London, England. Kocha Jose Mourinho amesema kudaka mipira migumu na kuondoa hatari nyingi langoni kwake kumemfanya kipa wa Atletico Madrid, Thibaut Courtois kuiondoa Chelsea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi usiku.
Courtois alichupia upande wa kushoto kuokoa mpira wa hatari wa kichwa uliopigwa na nahodha wa Chelsea, John Terry wakati timu zikiwa zimefungana bao 1-1.
Dakika chache baadaye, mshambuliaji Diego Costa alifanikiwa kupata penalti na kuiandikia Atletico bao la pili kabla ya Arda Turan kufunga la tatu.
“Dakika moja katika kipindi cha pili iliamua kila kitu,” alisema Mourinho. “Dakika ambayo kipa wa Atletico alipoupangua mpira wa hatari wa kichwa wa John Terry, kisha na penalti, viliua kabisa mchezo.
“Na baada ya pale kulikuwa na timu moja ambayo ilikuwa na morali ya juu, ikijua kwamba kuna nusu saa ya kufanya kazi ya kuwapeleka fainali.
“Kwa dakika 60, tulikuwa na mchezo mkononi, lakini nusu fainali nyingi na mechi muhimu zinakuwa na vitu vya msingi, ambavyo ndiyo hivi sasa.
“Hongera kwao kwa sababu ni timu nzuri na kile ambacho wanakifanya katika Ligi Kuu ya Hispania ni cha kushangaza mno.”
Nyota wa kimataifa wa Ubelgiji, Courtois (21), alikuwa akicheza mchezo wake wa 150 akiwa na Atletico katika msimu wake wa tatu mfululizo akiwa kwa mkopo kutoka Chelsea, timu ambayo hakuwahi kuichezea.
Aliisaidia timu hiyo ya Jiji la Madrid kucheza fainali za kwanza ya Kombe la Ulaya tangu miaka 40 iliyopita, huku wakiongoza Ligi Kuu ya Hispania wakiwa wamebakiza michezo mitatu.
Atletico Madrid iliitupa nje ya mashindano Chelsea baada ya kuichapa mabao 3-1 katika mechi ya marudiano ya nusu fainali juzi kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha timu hizo wiki iliyopita mjini Madrid, hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.
Atletico sasa itakutana na Real Madrid, ambayo pia ina uwezo wa kutwaa ubingwa wa Hispania, katika fainali itakayochezwa jijini Lisbon, Ureno Mei 24.