JK awafyatua wasaka urais; Ahoji walikuwa wapi hadi wagawe rushwa sasa, Atetea mawaziri ‘mizigo’, adai CC ilitimiza wajibu

RAIS Jakaya Kikwete amewaponda wanasiasa wanaopigana vikumbo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakisaka uongozi kwa rushwa ya fedha na vijizawadi kwa wananchi, akihoji walikuwa wapi wakati wote.
Pamoja na kutowataja kwa majina walengwa, ni dhahiri Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alikuwa akiwalenga vigogo waandamizi walioshambuliana kwenye vyombo vya habari wakitetea makundi yao ya urais 2015 na kutupiana tuhuma kuhusu mwenendo wao wa kukivuruga chama.

Kwa takribani wiki nzima iliyopita, yamejitokeza makundi mawili; la wafuasi wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa likijibu mapigo ya kundi jingine linaloitetea Sekretarieti ya CCM na kumshambulia mwanasiasa huyo kuwa anakivuruga chama na hana sifa za kuwa rais mwaka 2015 kwa kuwa anaendesha kampeni kabla ya wakati.

Akihutubia mkutano mkubwa jana jijini Mbeya uliorushwa moja kwa moja na redio na televisheni katika maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM, Kikwete alionyesha kuwashangaa viongozi wa chama hicho wanaotembeza rushwa ya fedha na zawadi kwa wanachama ili kuwashawishi wawachague.

Alisema kuwa japo chama kinahitaji kusaidiwa, lakini lazima wanachama wawe makini na misaada inayotokana na fedha chafu na za ruswa.

“Mnapomuona mtu anajitolea kipindi hiki anagawa rushwa na zawadi, muulize ulikuwa wapi miaka yote hadi aje kujitolea leo kwa kisingizio kwamba anaimarisha chama,” alisema.

Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa chama kimeunda kamati ya usalama na maadili ambayo itakuwa na kazi ya kuwabana wanachama wanaokiuka maadili ya chama.

Hata hivyo, pamoja na Rais Kikwete kukemea michezo hiyo michafu ya rushwa ndani ya chama, hali hiyo ndivyo ilivyojitokeza wakati wa mchakato wa kumsaka mgombea urais mwaka 2005 ambapo aliibuka kidedea.

Baadhi ya makada ambao ni wafanyabiashara maarufu waliokuwa katika mtandao wa Rais Kikwete mwaka 2005, wanadaiwa kuendesha mbinu za rushwa ili kumpigia debe aungwe mkono, jambo ambao sasa linaendelezwa na wale wanaosaka nafasi hiyo.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alizima mjadala wa sakata la la mawaziri waliotajwa na chama chake kuwa mizigo, lakini akawateua tena, akisema kuwa haikuwa lazima kwamba wafukuzwe kazi.

“Kuna watu walitaka niwafukuze kazi na sasa yameibuka malumbano kwamba waliitwa na kuhojiwa Kamati Kuu (CC), lakini sikuwafukuza. Si lazima ufukuzwe kazi baada ya kuhojiwa,” alisema.

Alisema kuhojiwa Kamati Kuu ilikuwa ni sehemu ya haki yao ya kusikilizwa kwani inawezekana wao walifanya kazi zao vizuri, lakini sababu ikiwa ni serikali haijawapa fedha.

“Kamati Kuu imetimiza wajibu wake, kazi sasa imebaki kwa serikali,” alisema Kikwete.

Aliongeza kuwa wamepewa mikakati kuhusu jinsi watakavyoyapatia ufumbuzi matatizo hayo ikishindikana mabadiliko yanaweza kufanyika.

Katika hatua nyingine, Kikwete aliwakemea viongozi wa chama hicho na kuwaambia ni lazima waende kwa wananchi badala ya kukaa maofisini kitendo alichokiita kuwa kinapunguza imani ya wanachama.

Alisema kiongozi mzuri ni yule anayekwenda kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia majawabu katika kipindi muafaka.

Pia aliwataka viongozi wa chama hicho kuwa waadilifu, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea chaguzi za serikali za mitaa, na kubwa zaidi kujiepusha na rushwa katika uteuzi wa wagombea.

Hata hivyo, viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho wengi hawakuonekana, ingawa hakuna ufafanuzi wowote uliotolewa kuhusu kutokuwepo kwao.
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company