CHADEMA wapata mgombea ubunge Kalenga, Ni Grace Tendega aliyeukosa 2005

KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imemtangaza Grace Tendega kuwa mgombea ubunge Jimbo la Kalenga.
Jimbo hilo lipo wazi baada ya kifo cha mbunge wake, William Mgimwa, ambaye pia alikuwa Waziri wa Fedha. Alifariki dunia mwezi uliopita nchini Afrika Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya CHADEMA, Kinondoni jijini Dar es Salaam, jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema wana utaratibu tofauti wa kupata wagombea wao kwa kuzingatia vigezo vinne muhimu.

Alivitaja vigezo hivyo ni Kamati Tendaji ya Wilaya husika kukaa na kutoa maoni yake, lakini kigezo cha pili hutegemea pia kupata maoni ya wadau na viongozi wa taasisi mbalimbali katika eneo husika.

Vingine ni maoni ya viongozi wa kata zote katika jimbo, ambapo kwa Kalenga walishiriki wajumbe zaidi ya 450, na kigezo cha mwisho ni maoni ya utafiti na haiba ya wagombea kwa kushirikiana na sababu za kiusalama zinazoletwa na idara ya usalama ya chama.

Mbowe aliweka bayana kuwa wagombea wote 13 waliojitokeza walipewa fursa kwenye Kamati Kuu kujieleza, kisha kupewa nafasi wao wenyewe wachague wanaona nani anafaa kupeperusha bendera ya CHADEMA.

Aliongeza kuwa katika mchakato huo, wagombea hao walimchagua Grace, na Kamati Kuu ililiridhia.

Mbowe alisema Grace ndie mgombea wa chama hicho na si yule aliyeandikwa na vyombo vya habari hivi karibuni, Lucas Sinkala ambaye ni ofisa wa sheria wa chama hicho katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Akizungumzia uamuzi huo, Sinkala ambaye awali aliteuliwa na wajumbe wa wilaya kwa kura, alisema anaunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu.

Alisema anaona hoja ya msingi ni mabadiliko yanayohitajika Kalenga, ambayo yataletwa na CHADEMA bila kujali ni mwanaCHADEMA yupi.

“Ghala letu limevamiwa na panya kwa miaka mingi, hivyo katika kuwaondoa panya hatuangalii rangi wala jinsia ya paka, tunataka panya watoke, mimi namuunga mkono Grace Tendega na nitamsaidia katika kampeni hadi tufanikiwe kukiondoa Chama Cha Mapinduzi,” alisema Sinkala.

Grace aliwahi kugombea ubunge wa jimbo hilo mwaka 2005, kupitia Jahazi Asilia, ambapo alipata kura zaidi ya 13,000 akiwa mshindi wa pili nyuma ya mgombea wa CCM.

Mgogoro wa madiwani wa Arusha

Katika kikao hicho, Mbowe pia alisema Kamati Kuu imeondoa pingamizi la madiwani wa Jiji la Arusha, la kususia vikao vya jiji hilo vinavyoongozwa na meya aliyepatikana kutokana na uchaguzi batili ambao serikali imeshindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro huo uliosababisha mauaji mapema mwaka 2011.

“Kamati Kuu imewaagiza madiwani waende Arusha, wawaambie wananchi wa Arusha kuwa wameruhusiwa sasa kuhudhuria katika vikao, kudhibiti mianya yote ya ufujaji wa mali za umma unaofanywa na CCM na meya wao na kamwe wasitoke katika vikao,” alisema Mbowe.

Bunge la Katiba

Chama hicho kimesema kuwa wamepokea kwa masikitiko uteuzi wa wajumbe wa Bunge la Katiba uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete.

Kwamba sasa ni dhahiri kuwa rais na chama chake, hawana nia njema ya kutaka katiba mpya, bali kupata katiba yenye mawazo ya ki-CCM kwani katika uteuzi huo ameteua wajumbe ambao ni makada wa CCM kwa asilimia 75-80.

Mbowe alisema CHADEMA wapo tayari kushirikiana na wajumbe wote bila shida, lakini ikitokea CCM wanatumia vibaya wingi wao bungeni ili kupitisha mambo kinyume na ilivyopendekezwa na tume, basi CHADEMA watasusia Bunge ili CCM ipitishe katiba yao ambayo itakuwa sio katiba ya wananchi. Mbowe aliwataka wajumbe wote wa CCM wasitumie vibaya uwingi wao ila wazingatie matakwa ya wananchi na kuyaheshimu.

Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company