete ametangaza leo ni siku ya mapumziko kwa Watanzania wote kusherehekea Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais-Ikulu, ilieleza Rais Kikwete alitangaza uamuzi huo mjini Zanzibar ambako jana ameungana na Watanzania na Wazanzibari kusherehekea Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964.

Mapinduzi hayo yaliyoongozwa na mwasisi wa Zanzibar na taifa la Tanzania, hayati Abeid Amani Karume yalifanikiwa kuung’oa madarakani utawala dhalimu wa Sultan na kuwawezesha kwa mara ya kwanza katika historia Waafrika walio wengi kujitawala ndani ya nchi yao wenyewe.

Yalikuwa ni mapinduzi ya Zanzibar yaliyofungua njia ya kuzaliwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – miezi mitatu baada ya mapinduzi hayo – Aprili 26, 1964.

Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Ali Mohamed Shein, ametangaza kuwa leo ni siku ya mapumziko Tanzania Visiwani kusheherekea Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Shein alitoa kauli hiyo alipohutubia wananchi kwenye Uwanja wa michezo wa Amaan, Zanzibar katika kusherehekea Miaka 50 ya Mapinduzi.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company