
Kiongozi wa waandamanaji Ukraine
Dmytro Bulatov alionekana kwenye runinga juma lililopita sikio lake likiwa limekatwa na akiwa na jeraha usoni, akadai kuwa alitekwa na watu asio wajua na kuteswa kwa siku nane .
Hali yake iliibua hamaki miongoni mwa maelfu ya waandamanaji wanaomtaka rais Viktor Yanukovych ajiuzulu.

Yamkini Bulatov ni mmoja kati ya kundi la wamiliki wa magari wa AutoMaidan wanaokisiwa kuhusika na maandamano yanayoendelea katika ukumbi mkubwa wa Maidan square jijini Kiev.
Kiongozi wa upinzani Vitali Klitschko alisema viongozi wa muungano wa Ulaya ndio waliofanikisha matibabu ya Bulatov nje ya Ukraine baada ya kusikia kuwa aliteswa na watekaji wake .
Serikali inadaiwa ilituma maafisa wake kumkamata akiwa amelazwa Hospitalini lakini wafuasi wake wakawazuia.
Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Ukraine Leonid Kozharahata amepuuzilia mbali madai ya kutekwa na kuteswa kwake akisema ni uwongo mtupu .