
Katika taarifa, UNHCR imesema wakimbizi Wasomali wanaoshikiliwa wanapaswa kulindwa na kutokamatwa kiholela. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Joseph Ole Lenku amenukuliwa akisema zaidi ya watu 4,000 wamekamatwa katika siku za hivi karibuni. Kati ya wanaoshikiliwa katika oparesheni ya vikosi vya usalama Kenya ni zaidi ya Wasomali 1,000 ambao imeripotiwa wanazuiliwa katika uwanja mmoja wa michezo mjini Nairobi. Kuna ripoti kuwa waliokamatwa hawana chakula, maji na dawa katika uwanja huo. Vikosi vya usalama Kenya vinatekeleza oparesheni kubwa ya kiusalama yenye lengo la kuwasaka magaidi kufuatia hujuma za kigaidi katika miji ya Nairobi na Mombasa. Kundi la kigaidi la Al Shabab limenukuliwa mara kadhaa likisema litatekeleza hujuma Kenya kulipiza kisasi uingiliaji wa jeshi la Kenya nchini Somalia. Wanajeshi wa Kenya wako Somalia kama sehemu ya Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Afrika (AMISOM) ambavyo viko Somalia kupambana na kundi la al-Shabab.