Tumeachia itikadi za kisiasa zifanye kazi, tutakosa Katiba bora


Mchakato wa Katiba mpya unaoendelea nchini hauonyeshi dalili njema baada ya mijadala yake kuanzia kwa wananchi hadi ndani ya Bunge Maalumu kutawaliwa na hisia za itikadi za vyama badala ya utaifa.

Tangu mwanzo kuanzia utungaji sheria ya Katiba mpya, mchakato huo umegubikwa na misimamo kiitikadi. Jambo lililo wazi ni kwamba itikadi na misimamo ya kisiasa haitatupatia Katiba bora.

Ikumbukwe kuwa Katiba bora ni yenye kujenga taasisi imara na kuunganisha Taifa.

Katiba bora tunayotaka ni ile inayounda na kujenga taasisi imara na kuunganisha Taifa huku uamuzi wote ukitanguliza masilahi ya umma badala ya itikadi, utashi au nguvu ya viongozi. Tuseme kweli kwamba katika Tanzania tunataka Katiba inayosimamia matakwa ya watu wote, vitu vyote na mambo yote.

Tunataka taasisi imara na zenye nguvu na Katiba ya aina hii ndiyo yenye uwezo wa kutuhakikishia sisi katika Tanzania tunayoitaka katika nyanja zote kiuchumi, kisiasa na kijamii.


Tunahitaji Katiba itakayounda taasisi imara ya kimahakama, vyombo imara vya ulinzi na usalama na vinavyowajibika na kulinda masilahi ya umma badala ya vyama tawala.


Katiba inayotufaa ni inahakikisha nafasi za uongozi katika mamlaka, ofisi na taasisi za umma zinapatikana kwa kuzingatia taaluma, weledi, uwajibikaji na uadilifu badala ya ukada, uswahiba na kulipana fadhila.


Wenzetu Kenya, kwa mfano, Katiba yao mpya imeunda vyombo vya kusimamia uendeshaji wa mahakama, vyombo vya dola na ofisi zote za umma ndiyo maana hivi karibuni tumeshuhudia majaji wakiwemo wa mahakama za rufaa wakichunguzwa, kuhojiwa na kuchukuliwa hatua kwa uamuzi mbaya au upungufu kwenye utendaji wao.


Katiba yetu lazima iweke misingi na miongozo inayombana yeyote anayekabidhiwa dhamana ya uongozi bila kujali chama chake wala itikadi yake.


Katiba ya aina hiyo haiwezi kupatikana kupitia mijadala yenye misingi ya itikadi iliyojaa kejeli, matusi, dhihaka, ubaguzi, kubezana na hila kama inayofanyika Dodoma hivi sasa.


Katiba bora itapatikana kwa maridhiano ya wote na siyo kwa makundi kama inavyojitokeza hapa kwetu


Kwa sababu katiba ni zao la jamii, ni lazima ipatikane kwa misingi ya maridhiano, kuaminiana na kuheshimiana katika mambo ya msingi kitaifa bila kujali tofauti zetu.


Naamini Katiba bora inayopatikana kwa maridhiano itatujengea misingi ya sheria zenye nguvu na uwezo wa kuwadhibiti viongozi wanaokiuka miiko, tamaduni, mila na desturi zetu kama Taifa.


Katiba bora itawazuia viongozi wetu kutuongoza kwa mapenzi yao, hisia zao au matakwa ya vyama vyao.


Tunataka Katiba inayotoa na kuweka dira ya uongozi kwa yeyote anayekalia ofisi ya umma bila kujali chama chake, mapenzi wala utashi wake.


Hatutaki Katiba ya CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP, UDP, DP, Demokrasia Makini, PPT-Maendeleo au chama chochote cha siasa kilichopo sasa au kitakachokuja, bali tunataka Katiba ya Taifa inayobeba na kujali ajenda na masilahi ya makundi yote.


Ulinzi, kugawa na kufaidi rasilima za Taifa pia ni mambo ya kuzingatiwa tunapoandika Matiba Mpya.


Tutambue kuwa Katiba inayotufaa ni ile itakayotuhakikishia ulinzi na haki ya kumiliki, kufaidi na kutumia rasilimali za Taifa ikiwemo ardhi kwa faida yetu sote, badala ya hali ilivyo sasa ambapo licha ya kujaaliwa ardhi na rasilimali nyingine, wajanja wachache ndio huifaidi.
              psaramba@gmail.com, +255 766 434 354.
CHANZO MWANANCHI MTANDAONI
Share this article :
 
Support : Creating Website | SAMBA Template | HAKI LEO Template
Copyright © 2011. HAKI LEO - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by HAKI LEO Template
Imewezeshwa na Haki Leo Company